WAKATI Benki ya NBC ikiuzwa kwa wawekezaji wa Afrika Kusini mwaka 2000, kwa thamani ya shilingi bilioni 16, yenyewe ilikuwa na kiasi cha shilingi bilioni 151 taslimu katika akaunti zake mbalimbali duniani, Raia Mwema limebaini.
Kiasi hicho cha fedha ni mbali na thamani ya majengo na mali nyingine za NBC ilizokuwa ikimiliki wakati huo, na kwa maana hiyo, serikali iliuza benki hiyo kwa kiasi cha asilimia kumi ya kiasi ilichokuwa nacho kama akiba.
Mmoja wa wapinzani wakuu wa ubinafsishaji wa benki hiyo alikuwa ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye gazeti hili liliwahi kuripoti kwamba alilia machozi wakati alipopewa taarifa za kutaka kuuzwa kwa benki hiyo.
Sasa, Raia Mwema limefanikiwa kupata ripoti ya mwisho ya hali ya kifedha ya benki hiyo wakati ikiuzwa, inayoonyesha kiasi cha fedha ilizokuwa nazo katika mabenki mbalimbali duniani.
Chini ya taratibu za kibenki, NBC ilikuwa na fedha zake katika akaunti za mabenki mengine ya nchi za nje; maarufu kwa jina la Nostro Accounts, kama ambavyo mabenki ya kigeni yalivyokuwa pia yana akaunti zake NBC.
Gazeti hili limefanikiwa kuona ripoti, ambayo pamoja na mambo mengine, inaonyesha kwamba NBC ilikuwa na fedha katika nchi za Australia, Austria, Uingereza, Marekani, Canada, Ujerumani, Ufaransa, Uswisi, Uholanzi, Ubelgiji, Japan, Sweden na Norway.
Nchi nyingine ambazo NBC ilikuwa na fedha ni Denmark, India, Italia, Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Pakistani, Zambia na Zimbabwe.
Benki hiyo ilibadilishwa jina kutoka kuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kuwa NBC (1997) baada ya ubinafsishaji wake mwaka 1997, kabla ya kuitwa NBC Ltd baada ya kuuzwa mwaka 2000.
Baadhi ya mabenki ambayo NBC ilikuwa na akaunti ni Commonwealth Bank ya Australia, Barclays, Lloyds, ANZ Bank, Midland Bank, Deutsche Bank, National Westminster Bank, Citibank, HSBC, Canadian Imperial, Den Norske, Banque National du Paris, Banca Commerciale Italiano na nyinginezo.
Ubinafsishwaji na hatimaye uuzwaji wa benki hiyo ni miongoni mwa masuala tata yaliyogubika utawala wa serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa.
Serikali ilibinafsisha NBC kwa maelezo kwamba haikuwa na fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya kibenki, madai ambayo waliokuwa wakiongoza benki hiyo walisema hayakuwa ya kweli tupu.
Gazeti hili limefanikiwa kuzungumza na baadhi ya wakuu wa NBC, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Hazina waliokuwa kazini wakati huo na wengi wao walithibitisha kuwapo kwa kiwango hicho cha fedha na kwamba serikali haikutakiwa kabisa kuiuza benki hiyo.
“Ni kweli kwamba NBC haikuwa na fedha za kutosha kwenye akaunti zake za hapa nchini. Lakini jiulize kwanini ilifikia hapo? Ilifika hapo kwa sababu serikali ilikuwa imekopa kiasi kikubwa cha fedha pasipo kulipa.
“Hivyo serikali ndiyo iliyosababisha hali hiyo kwa kukopa bila kulipa. NBC ndiyo ilikuwa kimbilio la serikali kila ilipokuwa na tatizo la kifedha. Lakini dawa haikuwa kuiuza ile NBC. Serikali ingeuza tu majengo manne ya benki kwa mabenki haya ya kigeni yaliyokuwa yakitaka kuja nchini.
“Nakumbuka tulisema hivi, tuuze lile jengo la Bank House ambalo sasa ndilo linatumiwa na NMB jijini Dar es Salaam. Tungeweza kuuza na moja kubwa katika mikoa ile mikubwa ambayo mabenki haya mapya yalikuwa yanataka kuwa na majengo.
