TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749


Chalinze. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema hadi sasa wameshaandikisha wapigakura zaidi ya milioni kumi na moja kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini kote.
Kutokana na idadi hiyo, Jaji Lubuva amesema NEC ina uhakika wa kukamilisha kazi hiyo ya uandikishaji mapema Agosti mwaka huu.
Alisema hayo jana alipokuwa Msoga, Chalinze wilayani Bagamoyo wakati akitoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa wananchi wa eneo hilo waliojitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza kazi hiyo mkoani Pwani.
Alimueleza Rais Kikwete kuwa licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mchakato huo, hali ya uandikishaji ilipofikia nchini hadi juzi ni nzuri na matumaini ya NEC ni kukamilika mapema Agosti kwa kuwafikia walengwa wote waliokusudiwa.
Awali, Jaji Lubuva alikuwa akisema kuwa kazi hiyo ingekamilika Julai na hata uandikishaji uliposogezwa mbele kwa jiji la Dar es Salaam na Pwani, NEC ilisisitiza kuwa utakamilika kabla ya mwisho wa Julai.
“Mheshimiwa Rais, pamoja na changamoto nyingi na kelele nyingi zilizokuwa zikisikika huku na kule, tayari tumeandikisha watu 11,248,198 mpaka jana (juzi) kati ya lengo tulilojiwekea la kuwafikia watu kati ya milioni 21 mpaka 23 na mikoa iliyokuwa tayari imekamilisha zoezi hili ni 13, bado kumi na moja ambayo nayo nakuhakikishia itakamilisha na mapema mwezi Agosti kazi hii itakamilika,” alisema Jaji Lubuva.
Chanzo  Mwananchi

0 comments :

 
Top