TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

       
Hivi Ukawa hii ni mara ya kwanza wamesusa? Mbona tunalifanya kana kwamba hili ni jambo jipya? Pia, vyombo vyetu vya habari vimetengeneza picha kana kwamba hili ni jambo jipya, la hasha, kilichotokea kwa ukawa ni kupigia mstari msimamo waliouchukua awali. Juzi, Ukawa waliongeza ukubwa maneno katika sentensi ileile ya mwanzo, kwamba mchakato huu una matatizo na hakuna anayeonekana kutaka kushirikiana kutatua matatizo hayo.
Mimi binafsi pamoja na waliokuwa makamishna wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba msimamo wetu uko palepale, kwamba tuna matatizo makubwa katika mchakato huu na matatizo hayo yameletwa kwa sehemu kubwa na vyama vya siasa pamoja na wengi wetu kudhani kazi yetu iko kwenye Kura ya Maoni peke yake.
Sababu zilizowatoa Ukawa nje ya Bunge Maalum hivi ziliwahi kujadiliwa na kutatuliwa? Kama hapana, sasa kwa nini Ukawa washiriki kupakua chakula ambacho wao wanaamini siyo kizuri kwa matumizi ya binadamu? Nazungumza hili kwa sauti.
Unajua hata Ukawa wanaweza kuwa hawajui nguvu kubwa waliyo nayo, wakijitambua kwamba wana nguvu wanaweza kuanza kuleta ahueni kwa nidhamu ya kisiasa inayopotea kwa kasi, kuna wakati huwa nina shaka kama kuna uelewa huu miongoni mwa wana Ukawa.
Nikupe mfano mdogo tu, baada ya makubaliano ya Rais na TCD ambayo yakasomwa kwetu kwa umahiri mkubwa na John Momose Cheyo tena akiwa meza moja na wawakilishi wa vyama vyote, nini kimetokea baada ya makubaliano hayo kutupiliwa mbali?
Pia, mimi nilipata kusema kama hawatasema kitu nitatafakari kiwango cha heshima yangu kwao, sasa angalau Profesa Lipumba na wenzake wamenawa mikono na kusema hawatashiriki dhambi, sasa ni wakati wa kumkumbusha John Momose Cheyo kuhusu makubaliano yale, vipi, kulikoni?
Kwa msomaji anayefuatilia makala hii, baada ya Ukawa kususia Kura ya Maoni, aliyebaki sasa kuweka rekodi sawasawa siyo mwingine bali ni Mwenyekiti wa TCD ambaye aliratibu makubaliano na Rais atueleze iwapo makubaliano bado yapo au hayapo. Hivyo na yeye kama ‘Pilato’ aungane mkono kunawa maji. Akikaa kimya ataanza kuharibu taswira ya chama chake kwamba ni cha watu wasiothubutu, waoga, hawapaswi kuaminiwa au hata kupewa dhamana kwa nafasi yoyote ile na kwamba mkikubaliana nao wanaweza pia kupuuza makubaliano hayo na wakabaki na amani mioyoni mwao.
Bila kuweka masilahi ya chama ambacho mimi ni mwanachama na ieleweke kwamba chama chetu ninakipenda, hasa misingi yake na mimi ni mwanachama mkazi wa kudumu. Leo, kesho au siku za mbele, naomba niungane mkono kusema walichofanya Ukawa ni kitendo cha uzalendo.
Ukawa wanajaribu kuturejesha mezani kwa kila namna licha ya kwamba wanaonekana ni wanajipanga, hawana uwezo, ni dhaifu, ni wapiga kelele, hawana jipya na kadharika.
Turejee mezani tukaondoe tofauti zetu, tukaimarishe umoja wetu, tukajenge mwafaka wa kitaifa, tukafanye maridhiano na tukajenge uelewa wa pamoja juu ya Mchakato wa Kupata Katiba Mpya. Sifa hizi nimezitoa nikihusianisha jitihada zao pia katika mchakato wa kupata Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi na siyo kwa zile harakati za kuelekea Magogoni ambazo wao au chama chetu tabia zao ni zilezile.
Source Mwananchi

0 comments :

 
Top