1.Dhana ya Tafsiri.
Tafsiri imefasiliwa kuwa, ni
Kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha
maana. [TUKI 2002: 271]
Mwansoko na wenzake (2006),
wanafasili tafsiri kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi
kutoka lugha moja hadi nyingine.
Catford [1965:20] anasema
tafsiri ni, “Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja {lugha
chanzi} na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine {lugha
lengwa}.
AS-Safi akimnukuu Dubois
(1974), anaeleza kuwa tafsiri ni uelezaji katika lugha nyingine au lugha lengwa
wa kile kilichoelezwa katika lugha nyingine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na
mtindo wa matini chanzi.
Maana
zote hizo tulizoziangalia, utaona kuwa, kuna mambo matatu muhimu
yanayojitokeza, mambo hayo ni:
(i) Mawazo yanayotakiwa
kutafsiriwa sharti yawe katika maandishi.
(ii) Mawazo au ujumbe kati ya
lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.
(iii) Tafsiri inaweza kuwa
kutoa maana ya maneno au mawazo.
Kutokana na fasili hizo
tunaweza kusema kuwa tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe, au
taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha
lengwa bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi.
Fasili za dhana za msingi kama tafsiri,
mfasiri, n.k
Ø Tafsiri ni zoezi la kuhawilisha mawazo
yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Ø Mfasiri ni mtu anayefanya kazi ya
kutafsiri matini kutoka lugha moja hadi nyingine.
Ø Fasili ni kufafanua maana ya neno kwa
kina.
Ø Ukalimani ni uhawilishaji wa mawazo
yaliyo katika mazungumzo kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.
Ø Mkalimani mtu anayefasiri papo kwa papo mazungumzo
kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.
Ø Lugha chanzi/chasili ni lugha iliyotumiwa
katika matini chanzi
Ø Lugha lengwa ni lugha inatumiwa katika
matini lengwa.
Ø Matini chanzi/ chasili matini
inayotafisiriwa kwenda lugha nyingine
Ø Matini lengwa ni matini iliyotafsiriwa katika
lugha lengwa.
Mfasiri
Mfasiri
ni mtu anayefanya tafsiri kutoka lugha moja hadi lugha nyinge. {TUKI:2000:165}
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa, mfasiri ni mtu anayehamisha mawazo kutoka lugha
moja (lugha chanzi) kwa kutumia lugha nyingine ili mawazo hayo yaeleweke na
watu wasiojua au kuielewa lugha chanzi, na mawazo hayo sharti yawe katika
maandishi.
Sababu za kuanzishwa kwa
nadharia za tafsiri. Newmark (1982), Mwansoko na wenzake (2006) wanasema kuna
mambo matatu yaliyosababisha kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambayo ni:-
i)
Wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali; ilionekana kwamba,
kulikuwa na makosa mbalimbali kama vile makosa ya kimuundo, kimaumbo,
kimsamiati nk. Pia ilikuwa ni nadra/muhali kupata tafsiri zisizokuwa na makosa.
ii)
Kuwepo kwa idadi kubwa (na inayoongezeka) ya asasi zinazojishughulisha na kazi
za tafsiri. Hali hii ilisababisha kubuniwa kwa nadharia ya tafsiri ili kuwepo
kwa misingi inayokubalika. Mfano; nchini
Tanzania peke yake kuna asasi
nyingi zinazojishughulisha na tafsiri kama vile: BAKITA,TATAKI,
SHIHATA, WAFASIRI na vyombombalimbali vya habari kwa
mfano: TV, Magazetink.
iii)
Mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hasa Sayansi na Teknolojia. Hivyo
nadharia ya
tafsiri ilianzishwa kwa lengo
la kuleta ulinganifu wa istilahi hizo kati ya lugha moja na nyingine ili
Umuhimu wa tafsiri/mfasiri
Tafsiri
ina dhima zifuatazo:
§ Ni
njia ya mawasiliano
§ Nyenzo
ya kueneza utamaduni kutoka jamii moja hadi nyingine.
§ Mbinu
ya kujifunza lugha za kigeni
§ Mbinu
ya kukuza lugha
§ Mbinu
ya kuhamisha maarifa na ujuzi
§ Njia
ya kuongeza kipato{Kiuchumi}
2. Aina na mbinu za tafsiri
ü Tafsiri
ya neno kwa neno
Hii
ni tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pwekepweke kwa kuzingatia
maana zake za msingi bila kujali muktadha wala muundo wala utamaduni wa lugha
lengwa. Mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi haubadiliki,pia tafsiri
hii hulenga tu kupata maana ya kimsingi au ya kamusi. Katika tafsiri hii matini
iliyofasiriwa huandikwa chini ya matini ya
lugha
chanzi. Mfano
a) Kiingereza: this is a scien - tific text
Kiswahili: hii ni Ø sayansi – ki matini
b) Kiingereza: we will translate many more work - s
Kiswahili: tu – ta tafsiri n - ingi zaidi kazi – Ø
c) A
– li – safiri kwa basi.
