“Human is Politically Animal” ni mwanafalsafa wa Kigiriki
Aristotle aliyanena haya miaka mingi kabla ya ujio wa Yesu Kristo .Unajua
alimaanisha nini? Huwezi kuikwepa siasa kwenye maisha ya kila siku,na nilizidi kukubaliana
na hili miezi kadhaa zilizopita nikiwa na rafiki yangu ninayesoma naye tukiwa
kituo cha daladala Mwananchi,Tabata tukisubiri daladala kuelekea katika ofisi
za gazeti la Nipashe nilizofika kwa mara ya kwanza siku hiyo.
Watanzania ni wazungumzaji wazuri, kuingia tu ndani ya
daladala,mazungumzo yaliyotawala kwa asilimia kubwa ni juu ya siasa za “kibongo”. Kutokana msongamano nilitamani
nifike karibu na siti mbili za mwisho “soga” liliponoga hata niwasikilize kwa
umakini.
Jamaa mmoja wa makamo alidai “Watanzania “wanajitambua” tayari huwezi
kuwadanganya kwasasa”. Walio wengi wakaenda mbali kwa kupinga wakidai hali ya
nchi ilipofikia inatia shaka kiuchumi haswa kutokana na utekelezaji mbovu wamikakati
,hao wananchi wenye utambuzi wamechukua hatua gani kama demokrasia ipo mikononi
mwao?
Kwangu mimi na fikra zangu nikasema Watanzania wapo
katika “mchakato” wa kujitambua kwa
kuwakumbukusha asilimia 80 ya kura za
uchaguzi wa 2005 na asilimia 61.7 za
2010 alizoshinda Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete,basi Watanzania wanazidi kupata
elimu juu ya masuala yao ya kimsingi
siku zinavyozidi kwenda,umaarufu wa CCM unapungua kama wao ni kikwazo.
Hili suala la ufisadi na hakuna ajira,wananchi wamechoka na mtazamo wa baadhi yao wakadai bora itokee
“VITA”.Hapo ndipo nikachangia nikasema tusifike kwenye “SIASA NYEKUNDU” yaani
kumwaga damu(ikiwemo vita), kwenye “SIASA NYEUSI” iliyopo sasa ya kudanganywa na ufisadi
uliokithiri tuitengeneze
kuwa “SIASA NYEUPE” kwa kura za haki kwa wingi tumweke kiongozi mwajibikaji. Jamaa
mmoja wa makamo akaniambia “acha kuwa mwoga”,
ikabidi ninyamaze kidogo wakiendeleza “ ugomvi wa maneno”.Baadhi yao
wakisema bora vita katika kudai haki, iweje Waarabu wamezoea?
Jamani vita inazoeleka kweli waungwana ?Nikagundua kuna watu wanaopenda kubishana tu pasipo kuwa na
“mpangilio mzuri wa fikra” ili safari
ndefu ya daladala na foleni iishe. Nikakumbuka kumbe nipo jiji la Dar es Salaam.
Sikuwalaumu.
Sikupenda kuendelea kubishana nao, kuna ndugu mmoja wa
makamo nikamwita “anko” nikamwambia hali tutaibadilishaje wakati viongozi
wamewahadaa wananchi maisha bora na ajira kwa vijana imebaki kitendawili na
mteguaji hajulikani na ndio sababu baadhi ya Wananchi wanasema watumie njia
nyingine kimtazamo wa kawaida zisizo na mfanano na mazingira ya kitanzania.
Fikra zikamkumbuka shujaa aliyeuwawa kwa kutetea haki za Watu weusi Marekani
Malcom X alisema “If you’re not ready
die for it put the word freedom out of your mouth”- kwa tafsiri isiyo rasmi ni
kuwa “ kama huwezi kuifia, ondoa neno uhuru mdomoni mwako” lakini alikuwa sahihi.
Inawezekana kwa mapambano yale ni wazi
kujitoa kwa namna ile kulihitajika, muda unakwenda zama zinabadilika. Siku
hazigandi, mabadiliko. Kupiga kura hasa vijana kwa chaguzi zlizopita imekuwa ya kusuasua. Je hatua wanayowaza
inakuwaje? Ukomavu wa kisiasa wa hivyo hatujafikia.
Watanzania cha kufanya
ni kuigeuza kuwa “SIASA NYEUPE” yaani siasa safi na kura kwa sasa ndio silaha,haya tujiandikishe
kwa wingi tumweke mwajibikaji na mzalendo.Nikakumbushia lile balaa la Arusha la
milipuko ya mabomu, eneo la Sanawari na Maeneo baadhi Arusha mjini, watu hawakukaa kwenye maeneo yao
ya biashara ,kila kona mbio,vipi mabomu ya machozi yanavyozima migomo ya wanachuo? Hilo la “SIASA NYEKUNDU”
hatujalifikia hilo, dawa ni KUANDAA KURA YAKO VYEMA.
