Mkutano wa Smart Partnership
Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa kwanza ni wale waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global 2013 Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013. Mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 800
kutoka mabara yote duniani wakiwemo Watanzania. Miongoni mwa
waliohudhuria ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu,
wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa,
makampuni ya ndani na nje, wafanyabiashara, wasomi, asasi za kijamii na
watu wa makundi mbalimbali katika jamii. Makampuni yetu 21 nayo yaliungana na makampuni mengine 28 kutoka nje ya nchi kushiriki kwenye maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na mkutano huo.
Ndugu Wananchi;
Agenda kuu ya majadiliano ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika (Leveraging Technology for Africa’s Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way).
Tuliichagua mada hii kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa matumizi ya
sayansi na teknolojia ndiyo chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo
ya kiuchumi na kijamii katika nchi. Ndiyo siri ya mafanikio katika nchi
zilizoendelea na zinazopiga kasi kubwa ya maendeleo duniani.
Bahati mbaya sana kumekuwa na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi na
teknolojia katika Afrika. Ndiyo maana nchi za Afrika ziko nyuma
kimaendeleo ukilinganisha na zile zilizoendelea. Katika mkutano huo
umuhimu wa kuendeleza na kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia kwa
ajili ya maendeleo Barani Afrika ulitambuliwa na kusisitizwa.
Mkutano ulihimiza na kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya
maendeleo ya nchi za Afrika zitoe kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya
sayansi na teknolojia. Nchi zetu zimehimizwa kuwekeza katika elimu ya
sayansi na teknolojia pamoja na kujenga uwezo wetu wa ndani wa uvumbuzi,
ubunifu, umiliki na uendelezaji wa sayansi na teknolojia. Aidha,
imesisitizwa kwa nchi zetu ziongeze kasi ya kutumia sayansi na
teknolojia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili
kuongeza ufanisi na kasi ya maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kutia faraja kwetu nchini ni kwamba mambo yote hayo
tunayafanya. Tunachotakiwa sasa ni kufanya vizuri zaidi na kuongeza
uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia katika
shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Tutaendelea
kuboresha sera, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya
maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.
Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Mgeni wetu wa pili alikuwa Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama,
aliyefanya ziara nchini kwetu kati ya tarehe 1 - 2 Julai, 2013. Lengo
la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya
Marekani na Tanzania. Kama mjuavyo, nchi zetu mbili zina uhusiano wa
kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar mwaka 1964.
Uhusiano wetu umepita katika vipindi mbalimbali na kwamba hivi sasa
umekuwa mzuri zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya
nchi zetu mbili. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la misaada ya maendeleo
kutoka Marekani na uwekezaji wa vitega uchumi na biashara navyo vinakua.
Pia ziara za kiserikali za viongozi wa nchi zetu kutembeleana
zimeongezeka. Kama mtakavyokumbuka, mwaka 2008 aliyekuwa Rais wa
Marekani Mheshimiwa George W. Bush alifanya ziara ya siku nne nchini.
Pia Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Marekani wametembelea Tanzania
akiwemo Mheshimiwa Hilary Clinton akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani aliyekuja mwaka 2011.
Ndugu Wananchi;
Nchi ya Marekani imekuwa mshirika wetu muhimu wa maendeleo katika nyanja
mbalimbali. Kwa upande wa afya kwa mfano, tunapata msaada mkubwa
katika mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI. Katika maendeleo ya elimu,
nako wanatusaidia katika mafunzo ya wataalamu mbalimbali pamoja na
upatikanaji wa vitabu vya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za
sekondari. Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia, Marekani inatusaidia
katika kuimarisha miundomuinu ya barabara, umeme na maji. Ujenzi wa
barabara za Tanga – Horohoro, Namtumbo – Songea – Mbinga; Tunduma –
Sumbawanga na baadhi ya barabara za Pemba, ujenzi wa njia ya pili ya
kupeleka umeme Unguja kutoka Dar es Salaam, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Mafia na usambazaji wa umeme katika Mikoa 10 ya Tanzania bara ni
miongoni mwa matunda ya msaada wa Mfuko huo. Pamoja na hayo, ipo miradi
ya kuongeza maji katika jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Morogoro
ambayo inaendelea kutekelezwa.
Ndugu Wananchi;
Wakati wa ziara yake, Rais Obama alielezea na kusisitiza dhamira yake na
ya Serikali yake ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri
uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea kuridhika na hatua tuliyofikia ya
kukuza demokrasia nchini, utawala bora na kuwekeza katika maendeleo ya
watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zetu. Katika hili
ameahidi kuongeza misaada ya maendeleo na kiufundi katika sekta za afya,
elimu, kilimo, barabara, nishati na maendeleo ya vijana. Pia,
alithibitisha kwamba nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu
ya Pili ya Mfuko wa Changamoto za Millenia. Katika awamu hii, maeneo
yatakayopewa kipaumbele hapa kwetu ni umeme na barabara za vijijini.
Mazungumzo ya miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo yanaendelea
vizuri.
Power Africa
Ndugu Wananchi;
Rais Obama alitumia fursa ya ziara yake nchini kuzindua mpango wa
Serikali yake wa kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme katika Bara la
Afrika. Mpango huu unaoitwa “Power Africa Initiative” umetengewa kiasi
cha dola za Marekani bilioni 7 na Serikali ya Marekani na makampuni binafsi ya nchi hiyo yameahidi kuwekeza dola bilioni 9 katika mpango huo. Kwa kuanzia, nchi sita za Afrika (Ethiopia, Ghana, Nigeria, Tanzania, Liberia na Kenya) ikiwemo Tanzania zitahusishwa.
