TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


Pretoria. Gharama za maisha zimepanda katika Kijiji cha Qunu atakakozikwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika, Neslon Mandela na sasa chumba cha kulala kwa siku kinatozwa hadi Randi 8,000 kwa siku sawa na Sh1.4 milioni.

Habari kutoka Qunu, Mthatha katika Jimbo la Eastern Cape zinasema fedha zinazotozwa sasa ni karibu mara 20 zaidi ya gharama za kawaida ikiwamo vyumba vya kulala.

Kwa kawaida, gharama za vyumba ni kati ya Randi 400 na 500, lakini vimepanda zaidi kutokana na idadi kubwa ya watu kufika Afrika Kusini hasa kwenye mji wa Qunu ambako ndiko maziko yatafanyika.

Baadhi ya wakazi wa Qunu wameyahama makazi yao na kuwapangisha waandishi wa habari na watu wengine ambao wamepiga kambi kwa siku kadhaa katika kijiji hicho wakifuatilia msiba wa Mandela ambaye atazikwa keshokutwa, Jumapili.

Iliilazimu Idaya ya Utalii katika eneo hilo kuingilia kati na kutoa maelezo kwa wamiliki wa nyumba za wageni na hoteli kutopandisha bei za huduma kiasi cha wageni kushindwa kuzimudu.

Hali ilivyo ni tofauti na ahadi iliyotolewa na uongozi wa Wilaya ya OR Tambo ambao ulisema katika taarifa yake kwamba: “Tumejiandaa kuhakikisha kwamba tunamudu idadi kubwa ya wageni wanaotarajiwa kuwapo kwenye maziko ya Mandela”.

Juzi Meya wa wilaya hiyo, Nomakhosazana Meth alisema pamoja na mambo mengine pia wamejiandaa kuukabili msongamano wa magari na kwamba kutakuwa na barabara mbadala ambazo zitatumika.

Alisema maadalizi kwa ajili ya mazishi yamekamika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jukwaa ambalo litawekwa mwili wa Mandela wakati wa kutoa heshima za mwisho na maziko.

Polisi na wanajeshi wameendelea kuimarisha ulinzi nyumbani kwa Mandela, ikiwa ni pamoja na kufunga barabara zote zinazoingia katika lango kuu la makazi ya kiongozi huyo.

Polisi pia wamefunga kilometa kadhaa za Barabara Kuu ya N2 ambayo inaingia na kutoka Qunu.

Meya alisema kumekuwa na mabadiliko ya matumizi ya Hospitali ya Mthatha ambayo hivi sasa inasimamiwa na Jeshi la Afrika Kusini (SADF) na kwamba wagonjwa wote wamehamishiwa katika hospitali nyingine isipokuwa wale mahututi.

Jana Uwanja wa Ndege wa Mthatha ulifungwa na hakuna ndege zozote za kiraia zitakazoruhusiwa kutua isipokuwa zile zitakazowapeleka viongozi na wageni mashuhuri

Source: Mwananchi

0 comments :

 
Top