S
/he |past| travel by bus.
Ambapo: Alama ya sufuri, Ø, huashiria kutokuwa kwa kisawe kwa vileumbo linganifu halitumiki katika lugha pokezi
ü Tafsiri
sisisi
Tafsiri
hii hutoa maana za kimsingi za maneno yakiwa pwekepweke kwa kuzingatia kanuni
za kisarufi za lugha lengwa hususani sintaksia. Mbinu hii haizingatii muktadha
wala utamaduni wa lugha lengwa.
ü Tafsiri
ya Kisemantiki
Mbinu
hii ya tafsiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa
kufuata sarufi ya lugha lengwa. Tafsiri ya kisemantiki huwekea mkazo
kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi.
ü Tafsiri
ya Kimawasiliano
Tafsiri
hii inazingatia na kumlenga msomaji wa matini lengwa ambaye hatarajii kupata
ugumu wowote katika matini anayosoma, anatarajia kupata tafsiri nyepesi ya
dhana za kigeni katika utamaduni wa lugha yake.
3. Masuala ya kiutendaji katika
tafsiri
Dhima za lugha na aina za
matini
Aina
za matini za tafsiri
i. Matini elezi (Expressive
Texts);
Ni
aina ya matini ambayo hujiegemeza zaidi kwa mwandishi, mwandishi anatumia lugha
kuelezea hisia zake bila kujali ujumbe huo utapokelewa vipi na wasomaji. Mfano
wa matini elezi ni kama: ushairi, hadithi fupi, tamthiliya, riwaya,
hotuba,nyaraka za kisheria, wasifu nafsi, insha nk.
ii. Matini arifu (informative
Texts);
Hizi
ni matini zinazohusu mada yoyote ile ya maarifa kama sayansi, teknolojia,
biashara na uchumi. Matini hizi huwa zinaandikwa katika maumbo sanifu, mfano
vitabu, ripoti za kiufundi, tasnifu au Makala katika magazeti ama majarida ya
kitaaluma n.k
iii. Matini amili (Persuasive
Texts);
Ni
aina ya matini ambayo imeegemea zaidi upande wa wasomaji. Matini amili
zinalenga kuibua hisia za msomaji na kumfanya afikiri au atende kwa maana
ambavyo imekusudiwa na matini mahususi. Mfano wa matini hizi ni matangazo,
maombi mathalani ya kazi au kitu kingine, maelekezo, propaganda na mialiko.
iv.
Matini za kifasihi
Ni
matini zinazohusu maandiko ya kifasihi kama hadithi fupi, riwaya, ushairi na
tamthiliya
v.
Matini za kiasasi
Ni
matini zinazohusu siasa, biashara, fedha, sheria, serikali na asasi nyinginezo.
vi.
Matini za kisayansi.
Ni
matini zinazojumuisha Nyanja zote za sayansi na teknolojia. Mfano maelekezo ya
matumizi ya vifaa mbalimbali vya kielektroniki.
vii.
Matini za kiufundi
Hizi
ni matini zinazotumia kiwango kikubwa cha msamiati wa kitaalamu au istilahi.
Mfano matini za utabibu, za kisheria na kisayansi.
viii.
Matini zisizo za kiufundi
Hizi
ni matini zinazotumia msamiati wa kawaida, mfano hotuba za viongozi mbalimbali,
kadi za mialiko n.k
Uchambuzi
wa matini ya tafsiri
Kabla
ya kutafsiri ni muhimu Kusoma matini nzima ili kubaini
v Lengo
la matini
v Lengo
la mfasiri
v Wasomaji
lengwa
v Umbo
la matini lengwa
v Mtindo
wa matini chanzi
v Ubora
na mamlaka ya matini chanzi
Mchakato wa kufasiri
Hatua
muhimu
(I) Maandalizi
(II) Uchambuzi
(III) Uhawilishaji
(IV) Usawidi
wa rasimu ya kwanza ya tafsiri
(V) Udurusu
wa rasimu ya kwanza ya tafsiri
(VI) Kusomwa
kwa rasimu ya tafsiri na mtu wa pili
(VII) Usawidi
wa rasimu ya mwisho ya tafsiri
i. Maandalizi
ya kutafsiri
Katika hatua hii, mfasiri
anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake, mtindo wa
matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri, anashauriwa
kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo
muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni
yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika
kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata
ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri
au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.
