TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


Vituo vya kulelea watoto (Daycare) vinavyoendeshwa bila kibali na visivyokuwa na sifa huenda vikafika mwisho baada ya Serikali kuanza kuvifunga.

Wakati Serikali ikitangaza kuchukua hatia hiyo, halmashauri ya wilaya ya Ubungo imetangaza kuanza kuvifunga vituo hivyo kuanzia Januari 21, 2021.

Maamuzi haya pia yanakuja ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu ukuta wa kituo cha kulelea watoto ‘Joy Unit Daycare’ kilichopo Bonyokwa jijini hapa kudondoka na kupoteza maisha ya watoto watatu na wengine sita kujeruhiwa.

Ukuta huo ulidondoka Novemba 18, 2020 wakati wanafunzi wakijiandaa kuanza masomo yao asubuhi, jambo ambalo pia liliifanya Serikali kuahidi kufanya msako wa vituo vya aina hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Dk Naftali Ng’ondi alisema kabla ya kufikia uamuzi wa kuvifunga, wamiliki wa vituo hivyo waliagizwa kufanyia kazi mapungufu katika maeneo yao.

Alisema pia kwa sababu kamishna anapewa mamlaka ya kusajili na kukagua vituo hivyo, pia husaidia namna ya kufanya maboresho kwa vituo vilivyo na uelekeo.

“Kabla ya kuanza utekelezaji wa kuvifunga wamiliki tuliwapa muda kuanzia Desemba 11 hadi 25, 2020 na sasa unaofanyika ni utekelezaji wa maamuzi.

“Hiyo ni kwa sababu vituo hivi vinalea watoto ambao wanahitaji uangalizi wa hali ya juu,” alisema Dk Ng’ondi.

Utekelezaji wa agizo hili pia unakuja kipindi ambacho kumekuwa na uanzishwaji wa vituo vingi vya kulelea watoto katika mitaa mbalimbali, hasa katika jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Zainabu Masilamba kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, vituo hivyo vitafungwa kutokana na kuendeshwa kinyume na Sheria ya mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na manispaa hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mmiliki atakayekaidi agizo hilo.

“Hatua za kisheria zitakazochukuliwa ni pamoja na kulipa faini kati ya Sh2 milioni hadi Sh5 milioni.”

Pia wazazi walikumbushwa kupeleka watoto wao katika vilivyosajiliwa kisheria ili watoto wapate malezi bora.

Novemba 19, 2020 alipozungumza na Mwananchi, Dk Ng’ondi alisema zaidi vituo 1,500 vya kulelea watoto vina usajili wa kudumu nchi nzima huku akitaja baadhi ya vigezo vya kufungua vituo hivyo kuwa ni uwepo wa jengo na hatimiliki ya eneo au mkataba wa kukodishiwa eneo husika.

Taarifa ya polisi inahitajika ili kuhakikisha kuwa mhusika si mtu aliye na rekodi ya uhalifu, awe wadhamini watatu, awe na kipato cha kuendesha kituo hicho, watumishi wenye uwezo kulingana na idadi ya watoto wanaojumuisha mhudumu wa ofisi, mpishi na msaidizi wa watoto.

Pia mtu huyu atahitaji barua ya mtendaji kuonyesha kuwa ana sifa na baada ya hapo ofisa ustawi atafanya ukaguzi kuonyesha kuwa ana kigezo, bwana afya atafanya ukaguzi wa mazingira kama ni safi na mazuri kwa watoto, eneo ni zuri lisiwe karibu na shughuli za watu kama soko au baa.

“Baada ya kuanzishwa pia huwa tunafanya ukaguzi wa kushtukiza katika vituo hivyo na kila baada ya robo ya mwaka hukaguliwa na maofisa ustawi wa jamii na vituo hivi huwa vinapaswa kututumia taarifa juu ya utendaji kazi wao,” alisema Dk Ng’ondi. BONYEZA HAPA KUSOMA MENGI ZAIDI

0 comments :

 
Top