“Siku hizi mabenki yamekosa majengo mijini hadi yanakwenda kutafuta maeneo vichochoroni na wanapata shida na majambazi. Tulitaka tuuze maeneo ya mijini kwao. Kwa kuuza majengo manne tu, NBC ingeweza kuwa katika hali nzuri na ikajiendesha. Cha ajabu wakubwa wakaamua kuiuza,” alisema mmoja wa watu walioshiriki kwa karibu katika mchakato mzima wa uuzwaji wa benki hiyo.
Raia Mwema limeambiwa kwamba ili kuhalalisha ubinafsishaji na uuzaji huo wa NBC, serikali kwanza iliomba ushauri wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu ambayo ilisema benki hiyo inaweza kujiendesha pasipo kuuzwa lakini baadaye ikaenda kuomba ushauri kwa mojawapo ya kampuni za kigeni, PriceWaterHouseCoopers ambayo ilipendekeza kuuzwa kwa NBC kwa maelezo kwamba haina fedha.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa NBC wakati wa mchakato wa kutaka kuiuza, Donald Kamori, anadaiwa kupingana na mpango wa kutaka kuiuza na inaelezwa ndiyo chanzo cha kung’olewa katika wadhifa wake huo.
Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, aliyepata kuwa Katibu Myeka wa Mwalimu Nyerere, Samwel Kassori, alipata kusimulia namna Kamori alivyoeleza umuhimu wa kutouza NBC, mawazo ambayo Mwalimu alikubaliana nayo.
Gazeti hili limeelezwa kwamba vigogo waliotaka NBC iuzwe kwa gharama yoyote walimwona Kamori kama mtu aliyewachongea kwa Mwalimu na ndiyo maana aliondolewa NBC haraka.
Gazeti hili lilimtafuta Kamori ili aeleze kuhusu uhusika wake katika ubinafsishaji na uuzaji wa NBC lakini alikataa kuzungumza chochote kwa maelezo kwamba hapendi kuzungumzia mambo hayo.
“Naomba utafute watu wengine wakwambie. Mimi sina cha kusema. Wapo watu waliokuja kuchukua nafasi yangu watafute na uwaulize. Naheshimu sana gazeti lenu lakini naomba nisiongee,” alisema Kamori.
Hata alipoelezwa kwamba mtu aliyechukua nafasi yake, Dk. Francis Mlozi, aliyetokea BoT, amefariki dunia na hakuna njia ambayo Raia Mwema linaweza kumpata, Kamori alisisitiza kwamba lazima wapo wanasheria au wahasibu waliokuwapo wakati huo ambao wangeweza kusaidia lakini si yeye.
Juhudi za gazeti hili kutafuta taarifa zaidi zililifikisha kwa aliyekuwa Mwanasheria wa NBC, Mathew Kakamba, ambaye naye hakutaka kuzungumza chochote kuhusu benki hiyo.
“Ndugu yangu mimi nimeondoka NBC zamani kidogo. Hapa katikati kuna mambo mengi yamepita na mengine nimesahau. Naomba utafute watu ambao wanaweza kuwa wanakumbuka vizuri,” alisema Kakamba.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, ambayo pia inasimamia shirika hilo, alisema wamezungumza na ofisi za Gavana wa BoT na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili suala la ubinafsishwaji na hatimaye uuzwaji wa NBC litazamwe upya.
“Sijajua hizo taarifa zako za Nostro Accounts kama ni za kweli au la lakini ninachojua ni kwamba zoezi zima la ubinafsishwaji na uuzwaji wa benki hiyo lina kiwingu kizito na ukweli ni lazima ujulikane. Gavana na CAG tayari wanaliangalia suala hilo,” alisema Zitto.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya NBC Ltd, kufikia mwezi Desemba mwaka 2010, benki hiyo ilikuwa na mali zenye thamani ya shilingi trilioni 1.4 na amana zenye thamani ya shilingi bilioni 153.
Benki hiyo iligawanywa mwaka 1997 ambapo taasisi tatu zilizaliwa. Taasisi hizo ni benki za NBC na NMB iliyopachikwa jina la Benki ya Makabwela na Shirika Hodhi la NBC ambalo kazi yake kubwa ilikuwa ni kusimamia zilizokuwa mali za benki hiyo kabla ya kugawanywa.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/nbc-ilikuwa-na-bilioni-150-ikauzwa-kwa-bilioni-16#sthash.N0LeQv1K.dpuf
0 comments :
Post a Comment