ii. Uchambuzi
wa matini chanzi
Katika hatua hii, mfasiri
anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, nahau, misemo pamoja na
maelezo mengine ya matini chanzi aliyoyaandika au kuyapigia mstari katika hatua
ya maandalizi na kuyatafutia visawe vyake katika lugha lengwa, hapa mfasiri
anashauriwa kutumia marejeo mbalimbali kama vile, kamusi, ensiklopedia, orodha
ya msamiati na istilahi mpya. Mfasiri anatakiwa kuwa na shajara au daftari dogo
kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu ya matini chanzi na
visawe vyake, visawe vinavyoonekana kufaa viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi
kuvirejelea wakati wa kutafsiri, vilevile mfasiri kama ataona kuwa matini
chanzi ni ndefu sana, anashauriwa kuigawa matini hiyo katika sehemu ndogondogo
kama vile, sura, aya au sentensi na kuanza kushughulikia sehemu moja baada ya
nyingine.
iii. Uhawilishaji
Uhawilishaji ni uhamishaji wa
mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, au uhamishaji wa mawazo au
ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya tafsiri. Hii ina maana kuwa katika
hatua hii, visawe vya kisemantiki [kimaana] vya matini chanzi vilivyobainishwa
katika hatua ya uchambuzi huamishwa katika matini lengwa [kutoka lugha chanzi
kwenda lugha lengwa] na kupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo
iwe na maana kwa wasomaji wake.
iv. Kusawidi
/Kuandaa rasimu ya kwanza ya tafsiri.
Katika hatua hii, mfasiri
huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini aliyoikusudia,
katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua
kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika hatua ya uchambuzi,
na hivyo kulazimika kuchunguza zaidi matini chanzi na hata kupekua zaidi na
zaidi marejeo yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri. Jambo la
kuzingatia, mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe azingatie umbo
na lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake.
v. Kudurusu
/ kuipitia rasimu ya kwanza
Baada ya kusawidi rasimu ya
kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri kati ya juma moja
hadi mawili baada ya kukamilika kwake na kuanza kuidurusu/ kuipitia rasimu hiyo
kwa jicho la kihakiki zaidi na kuangalia kama kuna makosa ambayo yamejitokeza
katika rasimu yake au la na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi.
vi. Kusomwa
kwa rasimu ya tafsiri na mtu/watu wengine
Baada ya mfasiri kuipitia
rasimu yake ya kwanza, na kuifanyia masahihisho kwa makosa yaliyojitokeza,
anatakiwa kuwapa watu wengine waidurusu rasimu hiyo iliyofanyiwa marekebisho
ili waipitie tena na kuirekebisha, hivyo basi wasomaji hao wanaweza
wakahakiki,wakashauri, n.k. Wasomaji hawa husaidia kuona kama tafsiri iko
sahihi, inaeleweka na ina mtiririko mzuri wenye mantiki.
vii. Usawidi
/Kuandika rasimu ya mwisho
Baada ya kupata maoni kutoka
kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia maoni, mapendekezo na maelekezo
yao kusahihisha tena tafsiri yake na hatimaye kuandaa na kutoa rasimu ya mwisho
ambayo itakuwa tayari kwa kusomwa na
wasomaji.
Baada ya kuangalia maana ya tafsiri, sasa tuangalie sifa anazotakiwa kuwa nazo mfasiri:
Sifa za mfasiri bora
Mfasiri bora anatakiwa kuwa na
sifa zifuatazo:
· Awe na ujuzi wa lugha fasaha, hii ina maana kuwa awe anajua kwa
ufasaha lugha zote mbili, yaani lugha chanzi na lugha lengwa. Hii ni kujua
vizuri nyanja mbalimbali za Isimu ya lugha husika kama vile;
Fonolojia-{Matamshi}, Mofolojia-{Maumbo}, Sintaksia-{Muundo} na
Semantiki-{Maana}
· Awe
na ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini chanzi na
uwezo au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha katika lugha lengwa.
· Awe
amesoma maandishi ya matini chanzi hadi ayafahamu kinaga ubaga
halafu aweze kuyafikiria katika lugha lengwa.
· Aweze
kutambua tamaduni za lugha chanzi na lugha lengwa.
· Aweze
kuibua hisia sawa kwa walengwa kama ilivyo katika matini chasili
· Awe
na stadi za uhakiki matini.
· Awe
na tajiriba kubwa ya usomaji wa aina mbalimbali za tafsiri.
· Awe
na tabia yakushirikiana na watu wengine katika shughuli za kufasiri.
4. Matatizo yanayojitokeza
katika tafsiri
Ø Matatizo
ya kitamaduni
Mfasiri
daima hulenga kuhawilisha maana kwa mujibu wa utamaduni wa jamii husika hivyo
lugha zenye utofauti sana kiutamaduni huwa tatizo kwa mfasiri.
