TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

 
Wakati bado msimamo wa Wajumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Ukawa ukiwa haufahamiki kama watarejea bungeni kuendelea na vikao hivyo mwezi Agosti au la, mjadala wa katiba mpya umechukua sura mpya, baada ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, kuungana na viongozi wa CCM kukibeza kikundi hicho.
Kwa kauli hiyo, Spika Kificho anaungana na Mawaziri wa SMZ katika kubeza uamuzi huo wa Ukawa, ingawa yeye akaenda mbali zaidi na kumtupia lawama Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akieleza kuwa alimlisha maneno.
Kificho kwa mara ya kwanza amechomoza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika Uwanja wa Kwamabata eneo la Magogoni na kusema hakukuwa na uamuzi wa pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kupendekeza Serikali tatu. Akasema dai hilo lilichomekwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba iliyokusanya maoni ya watu kuhusu katiba.
 
Kificho amewaeleza wananchi kuwa yeye amezaliwa ndani ya Afro Shiraz (ASP), akalelelewa na kukulia CCM, hivyo hathubutu, hatathubu na hakuthubutu kusaini waraka wa kutaka mamlaka huru ya Dola ya Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mara nyingine Kificho anaonekana kusafisha upepo mchafu uliokuwa ukivuma na kutaka kumpeperusha ndani ya chama chake huku baadhi ya wanachama na viongozi wenzake, wakimtaja kama mtu aliyeshiriki kutaka kuwasaliti na kuwazunguuka mbuyu.
Madai ya awali ya viongozi wenzake akiwemo Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar upande wa CCM Salmin Awadh Salmin, yanamtupia lawama Kificho na kumpasha hakukuwa na kikao chochote kilichoketi na kupitisha azimio la BLW kutaka Serikali tatu au mamlaka kamili ya Zanzibar nje Muungano uliopo.
Mvutano huo ulioibuka nje ya Bunge la Katiba, huenda ndiyo ulioambukiza mipasho, piga nikupige ya maneno na kutupiana vijembe vikali kati ya wabunge wa Bunge la Katiba wa CCM na CUF kabla ya kundi la Ukawa halijaamua kuliacha bunge na kusema wamechoshwa na matusi, kejeli na ubaguzi.
Kificho akihutubia mkutano wa hadhara, akasema amekuwa Mwakilishi wa CCM Jimbo la Makunduchi kwa miaka saba, akawa spika miaka 19, akijinasibu kuwa ni spika mzoefu baada ya Chifu Adam Sapi Mkwawa, kufika kwake alipo sasa kumetokana na nguvu za CCM, hivyo hana jeuri ya kusaliti sera za chama chake.
 
Akizungumza kwa kujiamni na kujiosha, akamtupia shutuma Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba akisema kuwa ndiye aliyemwandalia fitina hiyo.
Hata hivyo, waraka ulioandikwa na kusainiwa na Spika Kificho umeandikwa na kutaja bayana kuwa Azimio la BLW Zanzibar ni kuhitaji mamlaka huru ya Dola, jambo ambalo limechukuliwa na wengi kama linalohitaji serikali yenye mamlaka kamili Zanzibar.
Kificho anasema kilichomo kwenye waraka huo ni hitaji la kufanyika marekebisho na mageuzi makubwa ya msingi ili kuipa Zanzibar nyenzo za kujijenga kiuchumi na kujitegemea ijiendeshe kwa kusimamia mambo yasiokuwa ya Muuungano kwa uwazi na si kupigania mamlaka huru ya Dola .
Pia ameeleza kuwa katika moja ya waraka huo kulikuwa na kosa la kitaalamu katika uandikaji na tafsri ya kila anayeusoma kutoa fasiri aitakayo, lakini si kusudio la BLW au lake kutaka mamlaka huru ya Dola.
 
Chanzo Mwananchi

0 comments :

 
Top