![]() |
| Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (CHADEMA) |
KAMBI Rasmi ya Upinzani, imeitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kupata sheria mpya ya uhuru wa vyombo vya habari ili kufuta sheria kandamizi zinazominya uhuru wa habari.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Joseph Mbilinyi, wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Mbilinyi alisema ahadi ya Serikali kuleta muswada wa habari ni ya muda mrefu ambapo mwaka jana wananchi walifarijika kumsikia Rais Kikwete akitoa ahadi kwa maneno mazito mbele ya mkutano wa kimataifa ulioitishwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon.
Alisema Rais Kikwete, aliahidi serikali yake ingepeleka muswada wa Sheria wa Haki ya kupata Taarifa Aprili mwaka huu, lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezeka
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Kikwete akizungumza kwenye mkutano huo Oktoba 31, alisema sio tu kwamba aliwaahidi watanzania bali pia alitumia jukwaa hilo la kimataifa kuitangazia dunia nzima kuwa Serikali yake tayari inafanyia kazi utungaji wa Sheria ya Kupata Taarifa, kwa ajili ya kuwapatia wananchi haki ya kupata taarifa kutoka serikalini. Ahadi hiyo iko wapi?” alihoji Mbilinyi.
Hata hivyo alisema kuwa majibu ya Serikali yaliyotolewa hivi karibu bungeni kwenye mkutano huu wa 15 kuhusu miswada ya sheria hizi mbili na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Serikali ikashindwa kutoa majibu ya kuridhisha, inazidi kudhihirisha kuwa hakuna dhamira ya dhati kutekeleza jambo hili.
Alisema kambi rasmi ya upinzani inalaani kwa nguvu zote, sheria kandamizi zinazonyima uhuru wa habari ambao unasaidia kufichua maovu kama rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na hujuma za rasilimali za taifa.
Alisema sheria hizo zinatishia uhuru wa uhariri na kuleta woga wa kushtakiwa kwa makosa ya jinai.
“Wote tunafahamu kuwa sheria zilizopo zinazosimamia vyombo vya habari ni mbaya, ni kandamizi na hazina nafasi katika nchi inayojinadi kuwa ni ya kidemokrasia. Sheria hizi zinavifanya vyombo vya habari na wanahabari kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu,” alisema

0 comments :
Post a Comment