Kilimanjaro. Mwanamke mmoja mkazi wa Kibosho mkoani Kilimanjaro amekamatwa na polisi akidaiwa kumkata mtoto wake mwenye umri wa miaka minane nyama katika eneo la paja na kuichoma mithili ya mshikaki.
Mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina la Dafrosa Massawe anadaiwa kufanya kitendo hicho mwishoni mwa wiki na majirani wanasema mama huyo alifanya kitendo hicho akiwa amelewa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita alisema mwanamke huyo anashikiliwa na polisi wakati uchunguzi wa tuhuma hizo ukiendelea kabla ya kupelekwa mahakamani.
Akizungumza katika Hospitali ya Kibosho alikolazwa, mtoto huyo alisema hafahamu kosa ililofanya hadi mama yake ambaye ni mtengenezaji na muuzaji wa pombe za kienyeji kumfanyia kitendo hicho.
Alisema siku ya tukio, mama huyo alirudi nyumbani usiku na kumkuta amekaa na alimsalimia kisha akamwomba chakula. Alisema mama huyo aliingia jikoni na kuchukua kisu kisha kumkata nyama kwenye paja.
Alisimulia kuwa baada ya kuikata aliichoma kama mshikaki na ilipoanza kufuka moshi na kutoa harufu, aliitoa jikoni na kumwekea mtoto huyo puani ili avute harufu yake.
“Sikuwa nimekula chochote siku nzima... nikamwambia nina njaa, akanishika na kunikata kwenye paja kwa kisu halafu akaichoma nyama, ilipokuwa inatoa harufu akaniambia niinuse ili nisikie harufu ya nyama yangu ilivyo nzuri,” alisema.
Mtoto huyo anayesoma darasa la pili, alisema mama yake amekuwa na tabia ya kumpiga mara kwa mara lakini hakutarajia amfanyie hivyo.
Katibu wa Taasisi ya kuwatembelea wagonjwa nyumbani (Wakuwanyu) iliyopo Tarafa ya Kibosho, Paul Lazaro alisema mtoto huyo ni miongoni mwa watu wanaopatiwa huduma na taasisi hiyo kutokana na mama yake kutomjali na kumfanya aishi katika mazingira magumu.
“Huyu mtoto tumekuwa tukimtembelea na kumpa msaada kwa kuwa anaishi kama mtoto aliyetelekezwa, ili apate chakula ni lazima aende kwa majirani kuomba na tulipopita nyumbani kwake hatukumkuta, ndipo tulipopata taarifa kuwa amelazwa baada ya mama yake kumkata na kuchoma nyama yake,” alisema Lazaro.
Mmoja wa majirani wa mama huyo, Bernadeta Method ambaye alimpeleka mtoto huyo hospitali, alisema amekuwa na uhasama na mama wa mtoto huyo kutokana na kumpa mtoto chakula pindi anapoachwa.
Alidai kuwa baada ya kukatwa kipande cha nyama, mtoto huyo alifanya siri baada ya kutishiwa na mama yake lakini kutokana na njaa aliamua kutoka nyumbani na kwenda kwa jirani kuomba, lakini kabla hajapatiwa chakula alianguka na jirani huyo alimchunguza na kugundua jeraha ndipo akampeleka hospitalini usiku.
0 comments :
Post a Comment