MBINU zinazosukwa na vigogo wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu
Nchemba ili kukidhohofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
jijini Mwanza zimefichuka.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu (NEC) na Mwigulu wanatajwa kutaka kutumia harambee ya kuchangia
wafanyabiashara wadogo (Machinga) eneo la Makoroboi jijini hapa leo ili
kufanikisha hujuma zao hizo za kisiasa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA
Kanda ya Magharibi, Peter Makere, kupitia idara yao ya usalama
wamefanikiwa kunasa mikakati hiyo ya kutaka kuwadhoofisha.
Alisema kuna baadhi ya makada wa CCM
wamejipanga kuhujumu kadi na baadhi ya vifaa vya uenezi vya CHADEMA kwa
ajili ya kuvirudisha kwenye harambee hiyo ili kuhadaa umma kuwa chama
hicho hakikubaliki.
Makere alisema kuwa mgeni rasmi wa
harambee hiyo, ametajwa kuwa ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Lowassa ambaye
ataongozana na makada wengine wa CCM, akiwemo Mwigulu.
“CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi,
imebaini mbinu chafu na ovu zinazopangwa na makada wa CCM kuhujumu kadi
na vifaa vyetu. Hujuma hizi zinaandaliwa ili kuuhadaa umma eti CHADEMA
haikubaliki. Vifaa hivi vimepangwa kurudishwa kwenye harambee ya
kuchangia machinga itakayoongozwa na Lowassa,” alisema.
Alisema kuwa CHADEMA kama chama makini
na chenye dira thabiti ya kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye makucha ya
CCM yaliyojaa umasikini, wanaomba umma upuuze hujuma hizo na kuendeleza
mapambano ya kuiondoa madarakani 2015.
Aidha, Makere aliwaomba wamachinga na
wananchi wa Jiji la Mwanza bila kujali itikadi zao wapokee fedha za CCM
na waongeze ujasiri na mbinu za kuiondoa madarakani katika uchaguzi mkuu
ujao.
Alisema muda huu ni wa msimu, kwani
baadhi ya viongozi wa CCM wanaotafuta urais kwa gharama kubwa kupitia
makanisa na misikitini, wameanza kujipendekeza ili waungwe mkono, hivyo
ni vema Watanzania wakawaogopa watu hao kama ukoma.
“CCM lazima ibadilike, iachane na siasa
uchwara, hadaa, ghiliba na mazingaombwe. CHADEMA tunataka chama hicho
kupitia viongozi wake kiwaambie Watanzania kimewafanyia nini katika
sekta za elimu, afya, maji, ajira kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru,”
alisema Makere.
Wabunge wamtega spika
Kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda
kushindwa kuahirisha Bunge kama sehemu ya kutoa nafasi kwa wabunge
kuomboleza vifo vya wafuasi wa CHADEMA waliolipuliwa kwa bomu jijini
Arusha, kimezidisha uhasama baina ya taasisi hiyo na wabunge wa chama
hicho, Tanzania Daima limebaini.
Uhasama huo umefikia hatua ya wabunge wa
CHADEMA kuazimia kukataa kukatwa fedha zao za posho ya kujikimu ambazo
hutolewa kama rambirambi ya Bunge pindi linapotokea tukio kubwa la vifo
na majeruhi wakati vikao vya Bunge vikiendelea.
Utamaduni huo umekuwa ukitumiwa na Bunge
kwa wabunge kukatwa posho zao za siku moja sh 80,000, jambo ambalo
halikufanyika kwa waathirika wa tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha
la Juni 15 mwaka huu, kwenye mkutano wa CHADEMA eneo la Soweto, ambako
watu wanne walipoteza maisha na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wabunge hao
wa CHADEMA waliweka msimamo huo wakiwa jijini Arusha walikoweka kambi
wiki nzima kwa ajili ya kuomboleza wafuasi wao waliopoteza maisha na
kuwasaidia majeruhi.
Baada ya kupitisha azimio hilo,
walimkabidhi jukumu mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni ambaye
pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ili kuhakikisha
anafikisha taarifa hiyo kwa uongozi wa Bunge.
Akithibitisha juu ya azimio hilo jana,
Lissu alisema ni kweli waliazimia hivyo, kuwa hawako tayari kukatwa tena
fedha zao na uongozi wa Bunge bila ridhaa yao.
“Kama uongozi wa Bunge haukuona msiba wa
wafuasi wetu Arusha ni msiba unaowahusu wabunge wote, basi
wasituhusishe kwa kuchangisha kwenye misiba wanayoitambua wao,” alisema
Lissu.
