Mwenendo wa Kampeni za CCM
Hadi jana, tarehe 16 September 2015, Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe Magufuli, alikuwa amekwishafanya kampeni katika mikoa 12 na Majimbo 94. Amekwishafanya mikutano mikubwa ya hadhara 76 na mikutano ya barabarani 381. Amekwishatembea, kwa gari, jumla ya kilomita 13,720. Kwa ujumla amekwishakutana, moja kwa moja, na asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura. Kwa kuwa baadhi ya mikutano yetu inatangazwa moja kwa moja na redio za kijamii na luninga, wapiga kura waliopata nafasi ya kumsikia wanakadiriwa kufikia asilimia 70.
Hadi jana, tarehe 16 September 2015, Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe Magufuli, alikuwa amekwishafanya kampeni katika mikoa 12 na Majimbo 94. Amekwishafanya mikutano mikubwa ya hadhara 76 na mikutano ya barabarani 381. Amekwishatembea, kwa gari, jumla ya kilomita 13,720. Kwa ujumla amekwishakutana, moja kwa moja, na asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura. Kwa kuwa baadhi ya mikutano yetu inatangazwa moja kwa moja na redio za kijamii na luninga, wapiga kura waliopata nafasi ya kumsikia wanakadiriwa kufikia asilimia 70.
Tunafarijika na idadi kubwa ya watu wanaokuja kwenye mikutano ya
kampeni zetu. Tunafarijika pia kwamba karibu Watanzania wote wanaopata
fursa ya kumuona na kumsikia wamemuelewa na wamepata matumaini ya
Tanzania Mpya kupitia kwake. Utafiti wetu wa ndani, tulioufanya kwa
kipindi cha siku kumi zilizopita katika majimbo 246 kati ya majimbo 269,
unaonyesha kwamba Dr. Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3.
Tunaamini kwamba asilimia hizi zitaongezek kadri Watanzania wengi zaidi
wanavyopata fursa ya kumsikiliza Dr. Magufuli na kusikiliza Ilani na
sera za CCM.
Kwa
upande wa kampeni zetu za Ubunge, zaidi ya robo tatu ya wagombea Ubunge
wa CCM wamekwishazindua kampeni zao na wanaendelea vizuri. Sekretarieti
ya Kampeni ya CCM
inaanda program maalum ya kampeni katika majimbo yenye changamoto
mahsusi. Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha wana-CCM kwamba viongozi
na makada wengine wa CCM, waliopo madarakani na wastaafu watapita tena,
jimbo kwa jimbo, nchi nzima katika siku 30 za mwisho katika jitihada za
kuongeza ushindi wa CCM na Dr. Magufuli.
Midahalo ya Wagombea
Wiki tatu zilizopita, CCM, na kwa hakika vyama vingine pia, ilipokea
mwaliko wa Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe Magufuli, kushiriki
kwenye mdahalo wa wagombea Urais uliondaliwa na Baraza la Habari
Tanzania (Media Council of Tanzania) kwa kushirikiana na taasisi
nyingine kadhaa, ikiwemo Twaweza. Dr. Magufuli amekubali kushiriki
katika mdahalo huo. Kwa msingi huo, kauli ya UKAWA iliyotolewa jana na
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ndugu James Mbatia, kwamba UKAWA inaomba
mdahalo ni njia ya
kuwahadaa Watanzania tu kwa kuwa mwaliko wa mdahalo ulikwishatolewa
mapema kwa vyama vyote na wanaotakiwa kushiriki ni wagombea Urais wa
vyama.
CCM
inafurahishwa na utamaduni wa midahalo ambao unaanza kujitokeza katika
chaguzi zetu. Na inaamini kwamba midahalo ya Wagombea Urais ni sehemu
muhimu ya kuwashirikisha wapiga kura katika mchakato wa uchaguzi na
kuwasaidia waamue nani wamchague kwa misingi ya hoja na sera na sio kwa
ushabiki, kwa mihemko, na kwa propaganda. Mdahalo unatoa fursa ya
wagombea kuulizwa maswali ya moja kwa moja na kutoa ufafanuzi wa kina
kuhusu sera na ahadi zao, fursa ambayo hawaipati kwenye mikutano ya
hadhara kampeni.
Hatukubaliani na kauli ya UKAWA kwamba mdahalo usiwe baina ya wagombea
bali uwe baina ya Wenyeviti wa Vyama. Tunaamini hoja hii ni kichekesho.
