TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

UONGOZI wa Gereza la Keko Jijini Dar es Salaam, umebuni mradi wenye harufu ya kuwaibia wananchi wanaotembelea gereza hilo kila siku kwa ajili ya kukutana na kuwafariji ndugu na jamaa zao wanaotumikia adhabu ya kifugo pamoja na watuhumiwa walioko mahabusu.
Mradi huo wa wizi, unamtaka kila mwananchi anayetembelea Gereza la Keko kulipia Sh 300 kwa kila simu aliyonayo, kwa kuwa kisheria mtu haruhusiwi kungia ndani ya eneo la gereza akiwa na simu ya mkononi. Katika mradi huo, mwananchi anapofika katika lango la gereza hilo na kueleza shinda yake, kabla ya kuruhusiwa kuingia, huelekezwa eneo la kuacha simu zake za mkononi na vitu vingine vyote visivyoruhusiwa kuingia navyo ndani ya gereza.
Kwa hiyo, kama mwananchi huyo mmoja anamiliki simu moja, atalipia Sh 300, kama anamiliki simu mbili, atalipia Sh 600 na kama anamiliki simu tatu, basi atalazimika kuacha hapo Sh 900 kama gharama ya kulinda simu zake.
Kwa wastani, gereza hilo hupokea wageni zaidi ya 100 kila siku. Kwa hiyo, mradi huo unauhakikishia uongozi wa gereza hilo wastani wa mapato ya kiasi cha Sh 40,000 kwa siku, sawa na wastani wa Sh 280,000 kwa wiki, sawa pia na Sh 1,200,000 kwa mwezi.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu kwa wiki kadhaa sasa, umebaini kwamba idadi ya watu wanaotembelea gereza hilo kwa siku za wikiendi, kwa maana ya Jumamosi na Jumapili, ni kati ya 150 na 200 kwa kila siku, wakati katika siku za kawaida, kwa maana ya Jumatatu hadi Ijumaa, idadi ya watu wanaotembelea gereza hilo kuwaona ndugu na jamaa zao ni kati ya 60 na 100 kila siku.
Muonekano wa geti la kuingilia kwenye gereza la Keko lililopo jijini Dar es Salaam
Muonekano wa geti la kuingilia kwenye Gereza la Keko lililopo jijini Dar es Salaam 
Kwa mujibu wa takwimu hizo za idadi ya watu wanaotembelea gereza hilo kwa siku za wikiendi na siku za kawaida, ni wazi kwamba mradi huo wa wizi kwa wananchi hao wanaotembelea gereza hilo kwa lengo la kuona ndugu na jamaa zao, unatengeneza fedha nyingi zaidi kila ifikapo Jumamosi na Jumapili.
FikraPevu  imeshindwa kujiridhisha kama kweli mradi huo wa wizi umebuniwa, kuratibiwa na kusimamiwa na uongozi wa gereza hilo au umebuniwa na baadhi ya askari wake wanaokuwa zamu mlangoni, waliokaukiwa na maadili kwa sababu ya tamaa zao za fedha, lakini Mkuu wa Gereza hilo, Mbwana Senshida, ametolea kauli kuhusu suala zima hilo, akisema:
“Kwanza, hilo duka ambalo simu zinatakiwa ziwekwe ni la mtu binafsi, halihusiani kabisa na Idara ya Magereza nchini wala Gereza la Keko. Mgeni yeyote haruhusiwi kuingia na simu ndani ya gereza, kwa hiyo, askari wetu wanachokifanya ni kuwaelekeza wenye simu na vyombo vingine vya kielektroniki mahali salama pa kuhifadhi vitu vyao, sasa kama wanalipishwa fedha, hayo yatakuwa ni makubaliano ya raia mwenyewe na mwenye duka, lakini siyo magereza.
“Labda sasa kwa kuwa ninyi watu wa FikraPevu mmeniambia kuna tatizo la usalama na kutokuwa na dhamana yoyote pindi simu au mali yoyote inapopotea, tufanye kwamba nimeyapokea malalamiko hayo, nitayafanyia kazi ili kuhakikisha wananchi hawakutani na tatizo la kupotelewa na mali zao.
“Bado naamini kwamba askari wetu wanapotoa maelekezo ya wapi wakahifadhi simu zao, anafanya hivyo kwa nia njema tu kwa kuwa wageni wanaokuja gerezani ni wateja wetu, na sisi tunapenda wananchi waje gerezani kuangalia ndugu zao kwa sababu wanapokuja wanawapa faraja…hatuwezi kuwaambia kwa kuwa wana simu, basi hawaruhusiwi kuwaona ndugu zao, warudi makwao.
“Zamani wageni wetu walikuwa wanaingia na simu zao zikiwa zimezimwa.

