Na Khelef
Nassor
Zanzibar: Mgombea wa urais wa
Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi CUF anayeungwa mkono na vyama vinavyounda
Ukawa, Maalim Seif Sharif Hamad amesema akichaguliwa kuwa rais, ataifanya
Bandari ya Zanzibar kuwa huru ili wananchi waweze kuingiza bidhaa zao bure
nchini.
“Mkinichagua, nitaifanya bandari ya Zanzibar
kuwa huru ili kutoa fursa kwa vijana wetu kupata ajira. Sisi tunataka kila
kijana mwenye uwezo wa kufanya kazi apate ajira” Alisema.
Katika hotuba yake aliyoitoa hapo
jana mbele ya wananchi wa Jimbo la Mfenesini ambao walikusanyika kwa wingi
katika uwanja wa Mwakaje, Maalim Seif aliahidi kutatua kero za wakulima na
wafugaji kwa kuwajengea mazingira wezeshi ambayo yatawasaidia kupata soko la
uhakika.
“Tutatilia mkazo kwenye kilimo na
ufugaji wa kisasa ili viweze kuleta tija kwa wakulima, Tutaimarisha sekta ya
ufugaji kwa kutilia mkazo ufugaji wa n`gombe wa kisasa ambao watatoa maziwa
mengi kwa kuingiza mbegu bora” Alisema Maalim Seif huku akishangiriwa na maelfu
ya wananchi waliokusanyika uwanjani hapo.
Akizungumzia suala la Elimu, Maalim
Seif ambaye pia ni Makamo wa Kwanza wa rais wa Zanzibar, amesema ataiboresha
sekta hiyo na kuahidi kuwa elimu itakuwa bure kwa ngazi zote ili kutoa fursa
wananchi wenye hali duni kuweza kujipatia elimu.
“Tutaijenga elimu kwa kuifanyia
marekebisho makubwa ili iweze kufikia kiwango cha kimataifa” Alisema.
Hata hivyo amesema ameandaa mipango
madhubuti ya kuboresha sekta ya afya ambayo imekuwa nyuma kwa takriban miaka 50
katika kuwahudumia wananchi na hivyo ameahidi kuiga mfumo kutoka nchi nyengine
katika uboreshaji wa sekta hiyo.
“Tutatumia mfumo wa Oman wa Kuangalia
tangu kidonge kinapoingia hadi kumfikia mgonjwa ili tuhakikishe kidonge hicho
kinamfikia mlengwa” Alisema Maalim Seif na Kushangiriwa na wananchi.
Mgombea huyo ambaye amekuwa akipiga
vita suala zima la ubaguzi alisema: “Wako viongozi wa CCM wanaowadanganya
wananchi kuwa eti kuwa nikipata urais nitawafukuza vijana kutoka bara, hilo si
kweli!, katika uongozi wangu nitahakikisha watu wote wanakuwa sawa, na hata
vijana kutoka bara watapata haki sawa na Wazanzibari”.
Maalim Seif ambaye aliambatana na
Kampeni meneja wake Nassor Mazrui, mara baada ya kumaliza hotuba yake,
aliwataka wananchi kumchagua na kumuunga mkono Mgombea wa urais wa Jamhuri ya
Muungano kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwani ndiye kiongozi pekee
atakayeweza kuleta maendeleo kwa Watanzania.
0 comments :
Post a Comment