Haijawahi kutokea popote duniani kwenye utamaduni wa midahalo, kwamba
wagombea wasishiriki bali watu wengine ndio wafanye midahalo kwa niaba
yao. Tunaamini mdahalo huu unapaswa kuwa baina ya wagombea. Wao ndio
wanaoomba dhamana. Wao ndio wanaopaswa kujibu maswali na kufafanua
kuhusu ahadi zao. CCM inaamini kwamba ili mdahalo huu uwe na tija,
wagombea Urais wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki. Mdahalo
hautakuwa na maana kama mgombea mmojawapo wa vyama vikuu atatengeneza
kisingizio ili asishiriki.
UCHAGUZI WA AMANI
CCM inasikitishwa na kauli zinatolewa na baadhi ya viongozi wa UKAWA
zenye kuashiria fujo na vurugu. Kauli kwamba kura zitaibiwa hazina
msingi wowote. Kauli hizi zinaashiria maandalizi ya kushindwa na
maandalizi ya kufanya vurugu baada ya matokeo ya kushindwa.
Utaratibu wa uchaguzi wetu unajulikana na umekubalika na
vyama vyote. Kura zinapigwa kituoni na kuhesabiwa kituoni mbele ya
mawakala wa vyama vyote, wasimamizi wa uchaguzi na waangalizi wa
uchaguzi wa ndani na nje ya nchi. Baada ya kura kuhesabiwa, matokeo
yanajazwa katika fomu ambayo kila wakala anasaini na kupewa nakala.
Nakala ya matokeo hayo pia inabandikwa nje ya kituo cha kupiga kura.
Kila Chama, na kila Mtanzania, kina fursa ya kujumlisha matokeo yake
kwenye kila kituo na kupata jumla kuu. Matokeo ya nchi nzima
yanajumlishwa mahala pamoja huku kukiwa na waangalizi wa uchaguzi wa
ndani na nje ya nchi, pamoja na wawakilishi wa vyama vyote na wao wakiwa
na fomu zao za kila kituo nchi nzima.
Tunapenda kuwasihi Watanzania wasikubali vishawishi vya kufanya vurugu.
Mara nyingi, viongozi wanaohamasisha vurugu wanakuwa na ulinzi au
walinzi au uwezo wa kukimbilia pahala penye utulivu zaidi huku
wakiwaacha wafuasi wao katika wakihangaika.
UCHAGUZI NA UMOJA WA KITAIFA
CCM pia inapenda kusisitiza imani yake kwamba uchaguzi haupaswi
kutugawa kama taifa. Uchaguzi ni tukio la kupita. Kuna maisha baada ya
uchaguzi. Kuna taifa baada ya uchaguzi. Lazima taifa liendelee kubaki
moja, tuendelee kubaki wamoja. Tusitoe kauli za kupitiliza zenye mrengo
wa kujenga chuki katika jamii na kuhatarisha umoja na amani ya nchi
yetu.
Kama Chama
kilichoasisi umoja wa taifa letu, tunaendelea kuasa kwamba wanasiasa
wasijinadi kwa misingi ya udini, ukabila wala ukanda. CCM haina mpango
kuendeleza mjadala wa kauli ya Mgombea wa UKAWA Ndugu Edward Lowassa
aliyoitoa kanisani Tabora tarehe 6 September 2015 kwamba nchi ilishapata
viongozi Wakatoliki na kwamba sasa ni zamu ya Walutheri kuchukua nafasi
hiyo. Tunaamini mjadala huo hauna tija. Tunaamini kwamba Watanzania
wengi, wa dini na madhehebu yote, hawaamini katika siasa za namna hii.
Tuliamini kwamba UKAWA ingetumia fursa ya mkutano wao na waandishi wa
habari jana kuomba radhi kwa Watanzania. Kwakuwa hawakufanya hivyo,
tunapendekeza mjadala wa jambo hili ufungwe. Itoshe tu kwamba Ndugu
Lowassa amesema hivyo, Tume ya Uchaguzi imemuonya, na yeye hajajitokeza
kuomba radhi wala kufafanua. Watanzania wamemjua ni kiongozi wa aina
gani na watatoa hukumu yao tarehe 25 Oktoba 2015.
Imetolewa na
Ndugu Januari Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
16 Septemba 2015
Ndugu Januari Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
16 Septemba 2015
0 comments :
Post a Comment