TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi. Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.

Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.

Ndugu Wananchi;

Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.


Source: Hotuba ya Rais Mwisho wa Mwezi Julai 2013

0 comments :

 
Top