
Na Khelef
Nassor
Zanzibar: Mgombea urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema endapo
wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kuwaongoza, atalishughulikia suala zima
la muungano ikiwa ni pamoja na kuipatia Zanzibar mamlaka yake kamili.
Maalim Seif ameyasema hayo wakati
alipokuwa akiwautubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni
za chama hicho katika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti mjini Unguja ambapo
viongozi mbali mbali wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi Ukawa
akiwemo Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa na
Mgombea mwenza wake Juma Duni Haji waliudhuria katika uzinduzi huo.
Aidha Maalim Seif aliwalaumu viongozi
wa CCM kwa kudai wamekwenda kuiyuza Zanzibar kwenye Bunge maalum la katiba kwa
kuruhusu kupitisha vipengele kandamizi vinavyoinyima Zanzibar mamlaka yake na
hivyo ameahidi kushirikiana na Edward Lowassa kulishughulikia suala hilo wakati
watakapoingia madarakani.
“Hatuwezi kukubali kabisa kabisa.
Tutairejesha rasimu ya Jaji Warioba, na kuomba Bunge la katiba lifanye kazi
chini ya muongozo wa rais Lowassa na rais Seif Sharif Hamad” Alisema Maalim
Seif .
Hata hivyo Maalim Seif aliwaahidi
wananchi wa Zanzibar kuwa katika uongozi wake atazingatia misingi ya demokrasia
na utawala bora ili wananchi wake waweze kuishi katika nchi yao kwa amani na
utulivu.
“Nataka nikiwa rais wenu nianzishe
misingi ya utawala bora ili nyinyi wananchi muishi katika nchi yenu bila ya
woga, bila ya hofu na mwende kifua mbele kwa kujifakharisha na nchi yenu.
Siwezi kukubali kumuona Mzanzibari yoyote anadhalilishwa” Aliongeza Maalim
Seif.
Pia aliongeza kwa kusema atahakikisha
mashekhe wa Kizanzibari waliopelekwa katika mahakama za Tanzania bara
wanarudishwa mara moja katika mahakama ya Zanzibar ili waweze kuhukumiwa
Zanzibar.
“Nashangaa tunaambiwa nchi hii ina
rais, nchi hii ina Baraza la Wawakilishi na pia ina mahakama. Mahakama kuu ya
Zanzibar ina uwezo sawa na mahakama kuu ya Tanzania bara. Leo viongozi wajuu
wenye mamlaka katika nchi hii bila ya kutushauri sisi wenzao katika Serikali
wameamua mashekhe wetu kuwapeleka bara. Mimi nasema nikiwa rais watarudi hapa
hapa Zanzibar na kama wana makosa watahukumiwa na mahakama za hapa Zanzibar”
Alifafanua.
Akizungumzia Uchumi wa Zanzibar,
Maalim Seif alisema wakati atakapokuwa madarakani ataujenga na kuimarisha
Uchumi wa Zanzibar ambapo alikumbusha kuwa ahadi yake ya kuifanya Zanzibar kuwa
Singapore ya Afrika ya Mashariki bado iko pale pale.
“Tutaibadilisha Zanzibar iwe Singapore
ya Afrika ya Mashariki.Tutaweza kuakikisha tunajenga Bandari ya kisasa sio kwa
maneno lakini kwa vitendo” Alifafanua.
Hata hivyo alisema atafungua benki ya
uwekezaji ya Wazanzibari ambayo itatoa mitaji na mikopo kwa wanachi wa Zanzibar
ili waweze kujiajiri wenyewe.
“Wale vijana watakaojishughulisha na
uvuvi au kilimo, hiari yao! Benki itakuwepo, itatoa mikopo tena mikopo nafuu,
masharti nafuu na kila mmoja ataweza kumudu na kujiendeleza maisha yake”
Aliongezea.
Pamoja na hayo mgombea huyo ambaye
alionekana kuzikonga nyoyo za wananchi waliohudhuria katika mkutano huo na
kushagiliwa kila wakati aliwaeleza wananchi hao kuwa atalisimamia kikamilifu
suala la mafuta na gesi kwa kuunda wizara mpya ya mafuta na gesi ambayo
itashughulikia suala zima la mafuta na gesi pamoja na kuandaa sera na sheria
zake zitakazosimamia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati
ya maridiano ya Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo amewataka wananchi wa
Zanzibar kumchagua Maalim Seif kwani ni kiongozi anayejali maslahi ya Zanzibar
na Wazanzibari.
Aidha Moyo amewataka wananchi hao
kutowachagua Wabunge na Wawakilishi wa CCM ambao kazi yao ni kuhubiri chuki na
ubaguzi kwani kufanya hivyo kutapelekea kuwagawa Wazanzibari ambao wako kitu
kimoja.
Naye Mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa amesema
Chama Cha Mapinduzi kimeshindwa kuendesha kampeni za kistaarabu kutokana na
kitendo chao cha kuyapachua na kuyachana mabango ya wagombea wa Ukawa jambo
ambalo amelitaja kuwa ni kinyume na taratibu.
Pamoja na hayo Lowassa aliongeza kuwa
CCM hawatoweza kuiba kura kwani wamejipanga vizuri kwa ajili ya kuzilinda kura
zao na hivyo amewataka wananchi wa Zanzibar kuwaunga mkono yeye na Maalim Seif
kwa kuwapigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka
huu.
Kwa upande wake Msaidizi Meneja Kampeni,
Mansour Yussuf Himid amelikosoa vikali jeshi la Polisi kwa kudai jeshi hilo
limekuwa likiwadhibu kwa kuwapiga na kuwalawiti wananchi badala ya kuwalinda.
Aidha amesema mfumo wa Muungano uliopo
sasa hauna maslahi kwa Zanzibar kwani umekiuka malengo yote ya Muungano ambayo
yamewekwa na muasisi wake ambaye ni Mzee Abeid Aman Karume.
“Mzee wetu Karume alipindua ili
tujitawale, tusimamie haki kwa Wazanzibari wote, lakini CCM wamekosa radhi na
muda wao wa kuondoka madarakani umefika” Alisema.
Alisema wanaitaji kiongozi atakayesimamia utu,umoja na
misingi ya muungano kwa Wazanzibari ambaye kwake yeye anamuona Maalim Seif Kama
mtu sahihi wa kushika nafasi hiyo kutokana na kujitolea kwake katika kutetea
maslahi ya wazanzibari.
Chama Cha Wananchi CUF hapo jana
kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi mkuu kwa upande wa Zanzibar ambapo
leo watakuwepo Kwenye uwanja wa Tibirinzi kisiwani Pemba kuendeleza kampeni
zao.
0 comments :
Post a Comment