Ø Matatizo
ya kiisimu
Tatizo
hili hujitokeza iwapo mfasiri anafasiri lugha mbili zinazotengana sana kiisimu.
Ø Matatizo
ya kimtindo
Yampasa
mfasiri kuuelewa upekee wa mwandishi,wakati mwingine mfasiri anapojitahidi sana
kuhifadhi mtindo wa mwandishi huishia kutoa tafsiri tenge.
Ø Uundaji
wa maneno mapya
Hali
hii hutokea iwapo mfasiri anapokosa kabisa visawe vya istilahi za lugha chanzi
katika lugha lengwa.
Ø Matatizo
ya kiitikadi
(i)..Tofauti za kiisimu kati
ya lugha chanzi na lugha lengwa. Tofautui za maumbo, miundo na maana kati ya
lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza wakati mwingine husababisha matatizo
au upungufu katika tafsiri na ukalimani. Kwa mfano maumbo ya vitenzi vya
Kiingereza huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonesha umoja au wingi wa wahusika
wala majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo yanayotolewa tofauti
maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ambavyo huonesha umoja na wingi wa wahusika na
hata kuwa na majina ya vitu husika, tazama mifano ifuatayo kama ilivyotolewa
na, Mwansoko [2006]
Kingereza__
Kiswahili
No
parking? Usiegeshe gari hapa [je kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?]
No
Smoking? Usivute sigara[ Je ni sigara tu ndiyo hairuhusiwi kuvutwa?]
Arrivals?
Wanaowasili
Departures?
Wanaosafiri
Vilevile tofauti za maana kati
ya lugha ya Kingereza na Kiswahili huweza kuathiri tafsiri au ukalimani,
mathalani:
Kiswahili__
Kingereza
Wasiojiweza?
Disabled [Siyo wote wasiojiweza ni walemavu]
[na
siyo walemavu wote hawajiwezi]
Wezi
wa mifukoni? Pickpockets [Hawaibi kwenye mifuko, wanaiba kutoka
Mifukoni]
(ii) Tofauti za mitindo
kati lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti
za mitindo ya uzungumzaji pia, huweza kuathiri tafsiri na ukalimani na hii ni
kwa sababu unaweza kukuta kuna mitindo fulani inaweza kutumika katika muktadha
fulani lakini ikishindwa kupata tafsiri katika lugha nyinginekatika muktadha
ule ule mathalani:
Kingereza:
Kiswahili
(i)
Thou shalt not steal [mtindo wa kidini] Usiibe. Do not steal [mtindo wa
kawaida] Usiibe
(ii)
Lend me your ears [mtindo wa kishairi] Naomba mnisikilize May I have
your attention [kawaida] Naomba mnisikilize
Tafsiri zote tulizoziangalia
katika mfano wa (i) na (ii) zimetoa maana au taarifa ili ile iliyomo katika
matini chanzi lakini tafsiri hizo hazikuzingatia mtindo wa lugha iliyotumika
katika matini chanzi.
(iii) Tofauti za
kitamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti
za kiutamaduni, yaani taofauti za kimila, desturi na mazingira ya watumiaji wa
lugha chanzi na lugha lengwa huweza kufanya tafsiri au ukalimani kuwa mgumu,
kwa mfano, katika utamaduni wa Waingereza wana milo minne wakati Waswahili wana
milo mitatu na hii hupelekea kuwa
vigumu
kupata dhana za milo ya hiyo ya Waingereza katika dhana ya Kiswahili. Mfano:
Waingereza
wana: Waswahili wana:
Breakfast
------------------ Kifungua kinywa
Lunch
…………………... Chakula cha mchana
High
tea ……………………?
Dinner
……………………Chakula cha jioni
Supper
…………………….?
Kwa hiyo ukiangalia mifano
hiyo, utaona kuwa, high tea na supper kuzipata dhana zake katika lugha ya
Kiswahili ni ngumu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kuwa na milo kama hiyo
kwa siku. Lakini pia inakuwa vigumu kupata tafsiri ya vyakula kama vile ugali,
makande katika lugha ya Kiingereza kutokana na kutokuwa na vyakula vya aina
hiyo.
(iv) Tofauti za
kiitikadi kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti
za kiitikadi pia huweza kuathiri tafsiri na ukalimani, na hii ni kwasababu,
utakuta wafasiri wengi hususani waandishi wa habari kuegemea katika itikadi
zaidi, kwa mfano:
Kingereza
Kiswahili
Bussnessman
? mlanguzi [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi ya ujamaa]
mfanyabiashara [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi ya ubepari]
Freedom
fighter ? wapigania uhuru [Tafsiri ya vyombo vya habari vya Tanzania wakati wa
kupigania uhuru] Magaidi [Tafsiri ya idhaa ya BBC na Radio za Afrika
Kusini
wakati huo]
Hivyo
basi
5. Aina za tafsiri.
Tafsiri
ya fasihi
§ Tafsiri
ya riwaya
§ Tafsiri
ya tamthiliya
§ Tafsiri
ya ushairi
§ Tofauti
ya tafsiri za kifasihi na zisizo za kifasihi.
