TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetoa mwongozo ikisema kuwa matokeo ya udiwani, ubunge na urais yanayobandikwa kwenye vituo mbalimbali nchini ni ruksa kutangazwa na vyombo vya habari, lakini havina mamlaka ya kumtangaza mshindi wa nafasi yoyote.
Kamishna wa Nec, Prof. Amon Chaligha, alitoa mwongozo huo wakati akijibu maswali ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotaka kujua kama vyombo vyao vitaruhusiwa kutangaza matokeo ya urais kadiri yatakavyokuwa yakipokelewa kutoka kwenye vituo mbalimbali nchini.
Alisema awali, matokeo ya urais yalikuwa hayabandikwi wala mawakala kusomewa, lakini sasa imeamuliwa yasomwe, yabandikwe na kila mmoja kupewa nakala kwa lengo la kuongeza uwazi.
“Matokeo ya vituo yanaruhusiwa kujumlishwa na kutangazwa… waandishi wa habari wanaweza kutangaza matokeo ya vituo, lakini siyo kutangaza mshindi,” alisema Profesa Chaligha na kuongeza:
“Tunafanya hivi ili kuondoa hisia mbaya na kuziba mianya ya kuibwa kwa kura au kubadilishwa matokeo. Tume haina matokeo yake kama inavyosemwa, bali ni yale yatokanayo na kura zinazopigwa na wananchi,” alisema.
“Tangazeni matokeo, lakini msiandike huyu ni mshindi kwa sababu hiyo si kazi yetu,” alisema.
Kwa mujibu wa kifungu cha 80 cha sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 na kifungu cha 81 cha sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa, sura ya 292, Nec ndiyo yenye mamlaka kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais.
Wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo husika ndiyo wenye mamlaka kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi ya ubunge na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ndiyo wenye mamlaka ya kujumlisha na kutangaza matokeo ya udiwani.
JAJI LUBUVA ATOA NENO
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alivitaka vyombo vya habari kuzingatia maadili ya kazi yao kwa kuendelea kuandika ukweli bila kuegemea upande wowote.
“Tunaomba mtumie kalamu zenu kuelimisha wapigakura wajitokeze kushiriki uchaguzi mkuu,” alisema.
Kamishna wa Nec, Jaji mstaafu John Mkwawa, pia alifafanua juu ya wapigakura ambao walirekebisha taarifa zao, lakini hadi siku ya uchaguzi majina yakakosekana katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, akisema kuwa kitakachotumika kuwaruhusu kupiga kura ni hekima na burasa ya msimamizi wa kituo baada ya kujiridhisha na kitambulisho kitakachoonyeshwa na mpigakura.
Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema hadi kufikia Oktoba 15, vifaa vyote vya uchaguzi vitakuwa vimeshawasili katika majimbo yote nchini isipokuwa karatasi za kupigia kura ambazo alisema zitawasili baadaye.
Chanzo: NIPASHE

0 comments :

 
Top