TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


WAZIRI wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso leo Januari 6, 2021 amemvua madaraka Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Rorya, Mhandisi Evaristo Mgaya, kutokana na kushindwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji wananchi wapate huduma.

Waziri Aweso ameshusha ‘rungu’ hilo kwa Mhandisi Mgaya ikiwa ni siku moja imepita baada ya ‘kuwatumbua’ Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Sadick Chakka na mwenzake wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Marwa Murasa kutokana na uzembe wa aina hiyo kwenye maeneo yao ya uongozi.

Kilichompoza zaidi Mhandisi Mgaya ni miradi ya maji Kerogo na Shirati ambayo utekelezaji wake umekwamba na kusababisha wananchi wa maeneo hayo kuendelea kukosa huduma ya maji licha ya serikali kupeleka Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya kugharimia ukarabati, lakini pia milioni kadhaa kwa ajili ya usimamizi.

Imeelezwa kwamba mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni moja kwa ajili ya ukarabati wa mradi wa maji Kerogo, lakini hadi sasa hauoneshi dalili za kuwa msaada kwa wananchi.

Kwa upande wa mradi wa Shirati, imeezwa ulisimama kufanya kazi mwaka 2016 baada ya pampu kuharibika, ambapo serikali imetoa fedha za kuuhuisha lakini bado hakuna dalili kuanza kusambaza huduma ya maji kwa wananchi.

Kabla ya ‘kumtumbua Meneja huyo wa RUWASA Rorya, Waziri Aweso amempigia simu ya kiganjani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), CPA Joyce Msiru na kumuuliza gharama anazoweza kulipwa kwa ajili ya kuhuisha mradi wa maji Shirati, ambapo amemweleza Waziri kuwa kazi hiyo inahitaji Sh milioni 247.

Katika mawasiliano hayo, Waziri huyo ameahidi kuipatia MUWASA kiasi hicho cha fedha na kumtaka CPA Msiru kuanza kazi hiyo kesho Januari 7, 2021 na kuhakikisha inakamilika na mradi huo kuanza kusambaza maji kwa wananchi ndani ya kipindi cha siku 30 kama ambavyo Mkurugenzi Mtendaji huyo ameahidi. PAKUA APP YETU HAPA

0 comments :

 
Top