JESHI la Polisi,
Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, linazifanyia uchunguzi wa kina
taarifa zinazotolewa na wadau mbalimbali za baadhi ya watu wakiwemo
mawaziri, wabunge na wafanyabiashara kujihusisha na biashara haramu ya
dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limesema limechukua hatua mbalimbali
katika kudhibiti kushamiri kwa biashara hiyo nchini, ambapo kiasi cha
dawa zilizokamatwa kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, ni kidogo
ikilinganishwa na cha mwaka jana.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi,
Kamishna Msaidizi (ACP), Godfrey Nzowa, alisema Dar es Salaam jana
kwamba jeshi hilo limeongeza mbinu na mikakati ya kudhibiti biashara ya
dawa za kulevya na kuonya kuwa wahusika wote watakamatwa na kupambana na
mkono wa sheria.
“Wapo baadhi ambao tayari tumewahoji na uchunguzi unaendelea.
Ninachokiomba kwa wananchi ni kuwa wasitoe siri kwa kutumia mitandao ya
kijamii, watume siri hizo kwetu moja kwa moja, maana taarifa zinapotoka
kwenye mtandao wahusika wanapoteza ushahidi haraka,” alisema Nzowa
ambaye katika kuthibitisha hilo alisema jeshi hilo tayari limemhoji
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) kwa tuhuma za kujihusisha na
biashara hizo.
Kamishna huyo wa Polisi alisema taarifa za kuwepo kwa wabunge, mawaziri
na wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya, zimekuwa
zikifikia jeshi hilo kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ya
kijamii na kwamba hazipuuzwi bali zinafanyiwa kazi kwa nguvu kubwa.
Kuhusu Mbunge Azzan ambaye katika siku za hivi karibuni zimekuwepo
taarifa za kudaiwa kujihusisha na biashara ya dawa hizo, Kamishna Nzowa
alisema kwa kifupi; “Idd Azzan tumeshamhoji na uchunguzi unaendelea.”
Akizungumzia mafanikio ya mwaka huu, Nzowa alisema kuanzia Januari hadi
Julai, Polisi wamekamata kilo 32 za heroin, kilo 4 za kokeini, kilo
9,999 za bangi, kilo 6,628 za mirungi na kilo 11 za dawa mpya za kulevya
aina ya ephedrine, zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Afrika Kusini.
Alisema katika tukio la heroin watuhumiwa 44, kokeine watuhumiwa 18,
bangi watuhumiwa 1,478, mirungi watuhumiwa 532 na ephedrine mtuhumiwa
mmoja walikamatwa wakiwemo Wanaigeria watatu na wote wamefikishwa
mahakamani kujibu mashitaka.
“Tunawashukuru wananchi wa mikoa mbalimbali ambao ndio waliotupa
ushirikiano uliowezesha kuwakamata wahusika hawa wa dawa za kulevya
ambazo ziliingizwa kupitia katika viwanja vyetu vya ndege na baharini,”
alisema Nzowa.
Alisema vipo viashiria vinavyoonesha kudhibitiwa kwa biashara hiyo moja
ikiwa ni kupungua kwa kiasi ukilinganisha na takwimu za mwaka jana
zilipokamatwa kilo 260 za heroin na 151 za kokeini, lakini pia kupanda
ghafla kwa bei ya dawa hizo kufikia Sh milioni 50 na milioni 55 kwa kilo
moja.
Alisema vita dhidi ya dawa hizo si ya Tanzania pekee, bali dunia nzima
ambapo viongozi wa mataifa mbalimbali ya ndani na nje ya Afrika wamekuwa
wakikutana mara kwa mara kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na
biashara hiyo ambayo inawahusisha watu wenye uwezo mkubwa sana wa
kifedha.
“Sasa hivi tupo katika mikakati ya kuifanya sheria inayohusiana na dawa
za kulevya kuwa inayojitegemea badala ya kuchanganywa na sheria
nyingine, lakini pia tunataka kuweka adhabu kali kwa nchi zote ili mtu
anapokamatwa katika nchi yoyote anakumbana na adhabu kali na si katika
nchi nyingine adhabu kuwa ndogo.”
Alisema jeshi hilo limegundua pia kuwepo mbinu mpya za usafirishaji wa
dawa hizo kwa kubadili vifungashio kutoka katika gundi ya karatasi
(selotepu) ya awali na sasa kuwekwa katika vifungashio vinavyoonesha
kuwa ni kahawa halisi, sukari na hata kuzibadili dawa hizo kutoka katika
unga na kuwa vimiminika.
Kwa hisani ya habarileo.
Home
»
»Unlabelled
»
POLISI WAANZA KUHAHA NA KUTEMA CHECHE JUU YA MADAWA YA KULEVYA
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment