TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

              PAKUA APP YETU HAPA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu amewaapisha viongozi mbalimbali ambao aliwateuwa Aprili 4, 2021. Miongoni mwa viongozi hao ni makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa idara mbalimbali. Rais Samia awapongeza viongozi wote walioteuliwa na kuapishwa pamoja na kutoa hotuba fupi.

Akihutubia Rais Samia ameanza kwakusema kuwa “Nina salamu mpya nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnatakiwa kuitikia kazi iendelee”

Rais Samia aliendelea kwa kusema  “Watanzania tunakaribia Milioni 60 na zaidi ya Watanzania Elfu 5 walikuwa na sifa za kukaa mlipokaa leo lakini Mungu akaona nyinyi mpate nafasi, mlioapa leo nendeni mkafanye kazi”.

“TAMISEMI mbali na majukumu mengine mna jukumu la elimu na afya, Shule za Sekondari za Wanawake zina bajeti maalum naomba mkasimamie, tunatarajia kujenga Shule 26 mpaka 2025 naomba hili likatimie pamoja na kuendelea kujenga Hospitali za Wilaya”

"Naomba tuiangilie mitaala yetu, sote ni watanzania, tuangalie mitaala itakayotupeleka mbele. Nchini Afrika ya kusini, kiswahili ni moja ya somo katika mitaala yao, Tanzania pia, wenye lugha yetu na tunasema tunaipa kipaumbele lugha ya Kiswahili, bado pia Kiswahili ni somo hapa nchini, mkaliangalie hili"

“Natambua kuna Walimu wengi tu karibu Elfu 6 au zaidi ambao wamestaafu, wamefariki n.k na kunahitajika wakuziba nafasi hawa sio ajira mpya ni wa kuziba nafasi, Utumishi mko hapa na TAMISEMI mkalisimamie, Walimu Elfu 6 warudishwe haraka ili wakawatumikie Watanzania”

“Tumezoea tunapokwenda kwenye ziara Mikoani na Wilayani, tunapokewa na mabango ya Wananchi wakilalalimikia kero mbalimbali na mabango yale sio mambo ya kushughulikiwa ngazi za juu, naomba tunapokuja Mimi, Makamu wa Rais, tukikuta bango iwe mambo ya Kitaifa".

“Nataka niseme tukikuta bango moja aidha Mkurugenzi au Mkuu wa Wilaya umekwenda na hii haina maana mkazuie Watu kuandika kero zao, kero za Wananchi mkashughulikie na tukikuta malalamiko kwamba mnawafinya wasiseme hivyohivyo tutawashughulikia”.

“Naomba TAMISEMI mkakusanye mapato na matumizi yakafuate sheria na kanuni, nimemleta Mwana-Mama madhubuti (Ummy Mwalimu) nimempa Katibu Mkuu mzuri na Wasaidizi ni imani yangu kuwa kazi itafanywa”

“Najua TAMISEMI ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi na hiyo kazi itafuata hivi karibuni (Uteuzi na Utenguzi), ili safu itimie na kazi iende ikafanywe....Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Kazi Iendelee)”

"Tumewateua sio kwenda kuwa bughudha au kikwazo katika kazi, tumewateua ili mwende kuchapa kazi"

“Kuna ajira mpya za Madaktari upande wa afya, tumemaliza Hospitali na Vituo vingi, Bajeti ya mwaka huu ni kuweka vifaa na Watumishi kwahiyo Utumishi na TAMISEMI mkalisimamie hili la Watumishi na vitendea kazi kwenye huduma za afya”

"Wataalamu wamalize suala la bima ya afya kwa wote ili ijulikane kama linatekelezeka au la"

"Nakusudia kuunda timu ya wataalamu kuliangalia suala la Covid-19, waliangalie kwa upana wake, kuhusu tiba zetu, Tanzania sio kisiwa, lakini pia hatuwezi kukubali kila tutakacholetewa bila ya kufanya utafiti wa ndani"

