TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu      
 
Dodoma. Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana amewalipua baadhi ya mawaziri na wabunge kwa kugeuka ombaomba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza bungeni jana katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka 2014/15, Lissu alisema kuwa atawasilisha hoja binafsi katika Ofisi ya Spika ili iundwe tume kwa ajili ya kuwachunguza wabunge na mawaziri hao.
Huku akionyesha baadhi ya nyaraka ambazo wabunge hao wameiandikia mifuko hiyo ya jamii kuomba fedha, Lissu alisema kitendo hicho kimewafanya viongozi hao kusifia kila jambo linalofanywa na mifuko hiyo, hata kama ni baya.
Lissu alitoa kauli hiyo huku wabunge watano kati ya wanane waliomtangulia kuchangia mjadala huo, kuisifia mifuko ya hifadhi ya jamii nchini, huku wakimtaja kwa jina Mkurugenzi wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ramadhan Dau kwamba ni mfano wa kuigwa.
 
“Sifa hizi zina sababu yake. Kuna nyaraka na barua zinazoonyesha wabunge mbalimbali waliochukua fedha za mifuko hii kwa sababu mbalimbali,” alisema Lissu na kuongeza;
“Naomba baadaye Bunge liunde kamati teule ili kuichunguza mifuko hii na viongozi hawa.”
Hata hivyo, Lissu hakumalizia hoja yake hiyo baada ya muda wake wa kuchangia kumalizika na kutakiwa kukaa chini na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu.
Wahusika
Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho cha Bunge, Lissu alilionyesha gazeti hili nyaraka za vigogo hao zikionyesha wote wameomba kati ya Sh500,000 hadi Sh10 milioni.
Kati yao wapo mawaziri, naibu mawaziri ambao wameomba fedha hizo kwa ajili ya matumizi mbalimbali, huku baadhi yao wakieleza kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo katika majimbo yao, ikiwa pamoja na kununua jezi na mipira.
Sakata hilo pia linaihusisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambapo kigogo mmoja wa wizara hiyo (jina tunalo) ameomba mfuko mmoja wa jamii kumnunulia vifaa vya ofisi ikiwamo kompyuta kwa ajili ya matumizi ya wizara.
“Unaweza ukajiuliza maswali mengi. Wizara inaomba fedha katika mfuko wa jamii ili kununua kompyuta na vifaa vingine vya ofisi wakati ina bajeti ya ununuaji wa vifaa hivyo.
Ni wazi kuwa mhusika alikuwa akipeleka vifaa hivyo nyumbani kwake,” alisema Lissu.
Alisema atawasilisha hoja yake ili kuomba Spika aunde tume kwa ajili ya kufanya uchunguzi.
Awali, Lissu wakati akichangia mjadala huo alisema Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa miaka mitatu mfululizo ripoti yake inailalamikia mifuko ya hifadhi ya jamii kutumia fedha kuwekeza katika miradi isiyo na tija kwa mifuko yenyewe na pia wafanyakazi.
“CAG anaeleza katika ripoti zake kwamba Sh661 bilioni, ambazo mifuko ya jamii imewekeza katika miradi mbalimbali mpaka sasa hazijalipika. Fedha hizi zilitakiwa kuwekezwa katika miradi harafu zirudishwe kwa riba na CAG anasema fedha hizo hazilipiki” alisema Lissu.
Alisema kuwa taarifa ya CAG mwaka 2013/14 inaonyesha kuwa Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali (PSPF) una nakisi ya uwezo wa kulipa wanachama wao ya Sh6.4trilioni, kwamba fedha hizo ni za wafanyakazi na zimewekezwa katika mambo mbalimbali.

0 comments :

 
Top