Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Marten Lumbanga.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) majina 10 ya taasisi na halmashauri ambazo zimeonekana kuwa na viashiria vya rushwa katika matumizi ya fedha za Serikali mwaka 2013/14.
Bodi hiyo pia imezifungia kampuni 23 kushiriki zabuni za Serikali, huku ikiagiza menejimenti ya PPRA kufanya uhakiki kwa taasisi 19 ambazo katika ukaguzi, zimeonyesha kufanya ununuzi unaotia shaka wa Sh1.7 bilioni.
Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Marten Lumbanga alisema jana kuwa taasisi zilizoonekana kuwa na viashiria vya rushwa katika ununuzi ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Manispaa ya Kinondoni na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi na Mamlaka ya Maji na Mazingira Lindi.
Halmashauri nyingine zinazotakiwa kuchunguzwa na Takukuru ni za Kondoa, Monduli, Kilwa, Maswa na Manispaa ya Musoma.
Nyingine ni Halmashauri za wilaya ya Kigoma, Kibondo, Tarime, Musoma, Ukerewe, Maswa, Kishapu, Kilindi, Lushoto, Mkinga, Bunda, Butiama, Rorya, Kondoa Songea, Singida, Mwanza, Iramba na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi.
Mkurugenzi Mtendaji wa PPRA, Dk Laurent Shirima alisema kuwa tatizo kubwa katika ununuzi wa umma ni watendaji kutokuwa makini au kutofanya kazi zao kwa uaminifu.
Alisema PPRA imekusudia kuwaita wakuu wa taasisi zilizofanya vibaya ili kujua tatizo.
0 comments :
Post a Comment