Viongozi wa Chadema wakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara jana muda mfupi baada ya kukamatwa wakijaribu kuandamana. Viongozi hao walisomewa shtaka la kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria . Picha na Emmanuel Chacha
Bunda/Dodoma/Dar. Polisi wilayani Bunda jana walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wachache wa Chadema waliokuwa wanajiandaa kuandamana.
Tukio hilo lilitokea jana saa 5.40 asubuhi muda mfupi baada ya wafuasi hao kujipanga kuanza maandamano yaliyokuwa yaanzie Nyasura hadi Stendi ya zamani walikotarajiwa kufanya mkutano wa hadhara.
Katika purukushani hiyo, Polisi waliwatia mbaroni watu 13 akiwamo kada wa CCM, wakidaiwa kuandamana bila kibali.
Muda mfupi baadaye, watu hao wakiwamo Mwenyekiti wa Wilaya ya Bunda, Israel Mwinura, Mwenyekiti wa Jimbo la Bunda, Samuel Imanani, Diwani wa Kata ya Balili, George Miyawa na Katibu Mwenezi wa Jimbo la Bunda, Emmanuel Machumu, walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Bunda ambako walisomewa mashtaka ya kufanya mkusanyiko bila kibali.
Mwendesha Mashtaka, Masoud Mohamed aliieleza Mahakama hiyo kuwa washtakiwa kwa pamoja jana saa 2.00 asubuhi walifanya mikusanyiko bila kibali katika eneo la Nyasura mjini hapa. Aliiomba mahakama iwanyime dhamana kwa madai kuwa hali ya usalama wa eneo kulikofanyika mkusanyiko huo siyo shwari na kwamba, wanawatafuta watuhumiwa wengine waliofanikiwa kutoroka.
Mjini Dodoma, viongozi watatu na wanachama wengine wawili wa Chadema nao walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Waliofikishwa mahakamani ni Christopher Nyamanchi, Laurent Mangweshi, Agnes Stehano, Tuli Kiwanga na Elisha Daudi.
Wakili wa Serikali Chivanda Luwongo, alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Dodoma, Verynice Kawiche kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 18, mwaka huu katika kituo cha Mafuta cha Four Ways mjini hapa.
Hata hivyo, Chadema wamesisitiza kufanya maandamano leo jijini Dar es Salaam kama kilivyopanga ili kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba, alisema Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso amewataka wananchi kutoshiriki maandamano hayo kwa maelezo kuwa yanafanyika kinyume na sheria na watakaokaidi amri hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
0 comments :
Post a Comment