TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


        

Aliyewahi kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi, Matheo Qares, amemshutumu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akisema kuwa kiongozi huyo amepwaya katika kila nafasi ya uongozi.

Qares pia amehoji uhalali wa Sitta kuendelea kukusanya maoni ya Katiba Mpya wakati kazi hiyo ilikwisha kufanywa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake katika Kijiji cha Nkwaa nje kidogo ya mji wa Babati juzi, alisema katu haungi mkono hatua ya Sitta kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge akidai kuwa amepungukiwa sifa za uongozi.
Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa anajishughulisha na kilimo na ufugaji, alisema kitendo cha Sitta kuburuza vikao vya Bunge la Katiba na kuendelea kukusanya maoni kutoka makundi mbalimbali, ni ishara tosha kwamba hafai kuwa kiongozi wa wananchi kwa sababu hafuati misingi, sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa na kiongozi.
“Ni nani alimpa Sitta kazi ya kukusanya maoni ya makundi anayodai maoni yao hayakuchukuliwa? Ameonyesha dharau kwa Tume ya Jaji Warioba iliyokusanya maoni ya wananchi, anataka kila kitu kiandikwe kwenye Katiba, malisho ya wafugaji yaandikwe, maeneo ya kunyweshea maji, masoko kweli yote yaandikwe?” alihoji na kuongeza:
“Vipi makundi mengine kama wachimbaji wa madini pale Mererani, wavuvi nao wakiendelea kupeleka mambo yao yaandikwe kwenye Katiba, nasema katika hili amevurunda na amepwaya hawezi kuwapatia wananchi Katiba wanayoitaka bali watapendekeza Katiba ya viongozi,” alisema.
Alisema kinachoendelea sasa katika Bunge Maalumu la Katiba ni vurugu ambako kila mjumbe wa Bunge hilo anafanya anachoona kinafaa kwa masilahi yake au ya chama chake na hata kuondoa dhana ya kupatikana Katiba ya wananchi.
Qares alipinga hatua ya Sitta kuendelea kung’ang’ania vikao vya Bunge kwa vile ana malengo yake binafsi ya siasa, huku akiamini wananchi watamwona kama shujaa wao jambo ambalo halitatokea.
“Analichukulia kwa mtizamo na kwa malengo binafsi ya siasa akidhani atakuwa hero (shujaa). Lakini ameonyesha kushindwa tangu mwanzo. Ningekubaliana naye kama haamini Rasimu ya Warioba angekataa tangu mwanzo wasingeanza kuijadili ili wananchi waamini hiki anachokisema sasa kwamba rasimu ina upungufu,” alisema.
Kuhusu madai ya baadhi ya wanasiasa kwamba mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ulivurugwa na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge la Katiba, Qares alisema Rais Kikwete hakufanya kosa ila alikuwa anatoa maelekezo kwa Tume juu ya Muungano.
“Rais hakufanya vizuri kuwaambia wajumbe wa tume wasiruhusu mawazo ya kuhoji Muungano, kwa nini wananchi wasihoji? Kitendo cha kuwakataza kiliamsha hisia za wananchi wakaanza kuhoji kwa nini wakatazwe kuhoji muungano, tangu mwanzo niliposikia hivyo nikasema Katiba haitapatikana.”
“Kama haitoshi, Warioba na tume yake walipofika kwangu nilimwambia mmeanza na mguu mbaya na nimewasilisha maoni yangu kwa maandishi, nilisema hamuwezi kufunga mkokoteni mbele ya punda mkasema uko sawa tuu.
“…. sasa ukiwaambia hawa kwa nini mawazo ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano hayachukuliwi, wanadai tukiwauliza watavunja Muungano, sasa si ndiyo mawazo yao? Waachiwe wayatoe,” alisema.
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema mawazo na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na kundi la G 55 lililokuwa likiundwa na wabunge wa CCM mwanzoni mwa miaka ya 1990 yalikuwa bora zaidi ya kile kinachofanywa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Kile kilichokataliwa wakati ule ni bora zaidi kuliko hiki kinachopendekezwa sasa. G 55 ilipendekeza na kutoa mawazo mazuri sana kuhusu muundo wa Muungano, lakini sasa sielewi kinachofanyika huko Dodoma.”
Alisema makosa mengine yaliyofanyika ni kitendo cha kuwaingiza wanasiasa kuwa wajumbe wa Bunge hilo.
Qares alisema hicho ni kiini cha mkwamo unaoendelea na kamwe hawawezi kuwaletea wananchi Katiba bora bali wanaangalia masilahi yao.

0 comments :

 
Top