Maambukizi
Katika Njia ya Mkojo (UTI) ni moja kati ya magonjwa ambayo hayapewi msisitizo
wa kutosha katika jamii licha ya kuwa wengi huathirika kwa ugonjwa huu bila
kujua chanzo, tiba na kinga yake.
Ugonjwa huu
huanza kuathiri mirija inayopitisha mkojo, baadaye huenea katika kibofu na
figo. Mgonjwa anaweza kupata ugonjwa sugu wa figo na kupoteza maisha kama
ugonjwa huu hautatibiwa mapema.
Wataalamu wa
afya wanasema UTI husababishwa na vimelea ambao huingia kupitia mirija
inayosafirisha mkojo na kuutoa nje. Vimelea hawa wanashambulia kibofu na
baadaye huendelea mpaka kwenye figo. Hii ndiyo hatua kubwa ya ugonjwa ambayo
inaweza kusababisha kifo au tatizo la kudumu.
Hawa ni vimelea wa jamii ya bakteria
walio wanajulikana kwa jina la escherichia
coli(E.coli).
Bakteria hawa
wanapatikana katika utumbo mpana lakini husafiri kupitia njia ya haja kubwa
kwenda katika njia ya mkojo na kusababisha maambukizi katika kibofu na figo.
UTI inavyoenea
Dk Veronika
Kaniki kutoka hospitali ya Sekou Toure, anabainisha tabia na mazingira
yanayoweza kusababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuwa ni kushiriki ngono
mara kwa mara na watu tofauti bila kutumia kinga.
Anasema hii
inamfanya mtu kuchukua bakteria wa UTI kutoka kwa mwenzi wake ambaye tayari ana
maambukizi hayo.
Dk Kaniki
anaongeza kuwa kujitawaza kutoka nyuma kuja mbele baada ya haja kubwa
kunapelekea maambukizi hasa kwa wanawake.
Hii ni kwa
sababu vimelea hao hupatikana kwa wingi katika utumbo mpana.
Hivyo, kitendo
cha kujisafisha kwa njia hiyo, anasema huwasafirisha bakteria hao kutoka sehemu
ya haja kubwa kuja katika njia ya haja ndogo.
Anasema
mazingira haya husababisha UTI kwa wanawake kwa sababu njia ya haja kubwa na
ndogo zipo karibu sana.
“Mama wajawazito
pia wako hatarini zaidi kwa sababu mimba kukandamiza kibofu na
kusababisha kukosekana kwa uwazi katika njia ya mkojo ambayo kitaalamu
inajulikana kama incomplete emptying,” anafafanua Dk Kaniki.
Mtaalamu wa
magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Fransis Fredrick
anasema takwimu zinaonyesha kuwa kwa kila wanawake watano, mmoja amewahi kupata
ugonjwa huo.
Hali hiyo
anaielezea kuwa huweza kuwa ni ya kujirudia mara kwa mara kwa baadhi ya
wanawake, hasa kinamama wajawazito na watu wenye umri mkubwa.
Mbali na
wanawake kupata maambukizi zaidi, Dk Fredrick anaeleza kuwa watoto wa jinsi
zote pia wako hatarini.
Anasema ni vema
mazingira ya chooni na bafuni yawe safi ili kuwalinda watoto dhidi ya
maambukizi haya.
Dk Fredrick
anabainisha kuwa maambukizi katika njia ya mkojo yanaweza kusababishwa na
bacteria, fangasi au virusi. Anasema matibabu yake hutolewa kulingana na
aina ya vimelea waliosababisha maambukizi hayo.
Kisukari huathiri zaidi
Maambukizi haya
yanaweza pia kuwaathiri watu wenye kisukari kirahisi zaidi kwa sababu ya sukari
nyingi iliyopo katika mkojo.
Sukari hiyo
huchochea kuzaliana kwa bacteria wanaosababisha maambukizi.
Kwa mujibu wa
ripoti iliyofanywa na Chama cha Kisukari cha Marekani (ADA), asilimia 9.4 ya
watu wanaokutwa na kisukari wanaugua pia UTI wakati asilimia 5.7 ni wenye
maambukizi lakini hawana kisukari.
Wenye kisukari
wanaathirika zaidi kwa sababu pia bakteria kuzaliana kwa wingi na baadhi
ya mishipa inaharibika na kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Hata hivyo,
ripoti hiyo imebainisha kuwa sukari nyingi iliyopo kwenye damu ya mgonjwa wa
kisukari inaua seli nyeupe za damu, hivyo mwili unakosa kinga ya kupambana na
bakteria hatarishi walioingia mwilini.
Athari, dalili, tiba
Dk Kaniki
anafafanua kuwa endapo mtu hatatibiwa mapema au kumaliza dozi, ugonjwa huu
unaweza kuwa sugu na kusababisha kuharibika kwa figo na kibofu.
Anasema
maambukizi yanayotokea chini ya kibofu huathiri kibofu na mirija inayotoa mkojo
nje.
Maambukizi
yanayotokea katika figo ni hatua ya juu na athari zake ni kubwa zaidi kuliko
athari zitokeazo katika mirija na kibofu.
Alibainisha
athari nyingine kuwa mwanamke mjamzito anaweza kuzaa mtoto kabla ya wakati au
mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu.
Anasema wagonjwa
wanashauriwa kupata tiba mapema na kumaliza dozi na kwamba watoto wadogo na
wazee pia wanaweza kupata maambukizi hayo kirahisi.
Ripoti ya ADA
inabainisha dalili za awali kwa mtu mwenye maambukizi katika njia ya mkojo ni
maumivu wakati wa kukojoa, kuhisi kukojoa laini ukienda chooni mkojo unatoka
kidogo sana, kukojoa mkojo wenye damu na maumivu ya tumbo na mgongo.
Dalili kwa
maambukizi yaliyokomaa, zinaelezwa kuwa ni homa kali, kutetemeka, kutapika,
kuharisha na maumivu ya mgongo.
Hata hivyo,
kinga ya ugonjwa huu inaelezwa kuwa ni kuzingatia kanuni za usafi hasa baada ya
haja kubwa na kujisafisha kuanzia sehemu ya mbele kwenda nyuma ili kutoruhusu
vimelea kuingia katika njia ya mkojo kwa urahisi.
Inashauriwa
kumwona daktari baada ya kuona dalili hizi na kutumia kikamilifu dawa
itakayopendekezwa na daktari.
Ni muhimu kwa
mgonjwa kumaliza dawa ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa huo mara kwa mara na
kusababisha madhara au usugu.
0 comments :
Post a Comment