Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inaanza kusikiliza kesi ya kikatiba ya Bunge Maalumu la Katiba.
Kesi hiyo inaanza kusikilizwa siku mbili baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya kusimamisha kwa muda vikao vya Bunge vinavyoendelea Dodoma. Kesi hiyo, Namba 28 ya mwaka 2014 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilifunguliwa na mwandishi wa habari, Saidi Kubenea.
Katika kesi hiyo, Kubenea anaiomba mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011. Pia, Kubenea anaiomba Mahakama itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo, Kubenea pia alifungua maombi ya kutaka mahakama hiyo itoe zuio la muda la kusimamisha bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Hata hivyo, maombi hayo Namba 29 ya mwaka 2014 yalitupiliwa mbali na Mahakama Kuu juzi baada ya kukubaliana na hoja moja tu kati ya tatu zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu.
Jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija (kiongozi), Dk Fauz Twaib na Aloyisius Mujulizi, lilikubaliana na hoja kuwa maombi hayo yalifunguliwa chini ya kifungu cha sheria kisicho sahihi.
Baada ya kutupilia mbali maombi hayo ndipo mahakama ilipanga kusikiliza leo kesi hiyo ya msingi. kwa wakati mmoja pingamizi hilo la Jamhuri na kesi ya msingi kufuatia maombi yaliyotolewa na wakili wa Kubenea, Kibatala.
Wakili wa Kubenea, Peter Kibatala aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe ya karibu ya kusikiliza pingamizi la Jamhuri na pia akaiomba isikilize kwa pamoja pingamizi hilo na kesi ya msingi, kulingana na umuhimu na uharaka wa shauri hilo.
0 comments :
Post a Comment