TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

KATIBU Myeka wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Samweli Kasori, amepokea vitisho kutoka kwa watu kadhaa baada ya uamuzi wake wa ‘kufukua’ ukweli uliofichika, baada ya baadhi ya wanasiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kulihusisha jina la Mwalimu Nyerere na mbio zao za urais. Hali hiyo inajitokeza ikiwa ni siku kadhaa tangu Mzee Kasori kunukuliwa na gazeti dada na hili la Raia Tanzania, kwamba baadhi ya wanasiasa wanatumia vibaya jina la Mwalimu Nyerere kwa malengo yao. Gazeti la Raia Tanzania lilimnukuu Kasori, ikiwa ni siku kadhaa kupita tangu Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba, anayedaiwa kuwamo kwenye kambi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kunukuliwa na gazeti hilo la Februari 10, mwaka huu, akidai kabla Mwalimu Nyerere hajaaga dunia alimkubali (aliridhika na) Lowassa. “Ni kweli kwamba jina la Lowassa lilikatwa na Mwalimu kwa sababu mbalimbali, lakini Rais Mkapa alipotangaza Baraza lake la Mawaziri mwaka 1995, baada ya miaka miwili tu mwenyewe akaona kuna upungufu; akaamua kumuingiza Lowassa katika Baraza la Mawaziri. Ninaamini Mkapa alipewa ushauri na Mwalimu Nyerere,” alinukuliwa Komba. Vitisho dhidi yake Baada ya gazeti hilo la Raia Tanzania kuchapishwa likimkariri kujibu sehemu ya madai ya Komba, Mzee Kasori aliwasiliana na chumba chetu cha habari kueleza vitisho alivyopata kutoka kwa mmoja wa watumishi serikalini (jina lake na taasisi inahifadhiwa). Katika vitisho hivyo vilivyotolewa kwa njia ya simu kwake, Kasori anatakiwa kuacha kuharibu mipango ya maisha ya watu (hata hivyo, gazeti hili halikuweza kubaini mara moja mipango hiyo inayovurugwa ya maisha ni ya nani hasa). Taarifa zaidi kutoka vyanzo vyetu kadhaa vya habari kutoka serikalini zinaeleza kwamba, Mzee Kasori amechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzitaarifu baadhi ya mamlaka za juu serikalini. “Salaam, leo Alhamisi Februari12, 2015, saa 4:45 asubuhi nimepokea simu kutoka kwa (anamtaja mtumishi wa serikali) akilalamika kwamba namharibia (anataja jina la mwanasiasa) shughuli zake za kutafuta maisha katika kuwania (anataja nafasi ya uongozi wa dola),” inaeleza sehemu ya ujumbe wa Mzee Kasori kwenda katika moja ya mamlaka za juu serikalini. Ujumbe huo unaendelea kueleza; “Kweli huyu Mungu mpya aitwaye fedha ana nguvu za ziada ndani ya akili na mioyo yetu.” Alichokisema Mzee Kasori Kwa kuzingatia maelezo ya Komba kama yalivyonukuliwa awali, gazeti la Raia Tanzania lilimtafuta Kasori, mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa karibu wa Mwalimu Nyerere, ambaye aliweka bayana kwamba, haamini kama Mwalimu Nyerere aliridhishwa na Lowassa kama alivyodai Komba. “Haya masuala nilikwishayaeleza yote na kuyaweka kwenye mtandao. Siogopi nilikwishayaweka wazi,” alianza kueleza Mzee Kasori. Katika maelezo yake hayo, Kasori anaendelea kusema: “Tanzania nzima mtakumbuka kuwa huyu Mheshimiwa Edward Lowassa alikuwa ni mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais mwaka 1995 na akaenguliwa kwa hoja nzito ya kutokuwa muadilifu na Baba wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere, kwa ukweli (wala sio tuhuma) kuwa alikuwa amejilimbikizia mali nyingi kwa kipindi kifupi ndani ya CCM na Serikali. Muda mfupi alikuwa ni mtumishi wa CCM, muda mfupi kama Mkurugenzi wa kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha. “Mara baada ya kurudi Butiama, 1995, baada ya kuenguliwa kugombea nafasi ya urais, siku moja mapema asubuhi Bwana Lowassa alinipigia simu na kusema yafuatayo: “Bwana Kasori, naomba uende kumwambia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aende Monduli kusaidia kusafisha jina langu ili nisikose ubunge kutokana na yale aliyonisema Dodoma’. Nilishikilia mkono wa simu (TTCL) kwa zaidi ya nusu saa tukiwa tunazungumza na hatimaye mimi nilipata ujasiri wa kumwambia Bwana Lowassa kuwa siwezi kwenda kusema maneno hayo kwa Baba wa Taifa na kwamba akitaka aje Butiama na nitamruhusu waongee ana kwa ana. Nikanyamaza na