Yaliyotokea Tanzania Visiwani baada ya uchaguzi, mwaka 2001 ya wafuasi wa CCM na CUF kushambuliana, sipendi kuyasikia tena!
Unadhani Baba wa Taifa alikuwa “mjinga” kusita kuingia
kwenye vita kirahisi na kuamua kufanya maamuzi magumu kuruhusu Jeshi letu kakamavu
likapambane? Unajua alichofanya nasikia alikesha na rozari kanisani usiku
kucha?Alikuwa muumini mzuri wa “imani” Alijua madhara yake,Uchumi ulikuwaje
baada ya vita? Wazee wetu wanayo majibu.Uchumi ulishuka sana.
Yule niliyemwita “anko” alinikumbusha habari niliyohadithiwa
na mjomba wangu aliyesoma na kina Mheshimiwa Rais Kikwete pale Shule ya Tanga (Tanga
School )
enzi za Mwalimu Mkuu wa fikra yakini J.K
Nyerere, juu ya Elimu, Chakula(asubuhi chai nzito), na usafiri wa bure kwa gharama za Serikali. Akaniuliza leo
hii nyie madaftari ni elfu moja mpaka elfu tatu, fedha ya kitanzania, halafu tuna misitu mikubwa
nchini?
Nikawaza hali ya shule za msingi hakuna madawati ,Vyuo Vikuu
kuna suala mikopo,watoto wa wakulima tunavyojikaza, nani atakufikiria .
Nikazama kifkra zaidi nikakumbuka miezi ya karibuni, Mheshiwa Joseph
Mbilinyi “Sugu” yule nguli wa mziki wa
kufoka foka ( Hip Hop), mbunge wa Mbeya Mjini pale kwenye Bunge la Katiba
alichokisema juu ya Serikali isivyosikivu juu ya ushauri wa Vyama pinzani
kuhusiana na Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura unahitaji muda katika
kuuandaa na maswala mengine yenye
maslahi kitaifa yasiyohitaji mgawanyiko wa itikadi na uchama kwa kile alichosema nambari haidanganyi kwa kufanya mambo kwa
“ tathmini onyeshi” moja ni moja na nane si saba, nikagundua kuwa watu
wana uzoefu na matukio haya kinyama kwa kuona kwenye “video” , kuhadithiwa vita ya Kagera pasipo kushuhudia, na kusikia
mauaji ya kimbari kule Rwanda kuwa yalipoteza maisha ya Watu kadhaa bila
kutafakari kwa kina matokeo ya vitu wanavyofikiria.Wale wakimbizi pale Bulombora,Kigoma
hali ilikuwa inatishaje? Njaa, ambaye ni
adui namba moja alihusika pale.
“Nyuma ya pazia” eti Israeli alipompiga Libya enzi za Kanali
Muammar Qaddafi miaka ya nyuma katika sekeseke la Umoja wan nchi za Kiarabu
(Arab League) alichokumbuka alimletea chakula cha msaada.Unajua waliwaza nini?
Njaa kwa kuwa vita inaendelea nani anazilisha? tusiyawaze hayo Watanzania
tukomae kuleta “Siasa Nyeupe”, na tunailetaje? Hili ndio suala la msingi na sio
kusema wanatudanganya, na mfumo wao umekomaa. Utabadili sio maneno, mpiga kura
akijua kilo za sukari kutoka kwa mgombea zilivyo kitulizo cha njaa ya usiku kuamka asubuhi kuna siku ndefu tunaiita baada ya uchaguzi, ANDAA KURA YAKO.
Nikawaza mbali kwa kina
kuwakumbuka makada wa CCM na mbio
za kugombea urais kupitia chama hicho, zaidi ya 30 walikuepo katika vikumbo vya kuingia kwenye “hekalu la
kaisari” hatimaye Ndugu Dkt. John Magufuli akaibuka kidedea, chama kimepoteza sifa fulani,
wanataka kuirudisha.Usishangae walivyotupiana madongo. Wanajua wanachofanya.
ANDAA KURA YAKO VYEMA.
Nikatafakari nikajua kuna jambo walilifanya, yawezekana
kuwaachia uhuru wananchi kutathmini nani anastahili na kuwatengeneza vijana
waliotangaza nia njia na “CV” kwa miaka ijayo. ANDAA KURA YAKO SASA.
