Tangu juzi kumekuwapo na tetesi kuwa vyama vinavyounda umoja wa
katiba ya wananchi UKAWA, huenda umoja huu ukasambaratika kwa kile
kinachoelezwa kutokukubaliana kwa mgawanyo sawa wa majimbo kuelekea
uchaguzi mkuu Oktoba.
Imeripotiwa pia leo vijana wa chama cha wananchi CUF na NCCR mageuzi,
wanatarajia kuandamana ili kushinikiza viongozi wa juu wa vyama vyao
kuachana na UKAWA kwa kile wanachokiita kupunjwa usawa wa uwakilishi
katika majimbo na CHADEMA.
Naibu katibu mkuu wa CUF Tanzania bara, Julius Mtatiro amekuwa akitoa
mtazamo wake mara kwa mara kuhusu kadhia na migogoro hii ya UKAWA,
akisisitiza kutokukubaliana na kuvunjika kwao.
Timesfm.co.tz imeunasa waraka aliouandika kwenye ukurasa wake wa
Facebook, ili kufahamu kile ambacho anakifikiri kama kiongozi wa chama
kinachounda UKAWA.
“SHEREHE ZA KUVUNJA UKAWA??? Ndugu zangu, Tangu jana nimeona MATAMKO
ya watu mbalimbali wakijinasibu kwamba ni bora UKAWA ivunjike, wengine
wanasema vyama vyao vinamezwa, wengine wanasema hawakubali hili na lile
n.k. bahati mbaya haya yasemwayo ni mambo ambayo viongozi wa juu wa
UKAWA ndiyo wanapaswa kuyashughulikia, si viongozi wa kawaida wa vyama
au wanachama.
Mimi nataka tena kurudia kusema hapa, kwamba UKAWA ikivunjika kwa
sababu yoyote ile, ni KITENDO CHA VYAMA VYA UPINZANI KUWASALITI
WANANCHI. Hakuna lugha nyingine.
Na wale wanaofurahia UKAWA ikitetereka na wanaoombea ivunjike
waendelee kuomba maombi hayo yasiyo na tija kwa taifa. UKAWA
ikishavunjika vyama vya upinzani havitabaki salama hata kidogo.
Athari ambazo chama kimojakimoja kinazipata ndani ya UKAWA ni chache
kuliko chama kimojakimoja kikienda kivyake. UKAWA ilikuwa na malengo
makubwa sana, achilia mbali uchaguzi, kuna ajenda ya katiba.
Tuliondoka kwenye bunge la katiba na kuacha milioni 30 kila mjumbe
kwa sababu ya kujenga mshikamano wa upinzani. Kuvunja UKAWA leo ni
kusema pia TUNAIKUBALI KATIBA inayopendekezwa. Tukivunja UKAWA leo
#Tutapigwa_kwenye_uchaguzi_mkuu_huu lakini zaidi ya yote
#Wananchi_Watatupiga_Mawe_Tutakapojipeleka_Kuwaambia_Waikatae_Katiba_Inayopendekezwa
kwani tutakuwa
#Hatuaminiki_Kwa_Mambo_Madogo_Na_Hatuwezi_Kuaminika_Kwa_Mambo_Makubwa.
Mimi naamini katika USHIRIKIANO WA VYAMA VYA KIMABADILIKO ili
kulikomboa taifa, siamini kinyume chake hata kidogo. Kwa sababu viongozi
waliahidi leo ndipo wataamua mustakabali wa kila kitu, kila mpenda
mabadiliko anasubiri kwa hamu kujua viongozi wanaongoza tupite njia ipi.
Mungu awabariki nyote.” ameandika Mtatiro
0 comments :
Post a Comment