Bila ya shaka Mpango huo ukikamilika utasaidia sana kuimarisha
upatikanaji wa umeme barani Afrika ambayo ni nyenzo muhimu katika kuleta
maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni ukweli ulio wazi kuwa ukosefu wa
umeme wa kutosha na wa uhakika ni sababu kubwa inayokwamisha maendeleo
ya haraka katika nchi za Afrika. Hivyo basi, msaada huu ni muhimu sana
kwetu. Kwa ajili hiyo nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini iandae
mkakati madhubuti wa namna Tanzania itakavyoshiriki na kufaidika na
mpango huo. Nataka mpango huo utakapoanza kutekelezwa utukute sisi tupo
tayari kutumia fursa zake.
Vile vile, ndugu wananchi, katika ziara hiyo Rais Obama alielezea nia ya
Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza ushirikiano wa biashara na
uwekezaji baina ya nchi yake na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeelekeza Wizara husika yaani Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko nao watengeneze
mkakati utakaoonesha jinsi tulivyojipanga kufaidika na mpango huo.
Lazima tujiandae vyema na mapema tunufaike saiwa na mpango huo.
Ziara ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini
Ndugu Wananchi;
Sambamba na ziara ya Rais Obama, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa
tena na Rais Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush na mkewe
Laura Bush, tarehe 1 hadi 3 Julai, 2013. Kwa udhamini wa asasi ya
George W. Bush Foundation waliandaa Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika
uliofanyika hapa Dar es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai, 2013. Mama
Michelle Obama naye alishiriki mkutano huo uliozungumzia kuimarisha
maendeleo na afya ya wanawake Barani Afrika.
Katika mkutano huo, pia, Mheshimiwa George W. Bush alizindua mpango wa
kuimarisha mapambano dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi na matiti barani
Afrika. Kufuatia Mpango huo, Serikali ya Marekani imetoa dola milioni 3
na mashine 16 za Cryo Therapy zinazotumia baridi kali kuua chembechembe
za kansa. Msaada huo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kila mwaka hapa
nchini zaidi ya Watanzania 21,000 wanapata maradhi ya kansa. Kati ya
hao asilimia 29.4 ni wanawake wanaopata magonjwa ya kansa ya shingo ya uzazi na asilimia 6.2
wanapata kansa ya matiti. Naamini Mpango huu utatusaidia sana katika
kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi haya yanayowasumbua na kuua kina
mama wengi nchini. Nimeitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka
utaratibu mzuri ili msaada huo utumike ipasavyo na kuwanufaisha
walengwa.
Ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi Julai, 2013 pia tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa
Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair. Katika mazungumzo yetu Mheshimiwa
Blair aliahidi kuisaidia nchi yetu kupitia taasisi yake ya Africa
Governance Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua katika shule zetu
za sekondari vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme (TANESCO) na
kusaidia uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji
Utekelezaji wa Programu za Maendeleo (Presidential Delivery Bureau -
PDB). Tunamshukuru kwa ahadi yake hiyo itakayochangia katika jitihada
za kujiletea maendeleo.
Ziara ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Julai, 2013 tulimpokea Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri
Mkuu wa Thailand aliyefanya ziara ya siku tatu nchini. Lengo la ziara
yake ni kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Thailand na Tanzania.
Katika ziara hiyo, tumezindua Jukwaa la Wafanyabiashara wa Thailand na
Tanzania (Thai-Tanzania Business Forum) ili kukuza biashara na uwekezaji
baina ya nchi zetu. Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra alitumia fursa
hiyo kufafanua sera ya Thailand kwa Afrika inayosisitiza kukuza
ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na kibiashara. Pia amepata nafasi ya
kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea mwenyewe jinsi nchi
yetu ilivyobarikiwa kwa kuwa na kivutio hicho cha aina yake. Alipokuwa
kule nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika kulinda
na kuhifadhi wanyama pori.
Katika mazungumzo yangu na yeye, tumekubaliana kuchukua hatua thabiti
kukuza ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Tumetiliana saini mikataba
mitano ya ushirikiano kwa mambo yafuatayo: Kukuza na kulinda vitega
uchumi; kubadilishana wafungwa; ushirikiano wa kiufundi; na ushirikiano
kwa masuala ya madini. Aidha, Waziri Mkuu huyo ameahidi kuwahimiza
wawekezaji wa nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika sekta
mbalimbali za uchumi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda nakadhalika.
Pia, Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake itatoa
ufadhili kwa vijana 10 kusoma Shahada ya Uzamili nchini humo.
Vile vile, nchi hiyo itaanza kuleta wataalamu wa afya wa kujitolea kuja
kushirikiana na wataalam wetu kuimarisha huduma ya afya nchini.
Ziara hizi zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada zetu za
kujiletea maendeleo. Naomba Watanzania wenzangu tutumie vizuri utayari
huo wa dunia kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.
Home
»
»Unlabelled
»
RAIS KIKWETE ATOBOA SIRI YA UJIO WA OBAMA, BUSH NA WAGENI WENGINE WOTE WALIOTEMBELEA TANZANIA MWEZI JULAI
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment