LICHA ya onyo na tambo kwa mabalozi, Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekwepa kuwachukulia hatua, Balozi Dianna Malrose wa Uingereza na Lu Youqing wa China wanaodaiwa kukiuka taratibu za kidiplomasia.
Hatua hiyo inatokana na kauli ya Ikulu kukana taarifa za uchochezi unaodaiwa kufanywa na Balozi wa Uingereza nchini, zilizotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa naibu waziri, Steven Maselle.
Hii ni mara ya pili kwa serikali kuonesha udhaifu huo, ambapo pia Desemba mwaka jana, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilikiri kuwa Balozi wa China, alivunja mkataba unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia lakini ikashindwa kumchukulia hatua.
Balozi huyo alituhumiwa na Chadema kwa kukiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kutokana na hatua yake ya kushiriki kazi ya uenezi wa siasa za majukwaani za CCM katika ziara ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana mkoani Shinyanga.
Wakati balozi Youqing akiwa hajachukuliwa hatua yoyote, serikali hiyo hiyo iliyomtuhumu balozi wa Uingereza kuendesha vitendo vya uchochezi, imegeuza kauli yake ikisema taarifa hizo hazijawahi
kuwepo mezani kwa Rais wala ofisi yoyote ya Ikulu.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikaririwa na gazeti moja la kila siku (sio Tanzania Daima), akisema kwa mujibu wa sheria za kidiplomasia, balozi wa taifa la nje haruhusiwi kuingilia mambo ya ndani ya nchini aliyomo na kwamba zipo taratibu za kufuatwa inapotokea hali kama hiyo.
Serikali yabanwa
Kufuatia mkanganyiko huo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Bukoba, Dk. Azaveli Lwaitama alisema kuwa kauli ya Maselle inaongeza shaka zaidi kuwa vigogo wa serikali kweli huenda wamehusika kukwapua fedha katika akaunti ya escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania kama ilivyodaiwa hivi karibuni.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Dk. Lwaitama alisema kuwa majibu ya Maselle yalikuwa ni ya kuhamaki, tena yakionesha serikali ilikuwa haijajipanga, ndio maana majibu yaliyotolewa hayakuhusiana na kilichokuwa kinajadiliwa.
“Watu walikuwa wanaulizia kuhusu sakata la kukwapuliwa fedha katika akaunti ya escrow, yeye akaja kuhamisha watu kwenye mjadala kwa kuanza kumshambulia Balozi wa Uingereza nchini.
“Haya mambo hayahusiani, tena masuala ya Balozi wa Uingereza yalipaswa kuzungumzwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sio Naibu waziri,” alisema Lwaitama.
Alisema kitendo cha Maselle kumkemea Balozi wa Uingereza badala ya kauli hiyo kutolewa na Waziri wa Mambo ya Nje au Waziri Mkuu, ni cha serikali kujidhalilisha mbele za jumuiya ya kimataifa.
“Naibu Waziri hawezi kumwamuru Balozi kwenda kujieleleza kwenye wizara nyingine wakati hata Ikulu na wizara inayoshughulikia masuala ya kidiplomasia hazina taarifa, haijulikani wazi huyo naibu waziri alichukua wapi taarifa hizo au alikurupuka mwenyewe? Alihoji. Nanye mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema kuwa kama Ikulu imekana msimamo wa Maselle, basi Pinda anapaswa kujiuzulu na serikali isukwe upya.
“Hii inatokana na ukweli kwamba Maselle alipomaliza kusoma tuhuma nzito dhidi ya Balozi wa Uingereza, alifuatiwa na waziri Muhongo ambaye pamoja na maelezo mengine aliunga mkono maelezo ya mtangulizi wake na hivyo ulikuwa msimamo wa wizara ya Nishati.
Katika hali iliyoonesha msimamo wa Maselle ulikuwa wa serikali, baada ya Muhongo kuhitimisha Waziri Mkuu alimalizia na kuunga mkono maelezo yote yaliyotolewa na Wizara ya Nishati bila kukosoa,”alisema.
Kafulila alifafanua kuwa kama Ikulu imekana msimamo wa Maselle ambao ulikuwa na baraka za waziri wake na Waziri Mkuu, hivyo haoni sababu ya Pinda kubaki madarakani.
“Huo ndo msimamo wangu, natambua yote haya yametokea kutokana na nia ovu ya kuficha uovu wa serikali katika ufisadi wa sh. bilioni 200 za escrow,”alisema Kafulila ambaye aliibua kashfa hiyo bungeni. Aliongeza kuwa Uingereza ilisaidia Tanzania kurudisha chenji ya rada serikali haikusema inaingilia mambo ya ndani na kwamba serikali imezipangia matumizi ya vitabu, sasa iweje leo Uingereza ionekane inaingilia mambo ya ndani kwa kusema ni muhimu suala la ufisadi wa escrow uchunguzwe?
Kauli ya Sefue ilikuja baada ya Maselle kumtuhumu balozi wa Uingereza bungeni na kumtaka ajipime kujiona kama anafaa kuendelea kuiwakilisha nchini yake huku akimuagiza afike wizara ya mambo ya nje kujibu tuhuma hizo.
Maselle alitoa tuhuma hizo wakati akichangia majumuisho ya hotuba ya wizara ya Nishati na Madini akibu mashambulizi ya baadhi ya wabunge waliotaka ufafanuzi wa kashfa ya ufisadi katika akaunti ya escrow wa sh. bilioni 200 inayowakabili vigogo wa serikali. Naibu waziri huyo aliungwa mkono na waziri wake, Prof. Sospeter Muhongo ambaye naye alidai anao ushahidi wa kuonesha wabunge wa upinzani walivyohongwa na IPTL.
Chanzo Tanzania Daima

0 comments :
Post a Comment