Arusha: Mashuhuda wa tukio la mlipuko wa bomu uliotokea mwishoni
mwa wiki iliyopita Jijini Arusha, wamedai kumwona na kumtambua mtu
aliyehusika na tukio hilo lakini wanasema walishidwa kumkamata kutokana
na “kushambuliwa kwa risasi na polisi”.
Mlipuko huo ulitokea katika Viwanja vya Soweto
kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani jijini humo na
kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi zaidi ya 100.
Mashuhuda hao ambao wote walijeruhiwa kwa risasi
wanasema mlipuaji wa bomu alikuwa amevalia shati la kijivu lenye mistari
myeusi na suruali ya jeans yenye rangi ya blue na kwamba wajihi wake ni
mtu wa kimo cha kati.
Mmoja wa mashuhuda hao ni mlinzi katika Kikosi cha
Ulinzi cha Chadema (Red Brigade) ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini, alidai kwamba alimwona mtu aliyerusha bomu mara tu baada ya
tukio hilo.
Mlinzi huyo ambaye alipigwa risasi za mguuni na
kifuani wakati akimkimbiza mtu huyo, alisema bomu hilo lililipuka mara
tu baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia na
kushuka jukwaani.
“Baada ya Mwenyekiti Freeman Mbowe kushuka
jukwaani, nikawapanga walinzi kwa ajili ya kuwalinda viongozi waliokuwa
wakichangisha fedha. Ghafla nikasikia mlipuko, sikujua ni nini, lakini
kuna mama mmoja alikuwa karibu yangu akanionyesha mtu aliyelipua,
akisema yuleee…” alisema na kuongeza:
“Alikuwa amevaa shati la kijivu lenye mistari
myeusi na suruali ya jeans ya blue. Ni mtu wa kimo cha kati. Watu
walianza kumkimbiza kuelekea upande wa Magharibi wa Uwanja kwenye nyumba
za NHC. Tuliruka uzio alipopita yule mtu, mara nikasikia risasi
imenipata mguuni.”
“Tulikuwa na uwezo wa kumkakata yule mtu, lakini
nikaona risasi zimezidi upande wetu nikaona nigeuze na hapo hapo
nikapigwa risasi ya kifuani, nikaishiwa nguvu, sikuweza kufahamu mtu
huyo alikoishia. Nilijikongoja na kurudi uwanjani.”
0 comments :
Post a Comment