TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749



 
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana alitumia Ibada ya Shukrani iliyofanyika katika Parokia ya Hananasifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kulitumikia Taifa kwa zaidi ya miaka 15 na kuwaomba Watanzania wamsamehe kwa matamshi aliyoyatoa akiwa kiongozi, huenda yaliwakwaza baadhi yao. Alisema anasikia fahari kumaliza uongozi wake kwa furaha na amani.
Moja ya kauli tata zilizowahi kutolewa na kiongozi huyo iliyozua sintofahamu ni ile ya Juni 29, 2013 katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma alipoviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kauli nyingine tata ni ile ya mwaka 2009 baada ya kuwaeleza wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na vikongwe hawana budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri mahakama kuwahukumu, watakuwa wanakosea.
“Katika ibada hii ya shukrani, nimemuomba Mungu anisamehe kwa matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila mimi kujua. Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu nisipomshukuru Mungu kwa uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu nikiwa naibu waziri hadi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema.
Source: Mwananchi

0 comments :

 
Top