TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

Kocha wa Taifa Stars , Boniface Mkwasa akizungumzia mwenendo wa timu hiyo

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi chake kilikuwa na tatizo ufundi na kukosa mazoezi ya ukakamavu, upungufu uliosababisha kufanya vibaya chini ya mtangulizi wake, Mart Nooij.
Mkwasasa aliyeiongoza Stars kutoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Uganda Cranes Jumamosi iliyopita aliwaambia wanahabari jana kuwa kabla ya mechi hiyo, asilimia kubwa ya wachezaji wa Stars walikuwa na kasoro kubwa mbili.
“Tanzania hatukustahili kufungwa na Uganda, kama tungeitumia mechi yetu ya nyumbani vizuri, matokeo ya ugenini ya 1-1 yangetubeba, lakini kuna kitu ambacho nadhani kocha aliyepita hakuzingatia.
“Wakati nakabidhiwa timu nilichokigundua ni kwamba, wachezaji wengi hawakuwa na utimamu wa mwili na ufundi, hizo zilikuwa kasoro kubwa kwa timu yetu, nilijaribu kuwa nao kwa kipindi kifupi nilichokabidhiwa na taratibu wameanza kubadilika,” alisema.
Akizungumzia mchezo na Uganda Cranes, Mkwasa alisema, “Vijana wangu walicheza vizuri hata wenyeji hawakutarajia, kila mmoja alishangaa ni vipi walitufunga nyumbani mabao 3-0, ilifikia mahali baada ya kuzidiwa walitumia mbinu zisizofaa ili kututoa mchezoni.
“Kama tutaendelea hivi na kuungwa mkono, hakuna ubishi Stars itafika mbali,” alisema.
Aidha, Mkwasa alieleza kuwa, baada ya michuano ya Kombe la Kagame, Stars itaingia kambini kujiweka fiti kwa ajili ya mchezo wao wa Septemba 4 dhidi ya Nigeria wa kufuzu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2017.
“Wale watakaofanya vizuri Kagame nitawajumuisha kwenye kikosi changu, lakini pia kwa zile timu ambazo hazishiriki michuano hiyo, kuna programu inaandaliwa ili kuwapima wachezaji wao kabla ya uteuzi wa kikosi kipya cha Taifa,” alisema.

0 comments :

 
Top