© Tafsiri
ya matini za kisayansi/ kiufundi
Matini
za kisayansi au za kiufundi ni zile matini zinazotumia msamiati maalum, mfano
matini za tiba, uhandisi, elektroniki, sayansi ya kompyuta na sayansi
nyinginezo. Tafsiri ya matini hizi haijiegemezi katika utamaduni wowote na
hutofautiana na tafsiri nyingine kutokana na matumizi makubwa ya istilahi.
Matini za kiufundi pia hutumia picha, grafu, michoro, vielelezo, takwimu n.k na
huandikwa katika umbo la ripoti ya kiufundi. Mfasiri anapofasiri matini hizi hukumbana
na zoezi la uundaji wa istilahi mpyakutokana na kukosa visawe vya istilahi za
lugha chanzi katika lugha lengwa.
© Tafsiri
na Utamaduni
Lugha
ni kipengele cha utamaduni wa jamii, pia lugha inatumika kuelezea utamaduni wa
jamii husika. Maana za maneno katika lugha hujengwa kutokana na utamaduni wa
jamii inamozungumzwa lugha hiyo. Hivyo tafsiri siyo tu mchakato wa kiisimu,
bali pia ni mchakato unaojumuisha masuala yanayohusu utamaduni wa wazungumzaji
wa lugha husika. Tofauti za kiutamaduni baina ya lugha chanzi na lugha lengwa
ndizo zinampatia mfasiri matatizo makubwa
wakati
wa kufasiri, mathalani mfasiri anapofasiri lugha ya Kiingereza na lugha ya
Kiswahili. Vipengele vya kiutamaduni vinavyoweza kuleta ugumu katika kufasiri
ni kama nguo, vinywaji, violwa, ekolojia, siasa na dini.
© Tafsiri
ya mashine na tafsiri ya binadamu
Mchakato
wa kufasiri huweza kufanywa na binadamu au mashine. Mchakato wa kufasiri kwa
kutumia mashine umekuja kutokana na maendeleo ya sayansi na tekonolojia ambapo
badala ya binadamu kutumia maarifa yake zipo mashine ambazo zinaweza kufanya
kazi hiyo.
6.Tafsiri na ukalimani
Tafsiri
ni uhawilishaji wa mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja hadi
nyingine. Ukalimani ni uhawilishaji wa ujumbe au mawazo ulioko
katika mazungumzo kutoka lugha moja hadi nyingine. Hizi ni taaluma zenye
uhusiano kwani zote zinahusika na kuhawilisha ujumbe au mawazo kutoka lugha
moja hadi nyingine.
Katika
ukalimani matini chanzi huwa katika mazungumzo na matini lengwa pia huwa katika
mazungumzo. Katika ukalimani mkalimani hana muda wa kutosha wa kujiandaa kwa
sababu anatakiwa kukalimani kile anachosikia wakati ambapo mzungumzaji
anaendelea kuzungumza mambo mengine.
Aina za ukalimani
Kuna
aina mbalimbali za ukalimani kutegemeana na vigezo unavyotumia kuainisha au
kupata hizo aina;
1. Kigezo cha kwanza ni kigezo
cha Muktadha; Katika kigezo hiki vipengele vinavyojitokeza ndani ya
muktadha ili kupata aina tunazingatia mahali, lengo, aina ya hadhi, sifa za
walengwa nk.
© Ukalimani
wa Kijamii/community interpretation:
Huu
ni ukalimani ambao hufanywa katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile
afya, ujenzi wa shule huduma za kijamii kama vile maji, umeme, masuala ya
mihadhara ya kidini nk.
© Ukalimani
wa Mikutano au Makongamano/Conference;
Huu
ni ukalimani unaofanyika katika makongamano au mikutano
mbalimbali.
Mara nyingi aina hii ya ukalimani inafanyika katika mikutano ya kimataifa.
© Ukalimani
wa Mahakama/Mahakamani;
Aina
hii hufanywa na wanasheria katika mahakama za ngazi mbalimbali. Pia huitwa
ukalimani wa kisheria.
© Ukalimani
wa Kitabibu; Huu ni ukalimani ambao unafanyika mahali ambapo matibabu
yanapatikana, kwa kiasi kikubwa aina hii ya ukalimani inafanyika katika
hospitali kubwa kubwa.
© Ukalimani
wa Habari/katika vyombo vya habari; Huu ni ukalimani unaofanywa katika
vyombo mbalimbali vya habari, hususani redio na televisheni ili kuiwezesha
hadhira lengwa iweze nayo kuelewa matangazo yanayotolewa kwa lugha chanzi.
