TUMA HABARI YOYOTE ULIYONAYO KWENDA zimetokelezea@gmail.com AU Whatsapp No 0716790749

Vyombo vya habari ni moja ya nyenzo muhimu katika jamii si tu! Katika kuhabarisha na kuburudisha bali hata katika kuielimisha jamii yenyewe. Vyombo vya habari ni muhimili wa nne wa taifa badala ya ile mitatu ambayo ni baraza la utendaji linaloongozwa na raisi, mahakama na bunge.
Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya vyama vya siasa na wanasisa kuvitumia vibaya vyombo vya habari wakati uchaguzi mkuu unapokaribia. Wanafanya hivyo ili kutimiza azma yao ya kuingia madarakani. Kwa mfano vyombo vya habari hutumika kueneza propaganda za wagombea wa chama kimoja zaidi na kuwachafua wa chama chengine. Kwa mfano TBC na ZBC ambavyo vyote vinamilikiwa na serikali, hujikita zaidi katika kutoa taarifa za chama tawala (CCM) zaidi kuliko vyama vyengine vya upinzani. Hii si haki na ni ukiukwaji mkubwa wa demokrasia.
Kwa bahati mbaya sana baadhi ya vyombo hivyo hudiriki kuyatekeleza hayo si kwa matakwa yao binafsi bali ni kutokana na ushawishi mkubwa unaotoka upande wa wagombea na chama husika. Mara nyingi ushawishi huo unatokana na fedha ambazo vyombo vya habari hupokea kutoka kwa wanasiasa wanaosaka madaraka kwa udi na uvumba kiasi cha kupelekea vyombo hivyo kukiuka maadili yake.
Kuna wakati vyombo vya habari hudiriki hata kuyaficha maovu yaliyofanywa na chama Fulani iwe ni CCM, CUF au CHADEMA, kwa kuyafunika maovu hayo kwa guo la uzuri na wema (Propaganda). Kufanya hivyo ni kuwayumbisha wananchi na ukiukwaji mkubwa wa misingi ya kimaadili kwa vyombo hivyo.
Kazi kubwa ya vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu ni kutoa elimu kwa wapiga kura ambayo itapelekea wao kufanya maamuzi sahihi juu ya mustakbali wa taifa lao kwenye uchaguzi mkuu kupitia sanduku la kura. Inafaa tukumbuke kuwa asilimia kubwa ya wapiga kura hawana elimu ya kutosha juu masuala ya uchaguzi, hivyo basi ni wajibu wa vyombo vya habari kuhakikisha kuwa vinatekeleza wajibu wake wa kuwaelimisha wananchi hao badala ya kuwapotosha.
Elimu kwa wapiga kura ni muhimu sana kwa taifa lolote lile lenye kufuata misingi ya kidemokrasia. Miongoni mwa faida kubwa ya elimu hiyo ni kuwafanya wapiga kura hao wake kwa waume kuweza kuzitambua haki zao za msingi sambamba na mfumo mzima wa siasa uliopo. Kuyatambua hayo kutawafanya wao wajue mtu gani wa kumchagua wakati wa kupiga kura.
Pia inafaa wananchi waelezwe ni kwa namna gani serikali iliyopo madarakani  imetekeleza matakwa na maagizo yao waliyowatuma kwa viongozi wao? Sambamba na hilo vyombo vya habari viangaze matendo yote yaliyofanywa na viongozi wakati wa utawala wao (watchdog role). Kwa mfano katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Jakaya Kikwete kuna mambo mengi ambayo yamefanyika ikiwa ni kinyume na matakwa ya wananchi walio wengi. Hivyo basi vyombo vya habari havina budi kulifafanua hilo.
Ni wajibu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa ajili wa wananchi (Public service) badala ya kufanya kazi ya chama kwa manufaa ya chama (Party service). Kufanya hivyo itapelekea kuwa na vyombo vya habari bora na imara katika taifa letu.
Khelef Nassor Al-riyamy
0772274011/ 0718920331
Zanzibar.

0 comments :

 
Top