Kamati Kuu ya Chadema imepanga Agosti 4 kuwa siku ya kumpata mgombea wake wa urais ambaye ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vyama vinne vilivyounda Ukawa, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais, lakini kila chama kitateua mgombea wake kabla ya kukubaliana mtu atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Ratiba iliyotolewa jana na Chadema inaonyesha kuwa chama hicho kitatumia siku 76, kuanzia Mei 18, kumaliza mchakato wa kuwapata wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa kuhitimisha na Mkutano Mkuu. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Chadema itampata mgombea wake wa urais takriban siku 14 zaidi kulinganisha na mwaka 2010 wakati Dk Willibrod Slaa alipoteuliwa.
Kwa mujibu wa Ibara ya 7.710 (C) ya katiba ya Chadema, Mkutano Mkuu ndiyo chombo chenye mamlaka ya kumpitisha mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia wanahabari jana kuwa kamati hiyo imeridhia mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu uanze ili watia nia katika maeneo mbalimbali waanze kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge.
Katika ratiba hiyo , chama hicho kimeyapa kipaumbele maeneo yanayoonekana kutokuwa na madiwani na wabunge, kuanza kuchukua fomu siku ya kwanza ya kazi hiyo na kuzirudisha Juni 25.
Aidha ratiba hiyo inaonyesha kuwa makada waliopo kwenye maeneo yenye madiwani watachukua na kurejesha fomu ndani ya siku 10 kuanzia Julai Mosi.
0 comments :
Post a Comment