Dar es Salaam. Kesi ya madai inayoikabili kampuni ya Mwananchi Communications Ltd iliyofunguliwa na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imeanza kutajwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo imefunguliwa na IPTL, Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited pamoja na Harbinder Singh Sethi anayedaiwa kuwa mmiliki mpya wa IPTL dhidi ya magazeti ya Mwananchi na The Citizen kwa madai ya kuchapisha habari zilizolenga kuichafua kampuni hiyo.
Kesi hiyo namba 47 ya mwaka 2014 imepangwa kusikilizwa na Jaji Salvatory Bongole na ilianza kutajwa jana mahakamani hapo kabla ya kuahirishwa hadi Julai 22 itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo walalamikaji hao wanaiomba mahakama hiyo iamuru magazeti ya Mwananchi na The Citizen yawaombe radhi na kuilipa fidia ya jumla ya Dola 5.5 bilioni za Kimarekani (Sh8.8 trilioni). Walalamikaji hao wanawakilishwa na kampuni tatu maarufu za uwakili. Kampuni hizo ni pamoja na Bulwark Associates Advocates, Mawalla Advocates na ASYLA Attorneys.
Kwa mujibu wa hati ya madai walalamikaji wanadai kuwa Machi 5, 2014, gazeti la Mwananchi na mchapishaji wake Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa pamoja walichapisha habari iliyolenga kuwakashifu mbele ya jamii.
Pia wanadai gazeti dada la The Citizen na mchapishaji wa magazeti hayo ambayo ni kampuni ya Mwananchi Communications Ltd katika siku tofauti kuanzia Machi 3 hadi 12 lilichapisha mfululizo wa habari zilizolenga kuwachafua.
Tayari Mwananchi kupitia kwa wakili wake, Frank Mwalongo wa kampuni ya uwakili ya Apex Attorneys Advocates imeshawasilisha utetezi wake wa maandishi na mahakama imewaamuru walalamikaji wawasilishe majibu yao Julai 16, 2014.
Wakati walalamikaji hao wakifungua kesi mahakamani, Serikali imeagiza sakata hilo lichunguzwe.
Chanzo Mwananchi
0 comments :
Post a Comment