Kulikuwa na matangazo kila mahali kwamba ukionekana unaongea na simu ukiwa ndani ya eneo la gereza utachukuliwa hatua za kisheria. Lakini siku hizo kuna hali tete ya usalama inayotokana na wimbi la mashambulizi ya kigaidi. Mtu haruhusiwi kabisa kuingia ndani ya eneo la gereza akiwa na simu ya aina yoyote kutokana na habari za kiitelejensia kwamba simu zinaweza kutumika kama njia ya kulipulia mabomu.”
Mbinu zinazotumika na mahali pa kuweka simu hizo kwa malipo ya Sh 300
Kila mwananchi anayeingia lango kuu kutaka kuonana na ndugu au jamaa yake, huelekezwa na askari mmojawapo wa zamu sehemu ya kuweka simu zake kama anayo simu moja au zaidi ya moja. Sehemu hizo ziko mbili.
Sehemu moja mwananchi huyo anapoelekezwa ni kwenye maduka ya watu binafsi yaliyoko mbele ya geti la kuingilia gerezani hapo. Baadhi ya maduka hayo yanaelezwa na baadhi ya wenyeji wanaozunguka gereza hilo kwamba yanamilikiwa na baadhi ya askari magereza wanaofanya kazi ndani ya gereza hilo la Keko. Hapa wanaopokea simu na kutoza fedha kiasi hicho cha Sh 300 ni raia wa kawaida.
Sehemu ya pili ni ndani ya gereza. Hapa baada ya mwananchi au raia kukaguliwa, humwambia azime simu yake na kuikabidhi kwa askari magereza ambaye huibandika lebo yenye jina la mmiliki wa simu na kisha raia hiyo kutakiwa kuacha fedha kwa askari huyo kulingana na idadi za simu alizonazo.
Wananchi kulazimishwa kununua vitu katika maduka mbele ya gereza la Keko
Kwa kawaida ndugu na jamaa za wafungwa na au mahabusu wanayo haki ya kupeleka chakula na baadhi vifaa kama vile nyembe, dawa ya meno, miswaki, sabuni na kadhalika. Hata hivyo, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na uongozi wa gereza hilo, vitu hivyo havipaswi kununuliwe njea ya maduka yaliyoko mbele ya lango kuu la gereza hilo.
Kila mwananchi anayenunua vitu hivyo nje ya maduka hayo, haruhusiwi kuingia navyo ndani ya eneo la gereza kwa ajili ya kumkabidhi ndugu au jamaa yake anayetumikia kifungo au aliyeko mahabusu. Atarudi navyo nyumbani kwake.
 
Kinachoumiza na kinacholalamikiwa na wananchi si marufuku hiyo ya mtu kuja na vitu alivyonunu nje ya maduka hayo yaliyoko katika lango la gereza la Keko, bali bei kubwa ya kulangua ambayo wananchi wanalazimishwa kununua vifaa hivyo. Kwa mfano, inaeleweka kwamba mche wa sabuni kwenye maduka ya rejareja katika maduka ya kawaida huuzwa kati ya Sh 1,700 hadi 2,000 kulingana na aina ya sabuni, lakini katika maduka hayo mche wa sabuni huuzwa Sh 2,500 bila kujali aina ya sabuni.

Kauli za wananchi kuhusu kero hiyo ya gereza la Keko
FikraPevu imefahamishwa na baadhi ya wananchi wa maeneo mbalimbali nchini kwamba karibu magereza zote nchini zinaendesha miradi mbalimbali ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi, lakini mamlaka za juu za magereza zinapoulizwa juu ya malalamiko hayo ya wananchi hukanusha vikali kuhusu kuwepo miradi hiyo inayosababisha kero na usumbufu kwa wananchi.
Mama Husna mwenye umri wa miaka 57, aliyejitambulisha kwamba ni mkazi wa maeneo ya Mbweni, katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, ni miongoni mwa wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo ya kulazimishwa alipie Sh 300 kwa kila simu anayoimiliki, siku alipotembelea gereza la Keko kwa lengo la kumjulia hali ndugu yake.
“Mwanzoni tulikuwa tunaambiwa tuzime tu simu halafu tunaingia nazo ndani, lakini siku hizi uongozi umebadilisha utaratibu hali inayowakwamisha watu wengine kushindwa kuwaona ndugu zao kwa maana hata kama una simu tatu unaambiwa kila moja uilipie Sh 300, wakati mtu unakuwa hujajiandaa kwa kuipangia bajeti,” anasema Mama Husna katika hali ya malalamiko na kuongeza:
“Nadhani mambo kama haya ni sababu mojawapo inayofanya Jeshi la Magereza nchini lipoteze hadhi yake. Baadhi ya watendaji na wasimamizi wake hujihusisha na vitendo vya rushwa.
Wananchi wengine ni Karisa Birago na Edward Godfrey wakazi wa jiji la Dar es Salaam, ambao kwa nyakati tofauti baada ya kukumbwa na kadhia hiyo ya Keko, wanasema usalama wa mali za wananchi wanaokwenda kuwaona ndugu na jamaa zao katika gereza hilo, zinazowekwa kwenye moja ya maduka yanayotumika kuendesha mradi huo, ni mdogo.
“Kuna watu wanakwenda kuwaona jamaa zao pale gereza la Keko wakiwa na vitu vyao vya thamani katika mabegi yao kama vile laptop na simu za bei mbaya…hivi vitu hivi ukiviacha dukani pale halafu jamaa wakakuruka kwamba hujaacha kitu pale, utakwenda kushitaki wapi wakati huna ushahidi wala kielelezo chochote kwamba umeacha vitu vya thamani dukani mle?” analalamika Birago
FikraPevu inaendelea na juhudi za kumtafuta Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, CGP John Casmir Minja, ili pamoja na mambo mengine, aweze kutolea ufafanuzi juu ya mradi huu wa gereza la Keko na miradi mingine inayosababisha kero kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, baada ya juhudi za mwanzo kushindwa kumpata mkuu huyo.
Source FikraPevu

0 comments :

 
Top