Berlin, Germany. Zaidi ya watu 10,000 wamejitokeza katika uwanja wa ndege wa Berlin Tegel kuipokea timu yao ya taifa leo, kufuatia kutwaa kwake ubingwa wa Dunia kwa mara ya 4 mnamo Jumapili.
Vilio, nderemo na vifijo vilitawala uwanjani hapo pale ilipotangazwa kuwa ndege ilobeba timu hiyo toka Brazil imewasili, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya saa mbili asubuhi GMT.
Wapenzi wa Ujerumani walishaanza kukusanyika uwanja wa ndege toka alfajiri, huku maelfu wakiwa wamejipanga barabarani jirani na eneo hilo la Tegel wakisubiri mashujaa wao wawasili.
Ushindi wao dhidi ya Argentina katika uwanja maarufu wa Maracana mjini Rio de Janeiro uliiwezesha timu hiyo ya makinda kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza toka Ujerumani ya Kikabaila ya Magharibi na ile ya Kikomunisti ya Mashariki ziungane mwaka 1990.
Kabla ya kutwaa Kombe hilo katika michuano ya Brazil ya 2014, wa-Berlin hao wanaofahamika zaidi kwa jina la utani la ‘Die Mannschaft’ walishatwaa ubingwa mara 3, wakishiriki kama Ujerumani Magharibi.
“Hili ni tukio la kihistoria,” alisema dereva wa basi Bernd Hesse.
Akizungumza na AFP toka Tegel, Hesse alisisitiza kuwa Wajerumani wana haki ya ‘kujinafasi’ leo kwani wamekuwa wakisubiri huo ubingwa kwa takribani miaka 24.
“Mambo haya huyaoni kila siku,” alisema Hesse.
Meneja matangazo Lydia Lampa, 28, aliamua kupitia kwanza Tegel kuipokea Ujerumani kabla hata hajakwenda kazini. “Hivi ndivyo ninavyoionyesha shukrani [timu] yangu,” alisema Lampa.
Timu hiyo iloletea Ujerumani sifa kubwa ilitaraji kukutana na Meya wa Berlin Klaus Wowereit hapo baadaye, na kisha kwenda katika Gati Maarufu la Brandenburg ili kujumuika katika shamrashamra zinazoendelea.
Wakazi walojitokeza leo walionekana kuwa na raha, huku wakipeperusha kwa nguvu bendera za Ujerumani – jambo ambalo ni nadra kutokea kutokana na Ujerumani ya kale kutokuwa na historia nzuri.
Wengi walikuwa wametinga jezi zenye majina ya ‘masupastaa’ wao, kama vile Mueller, Schweinsteiger, Podolski, Goetze, Lahm na wengine wengi.
Katikati ya mashabiki leo alikuwapo Ulrich Felgentreff, aliyezaliwa miaka 60 ilopita wakati Ujerumani ikijaribu kukarabati mahusiano yake na mataifa mengine kufuatia maovu yaliyofanywa na uongozi wake kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
“Kwa kweli leo tunajivunia [tena] kuwa Wajerumani,” alisema Felgentreff, akiwa amevaa mavazi yenye rangi za bendera yake ya taifa. “Kila tunaposhinda Kombe, tunazidi kufurahia utaifa wetu.”
Shabiki mwingine aliyejitokeza ni Sven Engel, 18, ambaye hata hakuwa hai mara ya mwisho Ujerumani ilipochukua Kombe la Dunia.
Hata hivyo, suala hilo halikumzuia kufurahia ushindi wa timu yake ya taifa. “Ujerumani ilistahili tuzo hii,” aliiambia AFP akiongeza: “Tulikuwa bora zaidi ya timu nyingine zote.”
“Lakini mechi niliyoifurahia zaidi ilikuwa dhidi ya Brazili,” alisema Engel, akikumbushia zahama ilowakumba Selecao ya kunyukwa goli 7-1 na Wajerumani.


0 comments :
Post a Comment