Dar es Salaam. Marais wastaafu; Goodluck Jonathan wa Nigeria na Armando Guebuza wa Msumbuji wataongoza jopo la waangalizi wa kimataifa wanaotarajiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Miongoni mwa waangalizi 600 waliotangazwa kushiriki mchakato huo ni wawakilishi kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) pamoja na nchi za Uingereza na Finland, Muungano wa nchi za Maziwa Makuu, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola na Umoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC).
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Yahya Simba amesema leo jijini Dar kuwa marais hao wastaafu ni miongoni mwa watu mashuhuri watakaoongoza timu za waangalizi wa uchaguzi mkuu.
“Uchaguzi siyo siri na watu wengi wangependa kuja kujifunza namna tunavyosimamia mambo yetu. Hasa utekelezaji wa demokrasia za ndani. Tunatarajia kupokea wageni wengi ambao watatoka kwenye jumuiya mbalimbali za kimataifa. Rais (Mstaafu) Goodluck Jonathan anatarajia kuongoza wawakilishi kutoka Jumuiya ya Madola na (Armando Emilio) Guebuza atakuwa na wale wa SADC,” alisema Balozi Simba.
Alieleza kwamba wizara yake inaendelea na uratibu wa wageni wote waliomba ruhusu ya kuja kufanya hivyo nchini kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika utekelezaji wa uchaguzi huru na wa haki. Kuhusu mustakabali wa uchaguzi mkuu alisema msisitizo wa serikali ni amani kwa nchi na watu wote.
Source Mwananchi
Source Mwananchi
0 comments :
Post a Comment