TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

                           
Pamoja na maswali mengi wanayojiuliza wananchi juu ya kitendawili kinachotakiwa kuteguliwa na Rais Kikwete loe, wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wana maoni tofauti kuhusu matarajio hayo. Mhadhiri wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema: “Kesho (leo) Watanzania wanaweza kufurahi au kukasirishwa. Nasema hivyo kwa sababu hatujui Rais Kikwete ameshauriwa nini kuhusu suala hili la escrow.”
Alisema ni vigumu kujua kama atatekeleza maazimio ya Bunge kwa kuwa kimya chake kililenga kupata ushauri wa chama chake cha CCM na Serikali.
“Kwanza kuna hii kesi iliyofunguliwa mahakamani kuzuia utekelezaji wa maazimio ya Bunge na hii kauli ya Profesa Tibaijuka kuwa hajiuzulu. Mambo hayo mawili bado yanatuweka njiapanda,” alisema Jesse.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Nina wasiwasi kama Rais atatekeleza maazimio ya Bunge. Kwanza, tangu aliporejea kutoka katika matibabu amekuwa kimya, hajazungumza kuhusu suala hili, ni kama wiki tatu sasa zimepita. Pili, ni Ikulu kusema kuwa inafanya uchunguzi kuhusu wahusika, wakati tayari uchunguzi umefanyika na Bunge limetoa maazimio.
Sasa huu uchunguzi mwingine wa kazi gani. Pia Profesa Tibaijuka ametamka wazi kuwa hawezi kujiuzulu. Kwa mambo hayo machache sidhani kama Rais atamwajibisha mtu hapo.”
Kuhusu kesi iliyofunguliwa mahakamani, Profesa Mpangala alisema: “Kwa nini kesi ifunguliwe sasa wakati maazimio ya Bunge yametolewa wiki zaidi ya tatu zilizopita?”
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Professa Tolly Mbwete alisema: “Sikuona sababu ya wahusika kuzungumza kabla ya aliyewateua kuzungumza kuhusu escrow na tuhuma zinazowakabili aliowateua.”
Alihoji sababu ya waliokwenda mahakamani kufanya hivyo na kusema hatua hiyo inazidisha maswali mengi kwa wananchi na kuwa mtihani kwa Rais.”
Hata hivyo, Profesa Mbwete alisema mahali suala la escrow lilipofikia, ni wakati mwafaka kwa Rais Kikwete kulimaliza kabisa: “Anatakiwa kuchukua hatua bila kuogopa jambo lolote. Si vyema kuendelea na jambo hili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.”
Chadema yataka Waziri wa Fedha, Gavana waingizwe
Mbali na wale waliotajwa katika maazimio ya Bunge, Chadema kimemtaka Rais Kikwete kuwawajibisha Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kwa kuhusika katika suala la escrow.
Kauli hiyo inafanana na ile iliyotolewa na Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliyesema Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa kuwa nazo zinahusika.
Viongozi wengine waliotajwa na Chadema kuwa wanastahili kuwajibishwa na Rais Kikwete leo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba.
Desemba 4, mwaka huu, Jaji Warioba alisema uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara ya Nishati na Madini lakini utoaji wa fedha hizo uliihusu zaidi Wizara ya Fedha na usajili wa Kampuni uliihusu Brela ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Arcado Ntagazwa alisema Watanzania wanasubiri Rais Kikwete kumchukulia hatua Mkuya kwa sababu wakati fedha za escrow zinatolewa BoT kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, alikuwa kaimu waziri wa fedha.
Kuhusu, Gavana Ndulu, Ntagazwa alisema anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu hakuna benki inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha bila BoT kuidhinisha.
“Kupitia Benki ya Stanbic, Sh160 bilioni zilibebwa kwa magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku moja, BoT hawawezi kukwepa kuwajibishwa kwa kuwa walifahamu kutolewa kwa fedha hizo,” alisema Ntagazwa.
Alisema Dk Likwelile akiwa mtendaji mkuu wa wizara alitakiwa kuzuia uchotwaji wa fedha hizo huku Mkurugenzi wa Tanesco, Mramba ambaye ndiye Katibu wa Bodi ya Tanesco anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu licha ya kufahamu uchotwaji wa fedha hizo hakuchukua hatua zozote.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, Benson Kigaila alisema chama hicho kimepata taarifa za kiintelijensia kwamba Rais Kikwete ana mpango wa kuwalinda Profesa Muhongo na Maswi.

0 comments :

 
Top