“Rais Kikwete alituambia akili za  kuambiwa changanya na zako, tuweke na zetu tuwe na msimamo maalum unaoeleweka, sio tunasoma tu mambo ya Covid 19 Ulimwenguni, Tanzania deshi deshi deshi haieleweki, tueleweke kama tunakubali au tunakataa"

"Wanaosimamia vibali vya kazi  wamegeuka kuwa miungu watu, na wamegeuza kuwa ni sehemu ya kupiga pesa, mwekezaji akitaka kuwekeza hadi apate vibali atateseka hadi akipata dola elfu 10 imemtoka"

"Ndugu zangu, wawekezaji wamechoshwa na urasimu katika mchakato wa uwekezaji nchini kwetu. Ninaomba tuvute wawekezaji waweze kurudi tena Tanzania ,tupate ajira na pesa zizidi kuingia.

"Naomba tuvutie tena uwekezaji Tanzania, wawekezaji waje, kuna wawekezaji wengi wananipigia simu na kuwapigia simu wasaidizi kuwa wanataka kuonana na mimi, ili niwahakikishie mazingira ya biashara ili waje kuwekeza, tukarudishe imani kwa wawekezaji"

“Makampuni yanafungwa sio uongo kutokana na kero wanazokutana nazo wawekezaji, waacheni 'wa-enjoy’ kufanya biashara Tanzania”

"Najua tuna ubia na Barrick, lakini nafahamu pia kuna changamoto ndani yake, kuna suala la kodi halijakaa vizuri, hakuna haja ya kutunishiana misuli, maana tunafaidika pia" 

"Tumejenga ukuta mrefu Mirerani, na kuna wanajeshi wanalinda, jamani bado madini yanatoroshwa"

"Watu wa TRA kama kuna kodi ambazo hamuwezi kusamehe peke yenu zipandishe huko juu ili msaidiwe. Kodi tunazitaka, tena nawaambieni nendeni mkakusanye kodi, lakini kodi za dhuluma hapana kwa maana hazitutafikisha kokote"

"Watu wengi wameporwa ardhi, na waliofanikisha uporaji wa ardhi ni maofisa we ardhi, nendeni mkalisimamie hili, mkawasimamie watu wa wilayani, huko ndio kuna dhuluma kunwa"

"Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, na muwaelekeze kuhusu kanuni, na kanuni ziwe wazi kwamba kosa hili adhabu yake ni hii, msivifungie kwa mabavu"

“Wizara ya Habari, nasikia kuna Vyombo vya Habari mmevifungiwa, sijui 'Vi-TV' vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, tusiwape mdomo wa kusema tunabinya Uhuru wa Vyombo vya Habari, tusifungie tu kibabe” 

"Nimebahatika kukaaa na wakandarasi, moja ya manung'uniko yao ni kuwa, malipo ya fidia yanachelewa, wanasaini leo mkataba lakini malipo ya fidia yanakuja kulipwa muda mrefu baadaye"

"Mimi nilivyoingia kuwa Makamu wa Rais nilishughulika na suala la mradi wa kusindika gesi asilia(LNG), nilivyoona misuli yangu midogo nikaachana nalo, nadhani tufanye kama tulivyofanya kwenye SGR, walipotaka kutuvuta nyuma, tukaamua kwenda na mmoja, na tunajenga"

"Kuna suala moja katika mawasiliano, siku hizi kila mmoja anayekuja kuwekeza katika mawasiliano anataka kuweka mkongo wake, kwanini wasutumie mkongo wetu wa Taifa, hii ni kwa usalama wetu"

"Najua mfuko wa PSSSF una hali mbaya, sikutaka kuteua mtu kwanza, hadi niangalie angalie kwanza"

"Tukasimamie ilani ya CCM, mkiisimamia tutarudi tena hapa, msipoisimamia vizuri, wananchi nao wana maamuzi yao, twendeni tukaisimamie ilani vizuri "

0 comments :

 
Top