TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

Dar es Salaam. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikisisitiza kuwa ratiba ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura itakuwa kama ilivyopangwa, Chadema imesema itachukua uamuzi mgumu endapo shughuli hiyo itachelewa na kuharibu mchakato wa Kura ya Maoni.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba alisema jana kuwa uboreshaji huo utaanza Februari 16 na utamalizika kwa wakati ili kupisha ratiba ya Kura ya Maoni.
“Ratiba inazingatiwa, vifaa vitafika kwa wakati na kuanza kazi,” alisema Malaba.
Hata hivyo, Chadema imeeleza kwamba Kamati Kuu yake itakayokaa leo itajadili hatima ya mchakato huo kabla ya kupiga Kura ya Maoni Aprili 30.
Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene alisema watachukua hatua zaidi iwapo mashine za Biometric Voters Registration (BVR) zitabainika kuwa na kasoro katika uboreshaji huo.
Uandikishaji wa Watanzania milioni 26 wenye sifa ya kupiga kura ulitakiwa kuanza mwezi huu lakini NEC ilibadilisha ikisema inasubiri mashine 7,750 kwa ajili ya kazi hiyo.
Makene alisema muda uliobaki kwa ajili ya kazi hiyo hautoshi ndiyo maana wameamua kuitisha kikao cha dharura ili wafanye uamuzi.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema hana uhakika iwapo NEC itamaliza kazi hiyo kwa wakati na elimu ya Kura ya Maoni kutolewa kabla ya upigaji kura.
Sheria Namba Tatu ya mwaka 2014 kuhusu Kura ya Maoni inaweka utaratibu wa kutoa miezi miwili ya elimu na mmoja wa kampeni kabla ya kupiga kura ya maoni itakayofanyika nchini kote Aprili 30 mwaka huu.

0 comments :

 
Top