TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

  
Wakati Serikali ikijivunia mafanikio ya ujenzi wa shule za kata ambazo zimeongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari, kwa watu wengi shule hizo hazijazaa matunda stahiki.
Changamoto kubwa inayozikabili shule hizo ni kutoa wahitimu wengi wanaofeli mtihani wa kidato cha nne. Kwa mfano, matokeo ya mwaka 2012 yaliweka historia ya aina yake nchini, kwani wahitimu asilimia 60 walifeli kwa kupata daraja sifuri. Aghalabu, idadi kubwa ya watahiniwa hawa wanatoka shule za kata.
Bila shaka hii ni idadi kubwa ya vijana wa Kitanzania, ni jeshi la vijana wanaioishia mitaani na kukosa matarajio ya kimaisha. Kwa nini wanafeli na nini kifanyike kuwanusuru? Gazeti hili limewahoji wananchi wa kada mbalimbali wanaozungumzia hali hiyo.
Onike Kanyawana (Mkufunzi msaidizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
Kuna makosa yanafanywa na Serikali katika mfumo wa elimu, hasa kwa kuondoa mitihani muhimu ya kumpima mwanafunzi kutoka hatua moja kwenda nyingine.
Kwa wahitimu wa darasa la saba kinachofanyika ni sawa na kuhamishwa kutoka msingi kwenda sekondari badala ya kuchujwa kama ilivyokuwa zamani. Kama wasiostahili hawaenguliwi ili kuwapata wanaofaa kujiunga na sekondari, hakuna maana na watafanana tu na wale wa darasa la saba. Watakuwa wameongezewa muda wa kuwa shule, lakini matokeo yanabaki yale yale.
Hata mtihani wa kidato cha pili nao ni muhimu katika maendeleo ya wanafunzi hao. Kwa mwanafunzi mwenye uwezo wa chini, hawezi kufanya maajabu katika mtihani wa mwisho ikiwa alipitishwa pasipo vizingiti vyovyote. Laiti mtihani wa kidato cha pili ungekuwepo, hawa wanaofeli leo kidato cha nne wasingefika hapo, wangeishia kidato cha pili.
Jackline Champanda (mkazi wa Dar es Salaam)
Shule zihakikishe zinawabana wanafunzi kwa kuwapa mitihani ya kutosha, itakayowafanya wazingatie masomo katika muda mwingi na kujipanga vyema kabla ya mtihani wa mwisho.
Kuna wazazi wanaotingwa na kazi pamoja na majukumu mengine kiasi kwamba wanakosa muda wa kufuatilia mienendo ya watoto wao shuleni. Wengine hawakagui kabisa ripoti za maendeleo. Hii inatoa mwanya kwa watoto hao kujisahau, wanaacha kusoma na kujikita kwenye michezo na anasa nyinginezo zinazoendana na rika lao.
Rose Malinga (Katibu mwenezi wa CCM) Kata ya Kivule Dar es Salaam)
Kijana aliyefika kidato cha nne hata kama amefeli, anaweza kufanya mambo mengi ya kujikwamua kiuchumi na kuleta manufaa kwa jamii inayomzunguka. Hii ni kwa sababu uelewa wake uko juu, tofauti na yule ambaye hajaipata kabisa. Vijana hawa wana nafasi katika vyama vya siasa kwa kushiriki katika mambo mbalimbali.

0 comments :

 
Top