TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749



Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Profesa Ibraahim Haruna Lipumba, amesema Tanzania ipo katika hatari kubwa ya kupoteza vivutio vyake vya utalii wakiwemo tembo, kwani serikali imeshindwa kupambana na tatizo la ujangili ambalo linaonekana kushamiri siku hadi siku.
Lipumba ameyasema hayo wakati alipokuwa akifanya mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Redio Tehran ikiwa ni siku chache tu tokea taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya EIA kutoka nchini Marekani kuripoti kwamba ujumbe wa raisi wa China Xi Jinping uliotembelea Tanzania miezi 18 iliyopita, ulijihusisha na ununuzi wa meno ya tembo.
Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Lipumba amesema hana ushahidi kwamba ndege ya raisi wa China wakati wa ziara yake nchini ilihusika na ubebaji wa meno ya tembo.
Akijibu suali la muandishi wa habari linalohoji kwamba ni vipi kiasi kikubwa cha meno ya tembo kisafirishwe nje ya nchi na serikali isihusike kwa namna yoyote, Lipumba alisema
“Mtandao wa majangili ni mpana sana, na unahusisha vyombo vya dola wakiwemo askari wa wanyamapori, polisi, maafisa wa bandari, na usalama”
Aidha ameitolea mfano operesheni tokomeza ujangili kuwa nao walihusika katika kuruhusu ujangili huo kufanyika ambapo ilishuhudiwa kiasi kikubwa cha tembo kuuwawa, na meno yake kusafirishwa nchi za nje.
Tanzania ni miongoni mwa nchi inayokabiliwa na tatizo kubwa la ujangili ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010, jumla ya tembo 10,000 waliuwawa ikiwa ni sawa na wastani wa tembo 27 kwa siku.
Mwaka wa 2012, tembo takribani 23,000 wameuwawa ambao ni sawa na tembo 63 kwa siku, hii ni sawa na ongezeko la asilimia 57% kwa kipindi cha miaka miwili. Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na tembo kati ya 150,000 na 170,000.

0 comments :

 
Top