Mbunge mwingine wa CHADEMA kutoka Kanda
ya Ziwa ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si
msemaji wa chama, alisema kuwa ni jambo la ajabu kuona wakati wote
yanapotokea majanga makubwa ya kitaifa, wabunge wote wamekuwa
wakishikamana na kuchangia posho zao bila kujali wanamchangia nani, wa
itikadi wala dini gani.
“Wakati Bunge likiendelea, Mtwara
kulitokea vurugu mara mbili na Bunge likaahirishwa mara zote mbili.
Wabunge tulichangia posho zetu za siku moja kwa waathirika wa matukio
hayo bila kujali ni wakina nani. Hata wakati wa mlipuko wa bomu kwenye
Kanisa Katoliki eneo la Olasiti jijini Arusha tulifanya hivyo hivyo na
Bunge lilituma wawakilishi wake kuwajulia hali waathirika.
“Lakini tunajiuliza ni kwanini
lilipotokea tukio la mlipuko kwenye mkutano wetu na wafuasi wetu kupata
matatizo, Bunge liliendelea na vikao kama kawaida, Spika wa Bunge wala
wabunge wa CCM hakuna aliyetuma rambirambi wala kushiriki mazishi au
kupeleka wawakilishi. Utaratibu wetu wa kuchangia posho zetu nao
haukufanyia,” alisema.
Aliongeza kuwa ni kwa sababu hiyo
wabunge wote wa CHADEMA waliazimia kuachana na utaratibu huo wa kukatwa
posho zao kuchangia misiba bila ridhaa yao, kwani Spika wa Bunge na
viongozi wenzake wa serikali walikuwa na ajenda yao ya siri katika tukio
hilo la Arusha, ndiyo maana waliwabagua wafuasi wa CHADEMA wakiwafanya
kana kwamba si Watanzania.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, kumekuwa
na mvutano mkali baina ya Bunge na CHADEMA hatua iliyowafanya hata
wabunge hao kususia kuingia bungeni kuipitisha bajeti ya serikali kwa
mwaka 2013/14.
Akifafanua hatua hiyo ya kususia
upitishaji wa bajeti, Lissu alisema kuwa tukio la bomu kwa wafuasi wao
halikuwa la bahati mbaya, lakini walijiuliza ni kwanini Bunge
halikuahirishwa walau kwa siku moja kama ilivyo utamaduni ili kushiriki
kuomboleza msiba huo.
Alisema kuwa pamoja na kwamba kiongozi
wao wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na
Godbless Lema wa Arusha Mjini ndio walikuwa wamelengwa kulipuliwa, bado
Spika wa Bunge wala Waziri Mkuu hakuna hata mmoja aliyetuma salamu za
pole kwa viongozi hao.
“Waliolengwa kulipuliwa ni Mbowe, Lema
na James ole Millya, maana hata risasi zilizowaua wale wafuasi wetu
wanne zilikuwa zikielekezwa kwa viongozi hao. Sasa tunajiuliza Bunge
liliona waliokufa Arusha ni Watanzania, lakini kwa vile walikuwa kwenye
mkutano wa CHADEMA haiwahusu, hivyo kama wanajifanya hakuna kilichotokea
sisi tungeingia bungeni kufanya nini?” alisema.
Lissu alitaja sababu nyingine kuwa siku
zote kila unapotokea msiba mkubwa wa kitaifa wakati Bunge likiendelea na
vikao vyake, wamekuwa wakitumwa wawakilishi kuwafariji wafiwa na
majeruhi, lakini kwa tukio la Soweto, Bunge halikutuma mwakilishi wake.
Alifafanua kuwa walichukizwa na kitendo
cha Spika wa Bunge kupindisha ratiba ya Bunge ili kuwanyima nafasi
wabunge wa CHADEMA wasijadili bajeti hiyo, na hivyo kuhoji wangeingia
kupitisha kitu gani ambacho hawakushiriki.
“Hatukuweza kuwasilisha maoni ya kambi
kutokana na tukio la Arusha, lakini kulingana na ratiba tulimaliza
mazishi siku ya Ijumaa tukijua kabisa Jumatatu tungepewa muda wetu wa
nusu saa kuwasilisha maoni ya kambi.
“Sio hivyo tu, bali hata wale walioomba
kuchangia wangepata nafasi ya kufanya hivyo halafu sasa Jumanne bajeti
hiyo ingepitishwa kwa mujibu wa ratiba. Lakini kutokana na hofu kuwa
tungejibu mapigo kuhusu madai ya Arusha, waliamua kufanya mbinu za
kutunyima nafasi,” alisema.
0 comments :
Post a Comment