Na Khelef Nassor
Zanzibar:
Chama cha wananchi CUF kimewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kuwa
watulivu na wavumilivu katika kipindi hichi, kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa
Mwenyekiti wake wa chama Profesa Ibraahim Lipumba. Wito huo umetolewa na Kaimu
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa chama hicho mhesimiwa
Ismail Jussa Ladhu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika
ofisi ndogo ya chama hicho huko Vuga mjini Unguja.
Akizungumzia
hatua ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti huyo, mheshimiwa Jussa amesema chama chama
cha wananchi CUF kimezipokea taarifa hizo na wanaheshimu maamuzi yake kwani ni
haki yake kikatiba na kidemkrasia.
Aidha
emesema, Profesa Lipumba amekuwa na mchango mkubwa katika miaka yote 16 ya
uwenyekiti wake kwa chama cha CUF, nafasi ambayo imemfanya awe kiongozi wao
mkuu
“Kwa
nafasi yake hiyo, pia ametoa mchango
mkubwa katika ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu. Tunaithamini kazi hiyo na
tutaendelea kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa kwa chama chetu na nchi yetu.
Tuamtakia kila la kheri katika mipango yake ya baadae” Jussa alisema.
Jussa
ameendelea kusema kuwa, Chama Cha Wananchi CUF ni taasisi na kinaendeshwa
kitaasisi, hivyo basi maamuzi yake yote yamekuwa yakifanywa kitaasisi kwa
mujibu wa katiba na kanuni za chama.
Kwa
upande wa historia ya chama cha CUF, Jussa amesema chama hicho kimepita katika
dhoruba na misukosuko mingi lakini mara zote wamekuwa wakionesha uwezo mkubwa
wa kuhimili dhoruba na misukosuko hiyo, na kusisitiza kuwa hawana hata chembe
ya wasiwasi kwani mtihani huo watauvuka na kuwa chama imara zaidi.
Aidha
ameeleza kuwa Chama cha wananchi CUF kimepanga kuitisha vikao vya dharura vya
Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza kuu la Uongozi la Taifa siku ya Jumapili,
tarehe 9 Agosti, 2015 ili kujadili hatua hiyo na kufanya maamuzi juu ya hatua
muafaka zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi hiki hadi hapo chama
kitakapomchagua mwanachama mwengine kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti.
Akizungumzia
ushirikiano wa chama cha CUF na UKAWA, mheshimiwa Jussa amesema chama cha CUF
kitaendelea na shughuli zake kama chama na pia kama mshirika wa UKAWA ambayo
CUF ilikuwa ni katika waasisi wake. Hivyo amewahakikishia wanachama na
watanzania wote kwa ujumla kwamba chama cha CUF kitatumia nguvu, uwezo, juhudi
na maarifa yake yote kuhakikisha kwamba inaulinda UKAWA ambao unaonekana kuwa
ni mwiba kwa CCM.
Profesa
Lipumba amejiuzulu wadhifa wa uwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF kufuatia
kile alichoeleza kuwa ni kutokana na dhamira na nafasi yake kumsuta kwa kuwa
katika umoja wao wa katiba ya wananchi UKAWA wameshindwa kuzingatia tunu za
taifa ambazo ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji.
0 comments :
Post a Comment