TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

makada
MAKADA watano wa Chadema wameendelea kusota rumande, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, kusema haina uwezo wa kusikiliza kesi inayowakabili ya ugaidi. Washitakiwa hao walifika mahakamani hapo jana saa 4.12 asubuhi, wakiwa kwenye gari la Polisi na kuwekwa rumande ambako walikaa kwa takribani saa moja.
Baada ya hapo, washitakiwa hao wote walitolewa rumande na kufikishwa chumba cha Mahakama, ambapo Wakili wa Serikali, Juma Masanja, aliwasomea makosa ya ugaidi yanayowakabili, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Issa Ibrahim Magori.
Wakili Masanja alipomaliza kusoma makosa hayo, ya kumteka mfuasi wa CCM, Musa Tesha na kumdhuru kwa kumwagia tindikali, Hakimu Magori alisema Mahakama hiyo haina uwezo wa kimamlaka wa kutoa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa utetezi.
Alipendekeza maombi hayo, yawasilishwe katika Mahakama Kuu, yenye uwezo huo wa kimamlaka wa kupatia shauri hilo ufumbuzi wa kisheria. Baada ya kauli hiyo, washitakiwa hao walirudishwa mahabusu huku kukiwa hakuna maelezo ya lini watasomewa mashitaka yao.
Washitakiwa hao ni Evodius Justunian (30), mkazi wa Bukoba, Oscar Kaijage mkazi wa Shinyanga, Seif Magesa mkazi wa Nyasaka, Mwanza, Rajabu Daniel mkazi wa Dodoma na Henry Kileo, mkazi wa Dar es Salaam.
Kuachiwa huru Igunga Awali Juni 31, watuhumiwa hao waliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, kabla ya kukamatwa tena na kupelekwa Tabora kufunguliwa kesi ya ugaidi na ya kudhuru mwili kwa tindikali.
Kesi hizo mbili zilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, chini ya mawakili wa Serikali Masanja na Edelfonce Mkandala, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa, Joctan Rushwera.
Hata hivyo, kuliibuka mvutano kati ya mawakili wa Serikali na wa washitakiwa, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari, kuwa kesi hiyo ni batili, kwani baadhi ya vifungu vya sheria vilikiukwa wakati inafunguliwa.
Mawakili hao walidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya ugaidi, isipokuwa Mahakama Kuu ya Tanzania pekee. Pia walidai kuwa kwa sababu washitakiwa hao walikamatwa sehemu tofauti nchini, kesi zao zilipaswa kusikilizwa maeneo waliyokamatiwa.
Kutokana na mvutano huo, Hakimu Mkazi Rushwera, aliomba muda zaidi ili kupitia upya kesi hiyo na kutoa uamuzi kama ni kuendelea na kesi hiyo kusikilizwa au itupiliwe mbali, na alitoa muda baada ya kushauriana na mawakili wa pande mbili kuwa kesi hiyo itajwe tena jana.
Kauli ya Chadema Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Tabora, Athumani Barozi, akizungumza nje ya Mahakama, alisema chama hicho kina imani na vyombo vya Dola hususan Mahakama kutokana na utendaji wake.
Alitaka wanachama kuwa wavumilivu kwa wakati huu mgumu, huku wanasheria wa chama hicho wakiendelea kupambana kuhakikisha haki inatendeka, kulingana na tuhuma zinazowakabili.

0 comments :

 
Top