TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Taifa linapita katika wakati mgumu kwani hata yeye hana furaha licha ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, Machi 19, 2021, wakati akilihutubia taifa mara baada ya kula kiapo cha kuwa Rais Tanzania Ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia kifo cha Rais Magufuli na kwamba ametangaza kuwa na maombolezo ya siku 21.

Rais Samia amesema kuwa "Kwa masikitiko makubwa nawajulisha tena kwamba tulimpoteza kiongozi wetu shupavu aliyekuwa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, ambaye amefariki kwa tatizo la moyo ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10" 

"Kwa mujibu wa sheria, mazishi ya viongozi wa kitaifa, nchi yetu itakuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 21 na bendera zitapepea nusu mlingoti"

“Nimekula kiapo nikiwa na majonzi tele na nchi ikiwa imetandwa na wingu jeusi la simanzi, nimekula kiapo katika siku ya maombolezo kwa ajili hiyo mtaniwia radhi, nitaongea kwa uchache tutatafuta wasaa mwingine hapo baadaye tuzungumze.

“Leo sio siku nzuri sana kwangu ya kuhutubia Taifa maana nina vidonda vikubwa moyoni, kiapo nilichokula leo ni tofauti na vyote nilivyowahi kula katika maisha yangu, nimekula kiapo cha juu kabisa Tanzania nikiwa na majonzi tele, mniwie radhi nitaongea kwa uchache"

“Kwa mara ya kwanza tumempoteza Rais akiwa madarakani, nichukue fursa hii kumpa pole Mama Janeth Magufuli pamoja na Mama Suzan Magufuli (Mama Mzazi wa Marehemu Dkt.John Pombe Magufuli), tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu na kuahidi kuendelea kuwashika mkono."
 
"Nikiri kuwa ni jambo ambalo hatujawahi hata kuwa na uzoefu nalo katika historia ya nchi yetu ni kwa mara ya kwanza tumempoteza Rais wa nchi akiwa madarakani na ni mara ya kwanza pia kwa aliyekuwa Makamu wa Rais kuwa Rais"

“Natoa salamu za rambirambi kwa Watanzania wote kwa pigo hili kubwa ni msiba mzito ambao hatukuutarajia sote tunafahamu namna Rais Magufuli alivyoipenda nchi hii na alivyojitoa kuwatumikia watu wake, ameibadili taswira ya nchi kwa vitendo huku muda wote akimtanguliza Mungu."

"Mimi nilipata bahati ya kuwa Makamu wake (Rais Magufuli) alikuwa ni kiongozi asiyechoka kufundisha kuelekeza kwa vitendo vipi anataka nchi hii iwe, amenifundisha mengi amenilea na kuniandaa vya kutosha, naweza kusema bila chembe ya shaka kuwa tumepoteza kiongozi shupavu na mwana mwema wa Bara la Afrika".

"Sote tunafahamu Rais Magufuli alivyoipenda nchi yetu, sote ni mashahidi kwa namna ambavyo ameweza kuibadili taswira yetu ya nchi kwa vitendo na kwa utendaji wake imara usiotikisika huku muda wote akimtanguliza Mungu mbele"

"Niwaombe Watanzania tuwe na moyo wa subira, tujenge umoja na mshikamano, niwahakikishie kuwa tuko imara kama Taifa na sisi viongozi wenu tumejipanga vizuri, tunayo katiba ambayo nimeapa kuilinda na kuisimamia, nchi yetu inayo hazina nzuri ya uongozi iliyojengwa na viongozi waliotutangulia, niwahakikishie kuwa hakuna jambo litakaloharibika,"

"Isitoshe, nchi yetu inayo hazina nzuri ya uongozi na misingi imara ya utaifa, udugu, umoja na ustahimilivu na nidhamu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama iliyojengwa na viongozi waliotutangulia kwa kuanzia na waasisi wetu."

"Niwahakikishie hakuna jambo litakaloharibika."

"Kipekee nikishukuru chama cha Mapinduzi kwa ukomavu wake na uongozi wake madhubuti ambao ndio msingi wa kuwezesha mabadiliko haya kwa amani na utulivu, nitumie fursa hii pia kuwashukuru ndugu zetu wa vyama vya upinzani kwa salamu zao za kunitia nguvu, faraja na mshikamano walizokuwa wakinifikishia mara tu baada ya kutangazwa taarifa za msiba huu mkubwa."

"Vilevile nivishukuru vyombo vyetu vyote vya habari ambao wamekuwa wakirusha matukio yote mubashara bila kuwasahau wasanii wetu ambao wametunga tungo na nyimbo mbalimbali za faraja na mwisho japo si kwa umuhimu, nishukuru familia yangu hasa mume wangu."

"Niwaase ndugu zangu watanzania kusimama pamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha maombolezo, huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, udugu wetu, kudumisha amani yetu."

"Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini, si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo, si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele."

0 comments :

 
Top