Wahudumu wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa wamebeba masanduku ya kura za wajumbe waliopiga kura za siri kwa Sura ya 11 hadi 19 ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma/Dar. Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliopiga kura za hapana wamelazimika kuondoka Dodoma na kurudi Zanzibar kwa madai ya vitisho walivyopata kutoka kwa wenzao.
Mmoja wa wajumbe hao, Salma Said alisema jana jioni kuwa yeye na wajumbe wenzake wamekataa kuitikia wito wa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kwenye Kamati ya Mashauriano ili kuhojiwa kuhusu kura hiyo na kutokana na vitisho wanavyopata kutoka kwa wajumbe wenzao wameamua kuondoka Dodoma.
Vitisho hivyo vimeripotiwa muda mfupi baada ya Sitta kuunda Kamati ya Mashauriano ya watu tisa inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan kushughulikia kura hizo zilizopigwa na wajumbe saba zinazoweka njiapanda uwezekano wa kupatikana akidi ya kupitisha Katiba inayopendekezwa.
Wajumbe waliopiga kura za wazi za hapana kwa ibara zote ni Adil Mohamed Adil, Dk Alley Soud Nassor, Fatma Mohamed Hassan, Jamila Ameir Saleh, Salma Hamoud Said, Mwanaidi Othman Twahir na Ali Omary Juma.
Kwa upande wa Tanzania Bara aliyepiga kura ya hapana kwa rasimu nzima ni Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi na wajumbe 30 kutoka Zanzibar wakipiga kura ya siri.
“Baada ya kupiga kura za hapana leo (jana), walijitokeza wajumbe akiwamo (jina tunalihifadhi kwa sasa) wakaanza kutuzongazonga,” alisema Salma.
“Walituambia kuwa tumebaki hadi dakika ya mwisho halafu tunasema hapana kwa rasimu nzima ili kula fedha za bure, wanasema bora tungeondoka na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Hata hivyo, alipopigiwa simu yake ya mkononi mmoja wa watuhimiwa, alipokea na baada ya mwandishi kujitambulisha alikata simu na alipopigiwa mara ya pili alijibu alisema; “Mimi ni mheshimiwa mwana na niko Sudan.”
Salma alisema miongoni mwa wajumbe hao wakiwamo baadhi ya mawaziri waliwafuata hadi nje ya ukumbi wakiwatishia kuwa watawafanyia hujuma kwa kukataa kuunga mkono rasimu hiyo.
“Sisi tumeamua kuondoka kurudi kwetu, hatutaingia tena bungeni maana hivi vitisho vimezidi sasa,” alisema Salma.
Juhudi za kuwapata wajumbe wenzake kuzungumzia vitisho hivyo hazikuzaa matunda, lakini Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba amelichukulia kama suala la kisiasa.
Alisema wajumbe hao hawajasema wametishiwa kufanyiwa kitu gani, bali walimweleza kuwa wameambiwa kuwa wamekaa pale (bungeni) kwa ajili ya kupata pesa.
Kuhusu kukataa kwao kuhudhuria katika Kamati ya Mashauriano, Hamad alisema hawezi kulitolea jibu kwa kuwa litafanya maridhiano yasifanyike.
Kamati ya Maridhiano
Akitangaza kuunda kamati hiyo, Sitta alisema ana suala mbele yake ambalo linahitaji mashauriano chini ya Kanuni ya 54(4) kutokana na baadhi ya wajumbe kupiga kura ya hapana kwa ibara zote.
Kanuni hiyo inasema: “Mwenyekiti baada ya kushauriana na kamati ya uongozi anaweza kuunda kamati ya mashauriano pale linapojitokeza suala linalohitaji mashauriano.
“Baadhi ya wajumbe jana (juzi), walipiga kura za hapana kwa ibara zote, jambo ambalo haliwezekani kuwa hivyo. Kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti, nimeunda kamati hii ambayo naomba ikafanye kazi leo,” alisema.
Alisema kamati hiyo yenye wajumbe tisa itakayoongozwa na Samia na baada ya kikao chake cha jana itatoa matokeo bungeni. Wajumbe wengine ni Rashid Mtuta, Shamsi Vuai Nahodha, Omary Yusuf Mzee, Mohamed Aboud, Andrew Chenge, Dk Asha-Rose Migiro, Dk Francis Michael na Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi.
“Hawa watakaa na wale wawili walioniomba kwamba wanataka kusikilizwa kwa nini wamesema hapana kwa kitendo ambacho inaonekana kama wamepoteza muda kukaa bungeni ili kukataa Katiba yote,” alisema.
Alitoa nafasi kwa wajumbe wengine ambao walipiga kura za hapana watakaopenda kwenda katika kamati hiyo kueleza ni kwa nini waliikataa rasimu hiyo.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa upigaji kura jana, Sitta alisema kuwa hali inakwenda vizuri... “Inshallah hali inakwenda vizuri na dua la kuku halimpati mwewe.”
0 comments :
Post a Comment