hatimaye yeye akawa wa kwanza kukata simu. Hiyo ikawa itifaki njema kwangu! “Kesho yake tena asubuhi nilipokea simu, safari hii akawa ni Mheshimiwa Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwa maneno yake alisema, Bwana Kasori, jana ulizungumza na Edward Lowassa, naomba ufikishe ombi lake kwa Baba wa Taifa tafadhali” “Kutokana na heshima ya Mheshimiwa Mzee Kawawa, nilikubali na nikaenda na kabla ya hapo nilimuomba Mzee Kawawa akae karibu na simu ili nimpe jibu muda si mrefu. “Nilimueleza Baba wa Taifa kuwa, Mheshimiwa Edward Lowassa kupitia kwa Mheshimiwa Mzee Rashidi Mfaume Kawawa anaomba usaidie kusafisha jina lake kule jimboni kwake Monduli ili asikose ubunge kutokana na yale uliyomsema katika Kamati Kuu ya CCM Dodoma. Jibu la Baba wa Taifa alilonipa ni kuwa, nenda umwambie Mzee Rashidi Mfaume Kawawa asiwe mjinga kama Lowassa”! “Kwa kuzingatia heshima kati ya wazee hao wawili, Kawawa sikumwambia hivyo! Badala yake nilimdanganya (nawaomba radhi tena Watanzania) jibu nililompa Mzee Kawawa ni kuwa juma lililokuwa linafuata tungekuwa Dar es Salaam na kwamba aje Msasani aongee na Baba wa Taifa. Mheshimiwa Kawawa alikubali. “Nikarudi kwa Baba wa Taifa kusema uongo (naomba radhi tena) kuwa, Mzee Kawawa ameomba mzungumze tatizo la Lowassa tutakapofika Dar es Salaam. Baba wa Taifa alikubali na akaagiza nimuombe Mheshimiwa Mzee Kawawa kuwa Lowassa na Guninita na wapambe wengine wa Lowassa wote wafike Msasani. “Siku ya siku ikafika. Tukawepo Msasani na Mheshimiwa Mzee Kawawa akaja. Lowassa hakuwepo! Sababu anazijua mwenyewe (muulizeni maana nasema ukweli). Mkutano ulipoanza mzungumzaji wa kwanza nikawa mimi, kueleza lengo la mkutano. Mzungumzaji wa pili alikuwa Baba wa Taifa na swali la kwanza ni kuuliza Lowassa yuko wapi? “Bila kupoteza wakati Mwalimu alisema, Rashidi, huyu Kasori ananiambia eti niende Monduli nikasafishe jina la Mheshimiwa Lowassa eti asikose ubunge kwamba nilimchafulia Dodoma katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM. Kutokana na ombi lako nilimtuma akuambie usiwe mjinga kama Lowassa. Kasori alikuambia eh?” “Oneni, huko nyuma tayari nilishasema uongo kwa kutosema maneno hayo kwa Mheshimiwa Mzee Kawawa. Kweli hilo kurudiwa na Baba wa Taifa kwa Mzee Kawawa mbele yangu lilisababisha kalamu yangu kuanguka, nikatetemeka na nikatokwa na jasho jingi mbele ya hao wazee! Bila kutegemea na kwa mshangao mkubwa Mheshimiwa Mzee Kawawa alikubali kwa kuitikia “NDIO ALINIAMBIA”. Mwalimu akacheka sana! Sababu sijui hadi leo kwa nini alicheka sana. “Kwa kuendelea, Mwalimu alimwambia Mzee Kawawa kuwa, Kasori ana umri mkubwa kuliko Lowassa. Kasori alipata taabu sana kufikisha kwangu ombi la Lowassa na aliniambia kuwa jana yake alikuwa amekataa ombi la Lowassa. Sasa nasema kuwa kwa umri wangu mimi mzee, Lowassa ni mtoto wangu tena mdogo sana. Kwa heshima mliyonayo kwangu na kwa Chama cha Mapinduzi mtanishangaa sana mkisikia niko Monduli eti nipo kwenye majukwaa nasafisha jina Bwana Lowassa asikose ubunge. “Kweli Lowassa ni jasiri sana kusema maneno hayo. Hayo ningeambiwa na Kasori tu ningesita kumuamini. Lakini kwamba hata wewe Rashidi ulitumiwa kusema maneno hayo! Huyu Lowassa ni jasiri sana! Lakini kwa nini hajatuambia ukweli kuhusu mali hizo ambazo ni nyingi kuliko mimi ambaye nimekuwa Rais wenu kwa kipindi kirefu? Sasa Bwana Rashidi, nakuomba hivi, kamwambie mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Mwinyi aitishe wajumbe wote wa Kamati Kuu, chagueni tarehe na mahali popote Tanzania, mimi nitakuja kumsafisha Bwana Lowassa na nitagharamia mkutano huo kwa hela zangu. Kamwe msitumie hela za chama wala serikali. Monduli sitokwenda, umesikia eh?” “Mkutano ukaisha hapo Msasani. Hadi uchaguzi 1995, unafanyika na kumalizika Baba wa Taifa hakwenda Monduli. Alichukia sana tabia za Lowassa. Hadi Baba wa Taifa anafariki, sikuwahi na sijasikia wala kusoma popote ambapo Lowassa anakanusha alivyolimbikiza mali akiwa mtumishi wa CCM na serikali kwa muda mfupi kiasi cha kumzidi Rais wa Kwanza,” alidai Mzee Kasori. 

Source Raia Mwema

0 comments :

 
Top