© Ukalimani Sindikizi/Escort
interpretation; Katika aina hii ya ukalimani mkalimani hufuatana na mtu au
kikundi cha watu katika safari au katika usaili au mahojiano.
2. Kigezo cha pili ni
kigezo cha Muundo au Mfumo wa Lugha/Language mode/modality; Katika
kigezo hiki lugha inayotumika katika ukalimani inaweza ikawa lugha ya
kusema/kizungumza na lugha ya alama. Kupitia lugha ya alama tunapata aina moja
ya ukalimani yaani ukalimani wa viziwi
Kwa
kupitia lugha ya mazungumzo au kusema tunapata aina mbili za ukalimani ambazo
ni;
Ukalimani Mfululizo/Andamizi/Simultaneous
interpretation; Katika ukalimani mfululizo, kama jina lenyewe linavyodokeza
mkalimani huzungumza takribani sambamba na mzungumzaji wa lugha chanzi. Katika
aina hii ya ukalimani mkalimani lazima afanyekazi kwa haraka
sana
ili kuendana na kasi ya mzungumzaji kuepuka kupitwa na mambo muhimu.
Katika
ukalimani mfululizo makalimani huketi katika chumba maalum cha ukalimani
(booth) ambacho hakipitishi sauti (sound proof) na kisha huzungumza kwa kutumia
kipaza sauti huku akimwona na kumsikia mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia
visikizio (ear phones)
Ukalimani Fuatishi/Mtawalia (Consecutive
interpretation); Katika ukalimani fuatishi mkalimani huzungumza/hukalimani
baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza ujumbe wake au hata kama
hajamaliza ujumbe wake baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kutulia kwa sekunde
kadhaa ili kumpa makalimani fursa ya kukalimani kile kilichosemwa. Katika aina
hii mkalimani na
mzungumzaji
wa lugha chanzi mara nyingi wanakuwa pamoja wakiwa wamesimama kwenye jukwaa au
wakiwa wameketi mezani.
Sifa za Mkalimani
a) Awe
na ujuzi wa hali ya juu wa lugha anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake.
b) Ajue
lugha zaidi ya mbili za kimataifa kwani kadiri unavyojua lugha zaidi ndivyo
unavyokuwa mkalimani bora zaidi.
c) Awe
na ujuzi au maarifa ya kutosha juu ya mada, taaluma au uwanja unaozungumziwa.
Inamaana kwamba kama wewe ni mkalimani wa masuala ya kiuchumi basi hupaswi
kufasili masuala ya kisheria. Mfano; ukalimani wa mahakamani hufanywa na
wanasheria.
d) Awe
na ujuzi wa taaluma ya ukalimani; yaani awe amepata mafunzo ya ukalimani.
Katika hayo mafunzo atajifunza mbinu za ukalimani aina, changamoto na namna ya
kuzikabili.
e) Awe
na kipaji, yaani; Uwezo wa kukumbuka, Kuteua msamiati sahihi kwa haraka, Kipaji
katika kuunda istilahi haraka haraka na kuitumia. Kipaji cha ulumbi/awe na
ulumbi yaani kipaji cha kuongea na kuvuta watu. (eloquency)
Mfano
wa Tafsiri
Kiingereza Kiswahili
vision > ono
six > sita (thenashara)
around me > kunizingira
suffused > jaa
clear light > mwanga safia
fine mid-summer morning > asubuhi nadhifu ya kiangazi
dim light > mwanga hafifu
wet dawn > mapambazuko nyevunyevu
May > mwezi wa Mei
warning > onyo? ishara awali?
gold lettering > herufi zilizonakishiwa dhahabu
glow > angaza? nawiri?
Uwakilishi huu unamulika ugumu wa kupata visawe. Unapokosa visawe, unatafsiri kwa
kufasiri au kufafanua maana. Mbinu hizi zimetumika kwa matini za ‘without warning’ >
bila ishara awali, na, ‘gold lettering’ > herufi zilizonakishiwa dhahabu, mtawalia.
Kulingana na matumizi ya lugha unayokabili, ni muhimu kuzingatia masharti yafuatayo:
Majina maalumu hayatafsiriwi, isipokuwa pale pana tafsiri au neno-mkopo tayari.
Zingatia neno Biblia.
Majina ya mashirika au nyadhifa huwakilishwa kwa tafsiri sisisi, kama vileRedcross>Msalabamwekundu au Chairperson > Mwenyekiti.
Semi za lugha hutafutiwa visawe katika katika lugha pokezi. Zingatia: ‘One rotten
apple spoils the whole barre.’l >Nazi mbovu harabu ya nzima. Kisawe kikikosa,
unawakilisha ujumbe kwa usemi linganifu au tafsili ya maana.