UKAWA wanasoma alama za nyakati ulidhani Ndugu Edward Lowassa wangemkataa kuwepo kwenye umoja wao, na hao wengine kama Ndugu Fredrick Sumaye! wamechanganya maarifa, hivyo akili hazijaganda, wanaelewa nini Wananchi wanahitaji. ANDAA KURA YAKO.
Ujasiri ni pale unapojua "SIASA" si tatizo bali tatizo ni picha na taswira iliyojengeka mtu
kuwa "MWANASIASA" ndani ya jamii na jibu unalo ili kugeuza neno
"politics is dirty game" kwa "KUPIGA KURA PEKEE WASHIKAJI!.
Ukijiamini unafanikiwa, unaonekana shujaa kutoka kwenye dimbwi la mfumo usio na kweli kiutawala utaitwa msaliti ni bora kuliko kuonekana mnyenyekevu kwao halafu kwenye jamii uonekane kamuzu Banda wa Malawi. wazee wetu ukiwauliza watakujibu enzi za kupigania uhuru walimwita Dkt. Kamuzu Banda "aliyeolewa na mzungu" aliwabania waafrika haki zao , ndiyo nyimbo iliyokuwa kwenye mchamchaka.
Kwanini nimesema hayo? Nakumbusha raia wote wasaliti kwa machinga, boda boda, mama ntilie , wasakatonge , wasio na ajira kwa kubali kununuliwa kwa kofia, khanga ,kilo za sukari ni bora uonekane umemsaliti rafiki yako anayetafuta uongozi kwa njia ya kuzunguka kuliko kuitwa "umeolewa nao" na jamii ni mbaya sana, laana mbaya kabisa! ANDAA KURA VYEMA!
Nikamwona kifkra shujaa wa India, Mahatma Ghandi na falsafa
yake kuwa “I love your Christ but not your Christianity” nikimaanisha CCM na
UKAWA ni sehemu salama na sera zenye weledi lakini walioko ndani yake ndiyo kuna kila aina ya
ubaya,udhalimu, na siasa chafu japo kuna wasafi na wenye kweli daima. Naipenda
sera weledi yenye utekelezaji, itikadi ninayo,na “imani” kwa mgombea yoyote mwenye misingi fanikishi ya
kuileta “TANZANIA NINAYOITAKA”,mpya isiyo
ya “ skendo ya ESCROW, mauaji ya Mwandishi Mwangosi, kutekwa kwa Mwandishi
Kibanda na Dkt. Ulimboka na kauli za kibabe za
“makaisari” wetu na sio ushabiki
wa chama. Haya yakifanikiwa mbona “SIASA NYEUPE” itaonekana kama UKIANDAA KURA YAKO VYEMA!
Watanzania ni wepesi wa kusahau kama 2015 zao la kura litaleta watu makini, wazalendo,wenye dira
elekevu, na misimamo binafsi tutakuwa
tumefikia kiwango kikubwa katika “mchakato” wa kujitambua na kuutambua ukweli
na ule mtazamo wa siasa ni mchezo mchafu (politics is the dirty game) utaanza
kufifia kama UKIANDAA KURA YAKO VYEMA!
Kura ni haki ya kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na
zaidi, mwenye akili timamu na sababu zingine muhimu,vijana ndio chachu ya mageuzi
na sio kulalamika ni mchezo mchafu,tukajiandikishe, oktoba 25, mapema tujitokeze,
kwani kura ya Mtanzania mmoja mwenye
“imani” na maneno ya Mwalimu Nyerere “ sababu tunayo,nia tunayo,uwezo tunao na
nguvu tunazo” ni muhimu kuliko kura za
vichwa kumi zilizopewa kilo mbilimbili
za sukari na mgombea yule mwenye tai kubwa na maneno mengi yenye asali shubiri.
Najinukuu mwenyewe tena kama nilivyoandika hapo juu, "nakumbusha tu raia wote wasaliti kwa machinga, boda boda, mama ntilie , wasakatonge , wasio na ajira kwa
kubali kununuliwa kwa kofia, khanga ,kilo za sukari ni bora uonekane
umemsaliti rafiki yako anayetafuta uongozi kwa njia ya yake kuzunguka kuliko
kuitwa "umeolewa nao" na jamii ni mbaya sana, laana mbaya kabisa inaweza tafuna mpaka viunoni mwako!
PETER C. MMBAGA.
MWANAFUNZI CHUO
KIKUU, TANZANIA



0 comments :
Post a Comment