Mara kwa mara, unaruhusiwa kukopa sisisi hasa
ukijikuta umekwama kabisa na maendelezo ya neno yawe hayakaidi kanuni za mfumo wa sauti wa lugha pokezi.
Maneno mora, data, ajenda ni mifano mizuri ya mikopo sisisi.
Mifano ya matini zilizotafsiriwa
Matini
ya habari
Matini Chasili: Kiingereza
The Secretary General of the United Nations Organization, Kofi Annan, fired one top
official blaming him for failing to ensure the security of the officers of the organization.
Mr. Annan also chastised a highly respected deputy, Ms. Louise Frechette of Canada,
who submitted her resignation but Mr. Annan refused to accept it. The action yesterday
appeared to be unprecedented in the United Nations Organization, where senior officers
are almost never rebuked publicly for such an offence.
Matini Tafsiri: Kiswahili
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alimwachisha kazi kinara wake wa
usalama akimlaumu kwa kushindwa kuhakikisha usalama wa maafisa wa umoja huo.
Annan pia alimshutumu vikali naibu wake, Bi. Louise Frechette wa Canda, lakini alikataa
ombi lake la kujiuzulu. Hii ni mara ya kwanza kinara wa umoja huo kuzomea waziwazi
maafisa wake kwa kufuatia kosa kama hilo.
Tafsiri hii imehamisha ujumbe muhimu lakini ikashindwa kuhifadhi maana kamilifu.
Baadhi ya maana huonekana kupotea na zingine kupotoshwa. Tunabaini upungufu huu kwa kulinganisha baadhi ya kauli za matini hizi:
Kiingereza Kiswahili
one top official kinara wake wa usalama
a highly respected deputy naibu wake
submitted resignation?
appeared unprecedented ndio mara ya kwanza kinara . . .
publicly waziwazi























Kwanza kabisa, maana katika ‘submitted resignation’, haionekani kushughulikiwa. Arifa
katika kauli hii imetolewa kwa maana ya kushadidia uzito wa kitendo cha Katibu Mkuu
wa Muungano wa Mataifa. Pili, maana za kauli zingine zimepotoshwa ifuatavyo:
Kauli ya ‘One top official’ haina maana ya kinara wa usalama. Fasiri hii
imekiuka mipaka ya maana matini na kupotosha
ujumbe. Maana ya ‘highly respected’ haikushughulikiwa. Tena, matumizi ya kibainishi,
{a}, ina maana ya kuwa kuna manaibu wengine, na si yule mmoja pekee.
Kauli ya ‘appeared unprecedented’ Ina maana ya kuwezekana kuwa mwanzo, na
sio kuwa kwa uhakika unaosikika katika kauli “hii ndio’’.
Neno publicly halina maana ya “waziwazi” ila hadharani. Tendo linaweza kuwa
waziwazi lakini pia faraghani.
Matini ya riwaya
Matini Chasili: Kiingereza
The car sped smoothly along the coast road. Its own smooth running mixed with the soft
Sounds of the sea flowing over the sands. The man closed his eyes, and like a piece of
twine, the thought run round and round his head that it would never be possible to look at
such comfortable things and feel real contempt for them. Envy, certainly, but not contempt.
Matini Tafsiri: Kiswahili
Gari ilishika kasi ilipofika ile barabara iliyoko karibu na pwani. Ile sauti tulivu ya mngurumo wa
hiyo gari ilichanganyika na sauti ya bahari inayofurikia michangani. Yule bwana alifunga macho na
humo ubongoni mwake akawa anazungukwa na fikira kwamba haitawezekana kabisa kuviangalia
vitu vizuri namna ile kisha ukavidharau. Kuingiwa na husuda au kijicho ndio; lakini si dharau.
Matini chasili inatafakari vile tajiriba zetu za maisha ya anasa na starehe huja kuathiri
mielekeo yetu. Ujumbe huu umehifadhiwa katika matini tafsiri, licha ya hitilafu wazi za
baadhi ya maana. Hitilafu hizo zajitokeza kulingana na tafsiri za kauli kama:
Kiingereza Kiswahili
sped smoothly ilishika kasi
coast road barabara iliyokaribu na pwani
smooth running sauti tulivu
comfortable things vitu vizuri
env like
a piece of twine ? husuda au kijicho
Hitilafu hizi huashiria upotovu au upungufu wa maana unaoweza kufafanuliwa ifuatavyo:
Kauli ya ‘speed smoothly’ yaashiria mwendo wa utulivu. Kuna shaka kamakushika kasi kuna maana ya utulivu. Mara nyingi huwa ni kinyume chake.
Kauli ya ‘smooth running’ hairejei mngurumo wa gari pekee. Tafsiri ya sauti
tulivu, kwa hivyo, imebana maaana ya Kiingereza.
‘Coast road’ si lazima iwe ni ile barabara iliyo karibu na pwani. Inaweza kuwa
ni barabara ya kuelekea pwani: barabara ya pwani.
Matini ya Kishairi
Shairi ni tungo linalotiririsha taswira, mawazo na ujumbe kwa lugha nzito ya mkato,
yenye mnato wa maana. Umbo la shairi hurejelea idadi ya beti zake. Hata hivyo, kila
ubeti unafaa kuwasilisha ujumbe kamilifu unaowiana na maana ya shairi nzima. Ubeti
mfupi ufuatao kutoka, Wimbo wa Lawino, ni mfano wa tafsiri ya shairi. Umenukuliwa
kutoka Mwansoko (1996).
Matini Chasili: Kiingereza Matini Tafsiri: Kiswahili
“Maria the clean woman “Maria Mtakatifu
Mother of the Hunchback Mama wa Mungu
Pray for us Utuombee
Who spoil things Sisi wakosefu
Full of Graciya.” Uliyejaa neema.”
Matini chasili ni kinaya na imetumia lugha ya mzaha kimakusudi. Mtunzi wa ubeti huu analenga kukejeli imani na mafunzo ya Kikatoliki. Matini tafsiri imepuuza dhamira hii naadala yake ikatumia lugha ya kawaida ya heshima na uungwana. Kwa kufanya hivi, tafsiri imeikaidi dhamira na mwelekeo wa mwandishi wa matini chasili.
Mifano ya tafsiri ya kimawasiliano:
Tanzania National Electric
Supply Company Limited. >
Shirika la umemeTanzania.
A bird in the hand is worth two
in the
bush. >
Fimbo ya mbali haiui nyoka.
A burnt child dreads
fire. >
Mtoto akililia wembe, mpe.
Actions speak louder than
words >Ada
ya mja hunena, mwungwana ni kitendo.
A drowning man will catch at a
straw. >Mfa
maji haachi kutapatapa.
All good things come to those
who
wait. >
Subira huvuta heri.
A stitch in time saves
nine. >Usipoziba
ufa utajenga ukuta.
As you sow, so you shall
reap >Upandavyo
ndivyo uvunavyo
Charity begins at
home >Kutoa
ni moyo si utajiri.
Clothes don’t make the
man. >
Usichague mchumba siku ya Idi.
Mtoto wa nyoka ni
nyoka. >Like
father like son
Kwa
hiyo mfasiri yeyote yule ni muhimu kuteua mbinu atakayotumia wakati wa
kutafsiri kulingana aina ya matini anayotaka kutafsiri. Hata hivyo ni vigumu
kutumia mbinu moja pekee katika kutafsiri, kwani mbinu zote huweza kujitokeze
katika tafsiri kwa mfano, maneno mengine huweza kufasiriwa kisisi au
kisemantiki lakini pia ni lazima iwepo mbini ambayo inatawala mbinu zote.
Wataalam wengi wa tafsiri wanapendekeza mbinu ya tafsiri ya kimawasiliano
itumike zaidi hususani katika matini zenye lengo la kuelimisha au kuleta athari
sawa na ile ile iliyopo katika matini chanzi. Matini kama vile za kisheria
mbinu muafaka zaidi ni ile ya kisemantiki.
Zoezi
1. Linganisha na linganua kati ya taaluma ya tafsiri na ukalimani.
2. (a) Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiingereza
(i) Dua la kuku halimpati mwewe
(ii) Bandu bandu humaliza gogo
(iii) La kuvunda halina ubani
(iv) Mla vya watu naye vyake huliwa
(v) Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
(b) Ni njia gani umetumia katika tafsiri ulizotoa hapo juu,
unadhani ni kwa nini?
3.Kwa kutumia mifano, fafanua istilahi zifuatazo:
[a] [i] Matini chanzi
[ii] Matini lengwa
[iii] Lugha chanzi
[iv] Lugha lengwa
[b] Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiswahili
(i) All that glister is not gold
(ii) Looser casn't be a chooser
(iii) When you make your bed you must lie on it
(iv) There is no incense for something rotting
(v) When in Rome do, do as Romans do
(vi) Do not pray for an easy life,pray for the strength to endure
a difficult one.
(vii) Study without desire spoils the memory, and it retains
nothing that it takes it.
(c) Ni njia gani umetumia katika tafsiri hizo ulizotoa hapo juu,
unadhani ni kwanini?
4. "Mfasiri au mkalimani hukabiliana na changamoto mbalimbali
katika kufanikisha kazi yake." Huku ukitumia mifano thibitisha kauli hiyo



























0 comments :
Post a Comment